MEI 2, 2014
CHILE
Moto Mkubwa Wasababisha Uharibifu Jijini Valparaíso, Chile
PUENTE ALTO, Chile—Aprili 13, 2014, moto ulioanzia porini na kuchochewa na upepo mkali uliokuwa ukivuma kutoka Bahari ya Pasifiki ulisababisha uharibifu mkubwa katika jiji la kihistoria la bandarini la Valparaíso, nchini Chile. Watu 15 walipoteza maisha yao na wengine 500 wakajeruhiwa kutokana na moto huo. Nyumba 2,900 ziliharibiwa kabisa, na zaidi ya watu 10,000 walilazimika kuhama makazi yao.
Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Chile inasema kwamba mwanamume mmoja Shahidi aliyezeeka ni miongoni mwa watu waliokufa kutokana na mkasa huo. Isitoshe Mashahidi 89 walipoteza nyumba zao. Wengi wa waliolazimika kuhama wamepata hifadhi katika nyumba za Mashahidi wenzao. Mara moja ofisi ya tawi iliunda halmashauri ya kutoa misaada ambayo inaendelea kuwasaidia walioathiriwa na msiba huo. Vikundi vya wajitoleaji tayari vimeanza kazi ya kusafisha eneo hilo. Ikiwa hali zitaruhusu, wajitoleaji hao wataanza kazi ya kujenga upya nyumba 28 za Mashahidi wenzao ambazo ziliharibiwa na moto huo.
Jason D. Reed, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Chile, anaeleza hivi: “Tumesikitishwa sana kuona jirani zetu wakiteseka kutokana na moto huo. Tunaomboleza kwa sababu ya kumpoteza mwabudu mwenzetu katika kifo, na tunasali kwa ajili wale waliofiwa na marafiki au watu wa familia. Tutaendelea kuwapa msaada wale walioathiriwa ili waweze kukabiliana na majonzi na maumivu yaliyosababishwa na msiba huu.”
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000
Chile: Jason D. Reed, simu +56 2 2428 2600