Hamia kwenye habari

Picha ya karibuni ya baadhi ya waathirika katika kesi ya Gabunia

OKTOBA 24, 2017
GEORGIA

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yaridhishwa na Hatua ya Serikali ya Georgia Kukiri Kuwa na Hatia

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yaridhishwa na Hatua ya Serikali ya Georgia Kukiri Kuwa na Hatia

Oktoba 12, 2017, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) imethibitisha kuridhishwa na hatua ya Georgia ya kukiri kwamba ilikiuka haki za Mashahidi kumi wa Yehova. Katika kesi ya Gabunia na wengine dhidi ya Georgia, serikali ilikubali kulipa dola 947 za Marekani kwa kila mtu kama fidia kwa sababu ya kukiukwa kwa haki zao za uhuru wa ibada na kwa sababu ya kubaguliwa kama inavyoelezwa katika Kifungu cha 9 na 14 cha Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu.

Mnamo Septemba 2005, Mashahidi kumi waliwasilisha kesi kwenye Mahakama ya Ulaya kuhusu matukio manne ya kushambuliwa na makundi ya watu ambayo yaliongozwa na Waothodoksi wenye msimamo mkali. Matukio hayo manne yalikuwa sehemu ya kampeni ya mateso ya kidini ambayo yaliongozwa na Serikali dhidi ya Mashahidi wa Yehova nchini Georgia ambayo ilianza Oktoba 1999 hadi Novemba 2003. Maofisa wa serikali walihusika katika mashambulizi hayo ama kwa kushiriki katika vurugu au kushindwa kuwalinda waliofanyiwa vurugu.

Kabla ya uamuzi wa kesi hii ya Gabunia, Mahakama ya Ulaya tayari ilikuwa imetoa hukumu tatu kali dhidi ya nchi ya Georgia. Katika hukumu hizo, Mahakama ya Ulaya ilishutumu serikali kwa kushindwa kulinda haki ya Mashahidi kutokana na vurugu walizokuwa wakifanyiwa katika kipindi hicho. Mahakama hiyo ilifikia mkataa kwamba kupuuzwa kwa jambo hili na maofisa wa kusimamia sheria “kungefanya jamii iamini kwamba wawakilishi wa serikali walishiriki katika uhalifu huu.” Iliendelea kueleza kwamba “wenye mamlaka nchini Georgia walitengeneza mazingira yaliyofanya watu watende uhalifu bila hofu ya kuadhibiwa, na hilo lilichochea mashambulizi mengine dhidi ya Mashahidi wa Yehova nchini kote.” Mahakama ya Ulaya iligundua kwamba “mahakama za nchi hiyo zilifumbia macho matendo ya vurugu yaliyofanywa dhidi ya Mashahidi” na kwamba mahakama hizo za Georgia zilikuwa zikichunguza “kijuujuu na kwa upendeleo” malalamiko ya waathiriwa.

Kwa kutoa taarifa kwamba “inajutia” matendo ya ukiukwaji wa haki, Georgia imeepuka hukumu ya nne ambayo bila shaka ingerudia shutuma za hukumu tatu zilizopita. Leo, Mashahidi wa Yehova nchini Georgia hawashambuliwi na makundi ya watu wala serikali haichochei mateso ya kidini dhidi yao. Sasa wanafurahia uhuru wa ibada.