Hamia kwenye habari

JULAI 25, 2014
KROATIA

Mashahidi Watoa Misaada Katika Nchi za Balkani

Mashahidi Watoa Misaada Katika Nchi za Balkani

ZAGREB, Kroatia—Halmashauri za kutoa misaada za Mashahidi waliojitolea, wakisaidiwa na wawakilishi kutoka katika ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova iliyoko Ujerumani, walichukua hatua ili kuwasaidia waathiriwa wa mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea Bosnia-Herzegovina, Kroatia, na Serbia. Mvua kubwa sana iliyoanza Mei 13 hadi 15, 2014 katika nchi za Balkani, ilisababisha mafuriko makubwa sana na maporomoko 3,000 hivi ya ardhi.

Mara moja, halmashauri za kutoa misaada ziliandaa huduma za usafiri, chakula, nguo, na makao ya muda kwa walioathiriwa. Ingawa hakuna Shahidi hata mmoja wa Yehova aliyekufa wala kujeruhiwa katika msiba huo, nyumba zao 14 hivi ziliharibiwa kabisa au kubomolewa. Nyumba moja ya Ibada ya Mashahidi iliharibiwa pia. Sasa halmashauri hizo zinafanya mipango ili nyumba zilizoharibiwa zirekebishwe, na pia kuwajengea nyumba za muundo rahisi wale wasio na makao.

Josip Liović, msemaji wa ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Kroatia, anasema hivi: “Tunafurahi kusikia kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa katika makutaniko yetu kwenye msiba huo mbaya, hata hivyo, tunawasikitikia wale waliofiwa na washiriki wa familia na rafiki zao. Kotekote katika maeneo ya Balkani, tunajitahidi kwa njia ya pekee kuwafariji jirani zetu. Pia, tunawashukuru rafiki zetu kutoka Ujerumani waliofika hapa ili kutusaidia kutoa misaada itakayohitajiwa katika wiki na miezi ijayo.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Croatia: Josip Liović, simu +385 91 5336 511

Serbia: Daniel Domonji, simu +381 11 405 99 00