NOVEMBA 1, 2016
FILIPINO
Mashahidi Waandaa Misaada Baada ya Vimbunga Viwili Kuikumba Filipino
Mashahidi wa Yehova wanawasaidia waabudu wenzao na watu wengine katika kisiwa cha Luzon, kilichoko kaskazini mwa Filipino walioathiriwa na Kimbunga Sarika (kinachoitwa Karen nchini humo) na Kimbunga Haima (kinachoitwa Lawin nchini humo). Vimbunga hivyo vilitokea Oktoba 16 na 19, 2016. Kimbunga Haima, ni moja kati ya vimbunga vyenye nguvu zaidi ambavyo vimewahi kupiga Filipino tangu Kimbunga Haiyan (kilichoitwa Yolanda nchini humo) kilichosababisha vifo vya watu wengi kilichotokea mwaka wa 2013.
Hakuna yeyote kati ya Mashahidi wa Yehova 200,000 nchini Filipino aliyeuawa wala kujeruhiwa vibaya katika misiba hiyo ya asili. Hata hivyo, ripoti za mwanzoni zinaonyesha kwamba upepo wenye nguvu, mafuriko, na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na Kimbunga Haima yaliharibu angalau nyumba 1,058 za Mashahidi, Majumba ya Ufalme 43, au majengo ya ibada.
Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Filipino iliunda halmashauri ya kuandaa misaada wakati wa msiba katika jiji la Tuguegarao, Luzon, ambayo inakusanya bidhaa za msaada, kama vile chakula na maji safi ya kunywa. Kufikia sasa, malori manane ya bidhaa za msaada yamepelekwa katika maeneo yaliyoathiriwa. Pia, ofisi ya tawi imeanzisha mradi wa kujenga nyumba za muda na vilevile kukarabati nyumba na Majumba ya Ufalme yaliyoharibika.
Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova linasimamia kazi hii ya kutoa msaada wakati wa msiba likiwa katika makao makuu yao, kwa kutumia michango inayotolewa kwa ajili ya kazi ya Mashahidi ya kuhubiri ya ulimwenguni pote.
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, 1-718-560-5000
Filipino: Dean Jacek, 63-2-224-4444