Hamia kwenye habari

AGOSTI 22, 2017
AUSTRIA

Mji wa Austria Wawakumbuka Mashahidi wa Yehova 31 Ambao ni Waathirika wa Utawala wa Nazi

Mji wa Austria Wawakumbuka Mashahidi wa Yehova 31 Ambao ni Waathirika wa Utawala wa Nazi

Meya wa Techelsberg, Bw. Johann Koban (katikati) akifunua jiwe la msingi la Techelsberg, pamoja na Peter Stocker (kulia) na gavana wa jimbo la Carinthia, Dakt. Peter Kaiser (kushoto).

SELTERS, Ujerumani—Asubuhi ya Mei 19, 2017, manispaa ya Techelsberg, Austria, ilifanya sherehe ya kuwakumbuka Mashahidi wa Yehova ambao waliuawa au kufungwa katika kambi za mateso za Wanazi. Jiwe la msingi la kumbukumbu lililowekwa wakati wa tukio hilo liliwataja jumla ya Mashahidi 31 kuwa “waathirika wa Utawala wa Nazi katika mji wa Techelsberg na maeneo jirani.”

Programu ilianza kwa waimbaji 60 kuimba wimbo wenye kichwa “Songeni Mbele, Enyi Mashahidi!” bila kutumia ala yoyote ya muziki. Wimbo huo, ambao ulirekebishwa na unaendelea kuimbwa katika ibada za Mashahidi duniani kote, ulitungwa na Erich Frost, Shahidi aliyefungwa na Wanazi katika kambi ya mateso ya Sachsenhausen, wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Baada ya kuimba wimbo huo, wasemaji walitambulishwa ambao walikuwa Bw. Johann Koban (meya wa Techelsberg), Bw. Peter Stocker (mjukuu wa Gregor Wohlfahrt, Sr, mwathirika katika mji wa Techelsberg.), Prof. Peter Gstettner, Prof. Vinzenz Jobst, and Dakt. Peter Kaiser (gavana wa jimbo) na waliwahutubia wahudhuriaji 350 hivi. Tukio hilo lilichapishwa katika magazeti ya habari na stesheni za habari za Austria, ORF 2 na ORF Kärnten.

Prof. Peter Gstettner akiwazungumzia wahudhuriaji.

Wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, Mashahidi 212 kati ya 550 nchini Austria walipelekwa katika kambi za mateso, kwa sababu walionwa kimakosa kuwa tishio kwa serikali ya Kijamaa ya Ujerumani, kwa kuwa hawakuunga mkono upande wowote wa kisiasa na walikataa kutegemeza vita. Katika kambi za mateso, Mashahidi wa Yehova walilazimishwa kuvaa kitambaa cha pembetatu cha rangi ya zambarau ili kuwatambulisha. Jumla ya Mashahidi 154 wa Austria walikufa katika Maangamizi Makubwa ya Wanazi.

Kabla ya kufanyika kwa tukio hilo la ukumbusho, Mashahidi watano kutoka Techelsberg ambao waliuawa na Wanazi (Johann Stossier, Anton Uran, Gregor Wohlfahrt, Sr., Gregor Wohlfahrt, Jr., na Willibald Wohlfahrt) waliorodheshwa kimakosa katika kumbukumbu za vita kama “watu waliopotea.” Prof. Gstettner alifafanua umuhimu wa jiwe hilo la msingi: “Jiwe hili linatupatia historia sahihi, sasa limewekwa katika mahali panapofaa likiwa kumbukumbu ya kudumu ya watu hao, ambao kwa ujasiri mwingi, na kufuata kwa unyoofu wa imani zao, wamethibitisha kwamba kuwa imara kukataa kufuata mapenzi ya mfumo wa wanadamu usio wa haki ni jambo linalokubalika kimaadili, na mwishowe wanakuwa washindi.”

Jiwe la msingi la ukumbusho la Techelsberg kwa ajili ya Mashahidi wa Yehova 31 waliouawa, kufungwa, au kutendewa vibaya kwa njia nyingine na Wanazi wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Kwenye jiwe hilo la msingi kuna nukuu ya shairi lililoandikwa na Franz Wohlfahrt (ona sanduku lililo chini) na orodha ya Mashahidi watano kutoka Techelsberg ambao mwanzoni waliorodhesha kwenye kumbukumbu za vita kuwa “watu waliopotea.”

Johann Zimmermann, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Austria, alisema hivi: “Tunathamini sana matukio kama haya ambayo yanatambua ujasiri na imani ya Mashahidi wa Yehova licha ya mateso makali. Tunatumaini kwamba tukio hili limekuwa likitukumbusha ukatili ambao unaoweza kutokea wakati kikundi cha dini chenye watu wachache kinapoonekana kimakosa kuwa tishio lenye madhara kwa Nchi.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, +1-845-524-3000

Austria: Johann Zimmermann, +43-1-804-53-45

Ujerumani: Wolfram Slupina, +49-6483-41-3110