NOVEMBA 23, 2020
FILIPINO
Kimbunga Vamco Chapiga Sehemu za Filipino Zilizokuwa Zimeathiriwa na Dhoruba
Eneo
Luzon
Janga
Novemba 11, 2020, Kimbunga Vamco (kinachojulikana katika eneo hilo kama Ulysses) kilipiga eneo la Patnanungan katika jimbo la Quezon kisha kikasababisha uharibifu katika maeneo mengi ya Luzon
Kimbunga Vamco ndicho kimbunga cha 21 kuikumba Filipino ndani ya mwaka huu na kusababisha mafuriko makubwa kuliko wakati mwingine wowote
Kimbunga hicho kilitokea majuma mawili hivi baada ya Kimbunga Goni kinachokadiriwa kuwa kimbunga kikubwa zaidi kutokea nchini Filipino tangu 2013. Kilisababisha uharibifu mkubwa sana katika sehemu za Luzon
Dhoruba hizo zilizotokea kwa mfuatano ziliongeza kiwango cha maji kwa njia yenye kuhatarisha katika mabwawa makubwa. Kwa sababu hiyo, wenye mamlaka walilazimika kufungulia maji katika mabwawa hayo na hilo likatokeza mafuriko katika maeneo ambayo hayakuwa yameathiriwa na Kimbunga Vamco
Athari ambazo ndugu na dada zetu wamepata
Zaidi ya familia 600 zililazimika kuacha nyumba zao kwa sababu ya mafuriko. Baadhi ya familia hizo zilipanda juu ya paa za nyumba kwa sababu maji hayo yalipanda juu sana kabla ya kuokolewa
Ndugu mmoja kijana alijeruhiwa kioo kilichovunjika kilipomgonga usoni. Anaendelea kupata nafuu
Uharibifu wa mali
Ripoti ya awali inaonyesha:
Angalau Majumba 6 ya Ufalme na ofisi 1 ya utafsiri zimekumbwa na mafuriko
Angalau nyumba 20 ziliharibiwa
Nyumba 1 iliharibiwa kabisa
Jitihada za kutoa msaada
Waangalizi wa mzunguko na wazee wa eneo hilo walifanya kazi pamoja kuongoza kazi ya awali ya kutoa msaada, kwa kuandaa vitu kama vile chakula, maji, na makao kwa ajili ya waliolazimika kuhama
Familia fulani zimefaulu kurudi nyumbani na kuanza kazi ya kufanya usafi
Halmashauri 3 mpya za Kutoa Msaada zinaongoza katika kazi ya kutoa msaada
Akina ndugu wanachukua tahadhari ili kuhakikisha kazi yoyote ya kutoa msaada inafanywa kulingana na miongozo ya usalama ya COVID-19
Tunajua kwamba Yehova atawategemeza ndugu na dada zetu wakati wa kipindi hiki kigumu. Tunatazamia kwa hamu wakati ambapo watu wote wa Yehova wataishi kwa amani na usalama, bila kuogopa misiba ya asili.—Zaburi 4:8.