MACHI 1, 2016
KYRGYZSTAN
Je, Waliotendewa Kikatili na Polisi Jijini Osh Watapata Haki Yao?
Kwa mara ya tatu, Mwendesha-Mashtaka Mkuu wa Kyrgyzstan ameagiza Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka wa Jiji la Osh ifikirie kuanza upelelezi wa mashtaka dhidi ya maofisa kumi wa polisi. Polisi hao walivamia kinyume cha sheria mikutano ya kidini ya Mashahidi wa Yehova mnamo Agosti 2015 na kuwapiga sana baadhi ya wahudhuriaji. Licha ya kuwa na uthibitisho wa wazi wa mwenendo huo mpotovu wa polisi, Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka wa Jiji la Osh imekataa kufanya upelelezi wa kesi hiyo.
Polisi Wavamia Mkutano Kinyume cha Sheria na Kupiga Watu Vikali
Jumapili asubuhi, Agosti 9, 2015, maofisa kumi wa Idara ya 10 a ya kikosi cha polisi cha Osh walivamia mkutano wa kidini kwenye mkahawa uliokuwa umekodishwa ambapo watu zaidi ya 40 walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya ibada. Mmoja wa maofisa hao alimpigia makelele Nurlan Usupbaev, aliyekuwa akiongoza ibada, asimamishe ibada hiyo mara moja kwa sababu eti ilikuwa ikifanywa “kinyume cha sheria.” Mara kadhaa polisi hao walitishia kuwapiga risasi wote waliohudhuria. Mhudhuriaji mmoja aitwaye Tynchtyk Olzhobayev alipojaribu kurekodi video ya vitendo hivyo vibaya vya polisi, alichukuliwa na polisi hao na kupelekwa kwenye chumba kingine na kupigwa kikatili.
Maofisa hao wakawafikisha Mashahidi kumi wa kiume katika kituo cha polisi. Kisha wakawapiga sita kati yao na kuwakaba kooni watatu, kutia ndani Bw. Usupbaev. Wanaume hao kumi waliachiliwa siku hiyohiyo, na waliojeruhiwa sana walienda hospitalini kwa ajili ya uchunguzi.
Baada ya siku mbili, mnamo Agosti 11, maofisa wawili waitwao Kozhobek Kozubayev na Nurbek Sherikbayev—ambao ndio waliosimamia uvamizi na upigaji wa waliohudhuria ile ibada—walimkamata Bw. Usupbaev kwa shtaka la kufanya utendaji wa kidini kinyume cha sheria. Kesi yake ilipangwa kusikilizwa Agosti 20 na 21 katika Mahakama ya Jiji la Osh.
Mahakama Zatetea Haki ya Mashahidi ya Kuabudu
Kesi hiyo ilipokuwa ikisikilizwa, mwakilishi wa Idara ya 10 alisema kwamba mikutano hiyo ya kidini ya Agosti 9 ilifanywa kinyume cha sheria kwa sababu Mashahidi wa Yehova hawajasajiliwa jijini Osh. Pia, upande wa mwendesha-mashtaka ulidai kwamba kuwapo kwa watoto katika mkutano huo kulikiuka sheria ya kidini ya Kyrgyzstan, inayokataza kuandikisha watoto kwenye mashirika ya kidini.
Agosti 21, hakimu wa Mahakama ya Jiji la Osh hakumkuta na hatia Bw. Usupbaev ya utendaji wa kidini kinyume cha sheria. Mahakama ilifikia mkataa kwamba kesi dhidi yake ifutwe kwa sababu hakukuwa na uthibitisho wa kwamba alishiriki katika utendaji wa kidini kinyume cha sheria au kwamba “aliandikisha” watoto wajiunge na dini.
Mwendesha-Mashtaka wa Jiji la Osh alikata rufani kwenye Mahakama ya Mkoa ya Osh, akipinga kuachiliwa huru kwa Bw. Usupbaev. Mahakama ya mkoa ilikataa rufani ya mwendesha-mashtaka huyo na kukubaliana na maamuzi ya mahakama ya mwanzo ya kumwachilia Bw. Usupbaev. Mahakama ya mkoa ilieleza wazi tena kwamba Mashahidi wa Yehova ni dini iliyosajiliwa kisheria nchini Kyrgyzstan. Mahakama iliendelea kusema kwamba Baraza la Katiba la Mahakama Kuu tayari ilitamka kwamba kipengele cha sheria ya Kyrgyzstan kinachotaka dini zisajiliwe tena katika kila jiji ni kinyume cha katiba ya nchi. b Hata hivyo, tayari mwendesha-mashtaka amekata rufani kwenye Mahakama Kuu, na Mahakama itasikiliza kesi hiyo Machi 2, 2016.
Mwendesha-Mashtaka Aamriwa Kuwapeleleza Polisi
Kesi yake ilipokuwa ikiendelea kusikilizwa, Bw. Usupbaev pamoja na wengine waliopigwa kikatili na polisi mnamo Agosti 9 walifungua kesi ya malalamiko kwenye Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka wa Jiji la Osh. Waliomba kesi za mashtaka ya uhalifu zifunguliwe dhidi ya polisi kumi waliohusika katika vitendo hivyo. Huo ukawa mwisho wa kutoa maombi ya kufungua kesi. Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka wa Jiji la Osh ilikataa mara tatu kufungua kesi hiyo, na kila mara waathiriwa walikata rufani kwa Mwendesha-Mashtaka Mkuu. Mara mbili Mwendesha-Mashtaka Mkuu alipinga maamuzi ya Mwendesha-Mashtaka wa Jiji la Osh na kumwagiza afungue kesi hiyo. Hata hivyo, baada ya kupokea rufani ya tatu, Mwendesha-Mashtaka Mkuu hakuifungua kesi hiyo mwenyewe badala yake akairudisha kwa Mwendesha-Mashtaka wa Jiji la Osh ili afanye uamuzi. Mwendesha-Mashtaka Mkuu alifanya hivyo Januari 21, 2016 na hilo linatokeza shaka ikiwa kweli wanaume hao kumi watawahi kupata haki yao.
Mashahidi wa Yehova nchini Kyrgyzstan wanashukuru kwamba wamesajiliwa kitaifa na wanathamini maamuzi ya karibuni ya mahakama za Osh. Wanashukuru kwamba kuna mahakimu wanaopenda haki na wanaotetea kwa ujasiri uhuru wa kidini kwa kufuata sheria na kuunga mkono maamuzi ya serikali ya kutetea uhuru wa ibada na wa imani. Hata hivyo, kitendo cha maofisa wa serikali kutowahukumu polisi waliofanya vitendo hivyo kinyume cha haki kinawahangaisha. Mashahidi wa Yehova wanaisihi Ofisi ya Mwendesha-Mashtaka Mkuu ichukue hatua mara moja ya kuwafungulia mashtaka waliofanya kitendo hicho cha jeuri.
a Idara ya 10 ni tawi la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kyrgyzstan.
b Uamuzi wa Septemba 4, 2014. Ona makala “Mahakama Kuu ya Kyrgyzstan Yatetea Uhuru wa Kidini wa Mashahidi wa Yehova.”