SEPTEMBA 29, 2022
UGIRIKI
Miaka 100 ya Ofisi ya Tawi Nchini Ugiriki
Miaka 100 tangu ofisi ya tawi ya kwanza kuanzishwa nchini Ugiriki ilitimia Oktoba 6, 2022.
Katika siku zetu, habari njema ilianza kuhubiriwa nchini Ugiriki mwaka wa 1905. Mashahidi wa Yehova walihubiri ujumbe wa Biblia kwa bidii na katika mwaka wa 1922, Ndugu Joseph F. Rutherford alifungua ofisi ya tawi ya kwanza jijini Athens. Ndugu Athanassios Karanassios aliwekwa rasmi kuwa mwakilishi wa kwanza wa tawi. Ofisi hiyo ya tawi ilianza kuchapisha vitabu vya Kigiriki mwaka wa 1936. Miaka miwili baadaye, serikali iliweka sheria ambayo iliwakataza watu kuwashawishi wengine wageuze imani yao. Ndugu Karanassios alikamatwa kwa madai hayo, mwaka wa 1939. Kiwanda cha uchapishaji kikafungwa na mali ya tengenezo ikataifishwa kwa miezi kadhaa. Baadaye, nchi ya Ugiriki ilipoingia katika Vita vya Pili vya Ulimwengu, sheria ya kijeshi ilitangazwa, hivyo basi machapisho yetu yakapigwa marufuku na ofisi ya tawi ikafungwa.
Vita vilipoisha katika mwaka wa 1945, akina ndugu waliokuwa wakiongoza waliweza kupanga kazi ya kuhubiri upya mara tu baada ya marufuku kuondolewa. Miaka miwili baadaye, Ndugu Nathan H. Knorr aliwatembelea akina ndugu nchini Ugiriki na akafanya mipango ya kuanzisha ofisi mpya ya tawi katika mtaa wa Tenedou, jijini Athens. Ni wazi kwamba Yehova alibariki jitihada hizo. Kufikia mwaka wa 1951, kulikuwa na wahubiri 3,368 nchini humo, yaani, ongezeko la asilimia 26 kwa kulinganisha na mwaka uliotangulia.
Oktoba 1954, akina ndugu waliweka wakfu makao mapya ya Betheli katika mtaa wa Kartali, jijini Athens. Kazi ya kuhubiri ilisonga mbele licha ya mateso. Katika mwaka wa 1967, kulikuwa na mapinduzi ya kijeshi nchini Ugiriki na wanajeshi wakaanza kutawala. Kwa mara nyingine tena, mikutano ya kutaniko na kazi ya kuhubiri ilipigwa marufuku.
Ndugu Michalis Kaminaris na mke wake, Eleftheria, walitumikia Betheli katika kipindi hicho cha marufuku. Ndugu Kaminaris anaeleza: “Wakati wa marufuku, kiwanda chetu cha uchapishaji kilichokuwa Betheli kilifungwa. Kwa hiyo, nyumba ambamo mimi na Eleftheria tuliishi nje ya jiji la Athens ikawa kama kiwanda kidogo. Eleftheria alipiga chapa nakala za Mnara wa Mlinzi akitumia taipureta nzito. Aliweka karatasi kumi kwa pamoja kwenye taipureta kisha alibonyeza kwa nguvu sana herufi kwenye taipureta ili afaulu kuchapa vizuri na maneno yaonekane. Nami nilikusanya kurasa hizo na kuzishona pamoja. Kila jioni tulifanya kazi hiyo hadi saa sita usiku. Kulikuwa na ofisa wa polisi aliyeishi orofa ya chini, na tungali tunashangaa kwa nini hakuwahi kutushuku.”
Idadi ya wahubiri iliendelea kuongezeka licha ya marufuku. Marufuku ilipoondolewa katika mwaka wa 1974, kwa mara nyingine tena, ofisi kubwa zaidi ya tawi ilihitajika. Kadiri miaka ilivyozidi kusonga, idadi ya wahubiri nchini Ugiriki iliendelea kuongezeka na kwa sababu hiyo, ofisi ya tawi ikaendelea kupanuka. Ofisi ya tawi inayotumika sasa hivi, iko Drapetsona, Piraeus, na iliwekwa wakfu Novemba 18, 2018. Kwa sasa, kuna wahubiri 27,752 wanaotumikia nchini Ugiriki.
Licha ya vita, mateso, na kupigwa marufuku mara kadhaa kumekuwa na ongezeko nchini Ugiriki kwa miaka 100 hivi. Hilo linathibitisha kwamba hakuna kitu kinachoweza kumzuia Yehova ‘kuharakisha kazi hiyo kwa wakati wake.’—Isaya 60:22.