FEBRUARI 9, 2016
KOREA KUSINI
Kamati ya Haki za Kibinadamu Yaisihi Korea Kusini Itambue Haki ya Kukataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri
Baada ya uchunguzi wa kina wa rekodi ya haki za kibinadamu nchini Korea Kusini, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu ilitoa kauli yake ya mwisho Novemba 3, 2015. Kamati hiyo ilitaja maendeleo ambayo yamefanywa na Korea Kusini katika suala la haki za kibinadamu lakini kihususa ikataja nchi hiyo ilivyoshindwa kutii maamuzi ya awali ya Kamati hiyo kuhusu haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.
Haki ya Kuwa na Uhuru wa Dhamiri na Dini
Ingawa haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri inatambulika kimataifa kuwa haki ya msingi ya kibinadamu, bado Korea Kusini inaendelea kuwaadhibu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Tangu 1950, miaka 36,000 hivi ndiyo jumla ya miaka ambayo Mashahidi 18,000 wa Yehova wamehukumiwa kufungwa gerezani nchini humo.
Ripoti ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu imeisihi serikali ifanye yafuatayo:
Iwaachilie mara moja wote waliofungwa gerezani kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.
Ifute rekodi za uhalifu za waliofungwa gerezani kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, iwalipe fidia, na kuhakikisha habari zao za kibinafsi hazitolewi kwa umma.
Itambue kisheria haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na kuandaa programu ya utumishi wa badala wa kiraia kwa ajili ya wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.
Daraka la Kutekeleza Makubaliano ya Mkataba
Tangu 2006, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu imetoa Maamuzi matano dhidi ya serikali ya Korea Kusini kwa kosa la kutopitisha sheria ya kulinda haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na kwa kuwaadhibu wale wanaolindwa na haki hiyo. a Ripoti ya karibuni ya Kamati hiyo kwa mara nyingine imetaka serikali ya Korea Kusini “kuweka mipango ya utekelezaji na kuchukua hatua zinazofaa ili kutimiza kikamili Maamuzi ya Kamati,” kutia ndani kutekeleza kikamili Maamuzi ya awali yaliyopitishwa na Kamati hiyo.
Baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo ya Kamati, Seong-ho Lee, ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Korea, alikubali kwamba ukiukwaji wa haki za kibinadamu zilizotajwa katika ripoti umetokea. Katika maelezo aliyotoa kuishauri serikali itekeleze mapendekezo ya Kamati, Bw. Lee alimalizia hivi: “Serikali ina daraka la kutekeleza kikamili ICCPR [Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa].”
Kwa kuwa Korea Kusini ni mojawapo ya nchi zilizotia sahihi mkataba huo, ina jukumu la kulinda haki zinazotolewa na ICCPR. Kwa kuwa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu inasimamia utekelezwaji wa ICCPR na inatambua haki ya kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, Korea Kusini itakuwa ikiendelea kukiuka mkataba huo hadi itakapotekeleza Maamuzi na mapendekezo ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu.
Ripoti hiyo ya karibuni ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu inaongezea uzito malalamiko kutoka katika mataifa mbalimbali kuhusu jinsi Korea Kusini inavyowatendea wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Wengi waliopo nchini Korea Kusini na sehemu nyingine watatazama kwa makini kuona itikio la serikali baada ya kuombwa itekeleze daraka lake.
a Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu inatoa hukumu zinazojulikana kuwa Maamuzi baada ya kuchunguza ikiwa nchi fulani imekiuka haki zinazotelewa na ICCPR. Maamuzi matano yaliyotolewa dhidi ya Korea Kusini ya ukiukwaji wa Kifungu cha 18, “haki ya kuwa na uhuru wa kufikiri, wa dhamiri, na wa kidini,” ni Na. 1321-1322/2004, Yeo-bum Yoon and Myung-jin Choi v. Republic of Korea, Novemba 3, 2006; Na. 1593-1603/2007, Eu-min Jung et al. v. Republic of Korea, Machi 23, 2010; Na. 1642-1741/2007, Min-kyu Jeong et al. v. Republic of Korea, Machi 24, 2011; Na. 1786/2008, Jong-nam Kim et al. v. Republic of Korea, Oktoba 25, 2012; Na. 2179/2012, Young-kwan Kim et al. v. Republic of Korea, Oktoba 15, 2014.