Hamia kwenye habari

JUNI 22, 2015
GEORGIA

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu Imeridhishwa na Hatua ya Georgia Kukiri kwamba Ilikiuka Haki za Mashahidi wa Yehova

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu Imeridhishwa na Hatua ya Georgia Kukiri kwamba Ilikiuka Haki za Mashahidi wa Yehova

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu (ECHR) imeridhishwa na hatua ya serikali ya Georgia kukiri kwamba iliingilia haki za Mashahidi wa Yehova kuhusu uhuru wao wa kuabudu na kushirikiana. Kesi ya Union of Jehovah’s Witnesses na Wengine dhidi ya Georgia ilihusu hatua ya serikali kufuta usajili wa mashirika mawili ya kisheria yanayotumiwa na Mashahidi wa Yehova. Kufutwa kwa usajili huo kulichangia kuongezeka kwa vitendo vya jeuri dhidi ya Mashahidi tangu mwaka 2001 hadi 2004.

ECHR Yaridhishwa na Hatua ya Serikali ya Georgia Kukiri Kuwa na Hatia

Katika uamuzi wake uliochapishwa Mei 21, 2015, a ECHR ilisema kuwa mnamo Septemba 2014, serikali ilitoa taarifa iliyoeleza kwamba “inajutia matendo ya ukiukwaji” wa haki za Mashahidi wa Yehova. Katika taarifa hiyo serikali ya Georgia ilikubali kwamba kitendo cha kufuta usajili wa mashirika ya kisheria ya Mashahidi katika mwaka 2000 “kilikuwa si cha haki” na kwamba kukosekana kwa sheria zinazofaa kuliondoa uwezekano wa mashirika hayo kusajiliwa.

ECHR imekubali tamko hilo la serikali kuwa msingi wa kumaliza kesi hiyo. ECHR inaona kwamba “kukataa kusajili mashirika ya dini au kubatilisha usajili wake, kunaonyesha kwamba mamlaka inayohusika inakiuka haki ya uhuru wa kuabudu na kushirikiana, na hivyo kuvunja Kifungu cha 9 na 11 cha Mkataba wa Ulaya.” Serikali imekubali kulipa fidia ya euro 6,000.

Kufuta Usajili wa Mashirika ya Kisheria Kwasababisha Mateso

Mashirika mawili ya, Union of Jehovah’s Witnesses na Representation of the Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania (USA) nchini Georgia, yalisajiliwa rasmi mwaka wa 1998. Hata hivyo, mbunge mmoja mwenye uzalendo alitaka Mashahidi wa Yehova wapigwe marufuku nchini Georgia. Baadhi ya viongozi wa dini ya Othodoksi na watu wenye msimamo mkali walimuunga mkono kwa kusambaza habari za uwongo na kuwachochea watu wawatendee kwa jeuri Mashahidi.

Mnamo Aprili 1999, mbunge huyo, akiwakilisha chama chake cha siasa, alifungua kesi ya kuipiga marufuku dini ya Mashahidi wa Yehova na kufuta usajili wa mashirika yao mawili ya kisheria kwenye Mahakama ya Mkoa ya Isani iliyoko Tbilisi. Kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa Juni 1999, makasisi wa Othodoksi na watu wanaowaunga mkono walikuwa ndani ya mahakama. Nje ya mahakama, Vasili Mkalavishvili aliyeachishwa ukasisi na kanisa la Othodoksi pamoja na wafuasi wake walichoma hadharani machapisho ya Mashahidi wa Yehova.

Baada ya kuchunguza ushahidi, mahakama ya Isani-Samgori ilitupilia mbali malalamiko yasiyo na msingi ya mbunge huyo. Lakini aliamua kukata rufaa. Juni 26, 2000, mahakama ilibatilisha uamuzi wa Mahakama ya Mkoa na kuagiza usajili wa mashirika ya kisheria ya Mashahidi ufutwe. Baada ya uamuzi huo, wafuasi wenye msimamo mkali wa Othodoksi walitumia nafasi hiyo kupanga matukio ya kuwashambulia Mashahidi. Februari 22, 2001, Mahakama Kuu ya Georgia iliunga mkono uamuzi wa kufuta usajili wa mashirika ya Mashahidi kwa madai ya kutokuwa na sheria zinazofaa. Baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa mahakama za nchini mwao, Agosti 16, 2001 Mashahidi wa Yehova waliamua kupeleka kesi yao (ECHR).

Baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu, mateso na jeuri dhidi ya Mashahidi yaliongezeka sana, jambo lililosababisha washambuliwe kila mara. Mara nyingi, vyombo vya ulinzi na usalama vilishindwa kuwalinda Mashahidi na, hata nyakati nyingine, vilishiriki kuwashambulia. Mashahidi wengi walijeruhiwa vibaya. Wafuasi wa dini wenye msimamo mkali walivamia mikutano ya kidini ya Mashahidi, walipora na kuchoma moto nyumba zao, waliwaibia au kuharibu mali zao, na kuchoma machapisho ya kidini. Wenye mamlaka waliwazuia Mashahidi wasiingize machapisho na kisha wakawanyang’anya machapisho yaliyoingizwa wakati uliopita. Pia, wenye mamlaka waliwazuia Mashahidi kutumia majumba ya kukodi kwa ajili ya ibada. Kwa sababu ya kuongezeka kwa mateso na serikali kushindwa kuwalinda, Mashahidi wa Yehova nchini Georgia walipeleka kesi zao ECHR wakikazia jinsi wanavyotendewa isivyo haki na jinsi vyombo vya usalama vinavyoshiriki kuwatesa. Mashahidi wa Yehova wameshinda kesi mbili kati ya zile walizopeleka ECHR. b

Kadiri hali ilivyokuwa nzuri nchini Georgia, Mashahidi waliweza kusajili upya mashirika yao ili waweze kumiliki mali na kushughulikia mambo ya kisheria. Wakati huo, wenye mamlaka walimkamata na kumfunga Mkalavishvili, kiongozi wa mashambulizi dhidi ya Mashahidi, pamoja na baadhi ya wafuasi wake. Mateso makali dhidi ya Mashahidi yaliisha mwaka 2004.

Hali ya Wakati Huu

Ingawa serikali ya Georgia imejitahidi kuwatendea vizuri Mashahidi wa Yehova, bado wanakabili usumbufu wa hapa na pale katika shughuli zao za dini. Ripoti ya hivi karibuni iliyopelekwa kwenye Shirika la Ulaya la Usalama na Ushirikiano inaonyesha kwamba visa 63 vya uhalifu mbaya vilifanywa dhidi ya Mashahidi wa Yehova mwaka 2014, nchini Georgia.

Michael Jones, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Georgia, alisema hivi: “Tunashukuru sana kwamba Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu imetambua matendo yasiyo ya haki waliyofanyiwa Mashahidi katika miaka iliyopita. Tunafurahi kuona serikali ya Georgia ikifuata haki za binadamu, na tunatumaini uamuzi uliofanywa karibuni, pamoja na maamuzi mengine yaliyotolewa na Mahakama, yatasaidia Mashahidi wa Yehova watendewe vizuri na kupata uhuru mkubwa wa ibada nchini Georgia.”

a ECHR ilitoa uamuzi Aprili 21, 2015, lakini ilichapisha uamuzi huo mwezi mmoja baadaye.

b Washiriki wa Kutaniko la Gldani la Mashahidi wa Yehova na Wengine dhidi ya Georgia, na. 71156/01, 3 Mei 2007; na Begheluri dhidi ya Georgia, na. 28490/02, 7 Oktoba 2014.