Hamia kwenye habari

Ndugu 12 waliofungwa mwaka wa 2012 kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wakiwa na mawakili wao (walio katikati) Januari 2019

DESEMBA 9, 2019
ARMENIA

Armenia Iliwahukumu Kimakosa Ndugu 22 kwa Kukataa Kujiunga na Jeshi, Yasema ECHR

Armenia Iliwahukumu Kimakosa Ndugu 22 kwa Kukataa Kujiunga na Jeshi, Yasema ECHR

Desemba 5, 2019, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa uamuzi ambao haukupingwa wa kuunga mkono Mashahidi wa Yehova 22 wanaoishi nchini Armenia, waliokuwa wamefungwa isivyo haki kwa kukataa kujiunga na jeshi. ECHR iliamua kwamba nchi hiyo inapaswa kuwalipa zaidi ya dola 267,000. Hicho ndicho kiwango cha juu zaidi cha pesa ambacho ECHR imewahi kusema ndugu zetu walipwe katika kesi inayohusu kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Mnamo 2012, ndugu hao walifungwa kwa kukataa utumishi wa kijeshi na utumishi wa badala wa kiraia (ACS). Ndugu hao walikataa utumishi wa badala wa kiraia kwa sababu wakati huo, ulikuwa chini ya uangalizi wa jeshi na haukuwa wa kiraia. Hivyo, ni ndugu wawili tu kati yao ambao hawakuwa wamefungwa kabla ya mwaka 2013, serikali ya Armenia ilipoanzisha utumishi badala ambao kwa kweli ni wa kiraia na kuacha kuwafunga ndugu zetu walipokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Uamuzi uliofanywa na ECHR Desemba 5 ulitegemea ushindi ambao Mashahidi wa Yehova walipata katika mwaka wa 2017, katika kesi ya Adyan na Wengine dhidi ya Serikali ya Armenia. ECHR ilisema kwamba serikali ya Armenia ilipaswa kufanya mapatano na ndugu hao 22 mapema baada ya kesi hiyo. Licha ya kwamba ndugu zetu waliwasihi mara kadhaa, serikali hiyo haikutaka kufanya makubaliano hayo. Kwa hiyo, ECHR ilitoa uamuzi wa kuunga mkono ndugu hao.

Tunafurahi kwamba tangu 2013 serikali ya Armenia imebadili msimamo wake kuhusiana na kukataa kujiunga jeshi kwa sababu ya dhamiri. Ndugu zetu hawafungwi gerezani wala kuandikiwa rekodi za uhalifu kwa sababu ya msimamo wao wa kutounga mkono upande wowote. Kwa miaka saba iliyopita, programu ya utumishi wa badala ya Armenia imekuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine. Hata hivyo, uamuzi wa ECHR wa Desemba 5 umeonyesha serikali ya Armenia inapaswa kuwajibika kwa kuwa ilishindwa kutii sheria ya kimataifa katika mwaka wa 2012.

Kulingana na uamuzi huo, ECHR imeonyesha wazi kwamba itaiadhibu nchi yoyote inayokiuka sheria za kimataifa za haki za kibinadamu. Tunamshukuru Yehova kwa kuwapa ndugu zetu nchini Armenia ushindi mkubwa. Tunasali kwamba uamuzi huu uwasaidie ndugu zetu waweze kukataa kujiunga na jeshi na kupewa utumishi wa badala katika nchi ambazo hazijaanzisha mpango huo kama vile Azerbaijan, Korea Kusini, Uturuki, na Turkmenistan.