Hamia kwenye habari

MEI 25, 2023
UGIRIKI

Uamuzi wa Mahakama ya Ulaya Katika Kesi ya Kokkinakis v. Greece Unaendelea Kutumika Miaka 30 Baadaye

Uamuzi Uliosaidia Kulinda Haki za Msingi za Kidini Barani Ulaya

Uamuzi wa Mahakama ya Ulaya Katika Kesi ya Kokkinakis v. Greece Unaendelea Kutumika Miaka 30 Baadaye

Mei 25,2023, inahitimisha miaka 30 tangu uamuzi katika kesi ya Kokkinakis v. Greece ulipotolewa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR). Kulingana na wataalamu wa sheria, uamuzi huo ni mojawapo ya maamuzi muhimu zaidi yaliyowahi kutolewa na Mahakama ya ECHR. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa mahakama ya ECHR kuitia nchi yoyote hatiani kwa sababu ya kukiuka uhuru wa kidini. Tangu mwaka wa 1993, uamuzi huo umekuwa msingi thabiti wa kulinda haki za kidini katika nchi 46 zilizo katika Baraza la Ulaya. Kwa kuwa baadhi ya serikali zenye nguvu kama vile Urusi, zimeshambulia haki yetu ya kuwaeleza wengine kwa uhuru kuhusu imani yetu, uamuzi uliofanywa katika kesi ya Kokkinakis ni muhimu sana leo ili kutetea haki hizo.

Kufikia leo, tovuti rasmi ya Baraza la Ulaya inarejelea kesi ya Kokkinakis inapofafanua ulinzi unaoandaliwa katika Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu. Kesi hiyo inafundishwa katika shule za sheria na pia inatajwa katika kesi za rufaa zinazowasilishwa kwenye Mahakama ya Ulaya.

Uamuzi wa Kokkinakis unafafanua kwamba “kutoa ushahidi kwa maneno na matendo kuna uhusiano wa karibu sana na imani ya kidini.” Isitoshe, uamuzi huo pia ulitoa uhakikisho kwamba “uhuru wa kudhihirisha dini ya mtu . . . unatia ndani haki ya kujaribu kumsadikisha jirani yake, kwa mfano kupitia ‘kumfundisha.’”

Hakimu De Meyer, mmoja kati ya mahakimu tisa wa ECHR waliosikiliza kesi hiyo, alitoa maoni haya: “Kuwahamasisha watu wabadili dini, kwa maneno mengine ni ‘kuwa na bidii ya kueneza imani,’ na huo si uhalifu: ni njia—iliyo halali kabisa—ya ‘kudhihirisha imani [ya mtu].’”

Uamuzi huo wa kihistoria ulihitimisha pambano la kisheria la miaka 50 la Ndugu Minos Kokkinakis. Serikali ya Ugiriki ilimkamata Minos mwaka wa 1938 kwa sababu ya kuvunja sheria iliyokataza “kuwahamasisha watu kubadili dini.” Sheria hiyo ilikuwa imewekwa na dikteta Ioannis Metaxas, ambaye alikuwa mtawala wa Ugiriki. Minos, alikuwa na miaka 30 wakati huo, na alikuwa moja kati ya Mashahidi wa Yehova 19,147 waliokamatwa chini ya sheria hiyo kuanzia mwaka wa 1938 hadi 1992. Isitoshe, katika kipindi hicho, Mashahidi wa Yehova waliteswa, walidhalilishwa, na kutendewa kwa jeuri.

Hata hivyo, Minos aliendelea na huduma yake kwa ujasiri. Kwa sababu hiyo, alikamatwa zaidi ya mara 60, akapelekwa mbele ya mahakama za Ugiriki mara 18, akatumikia zaidi ya miaka sita gerezani na katika visiwa vilivyotumiwa kama magereza, na kutozwa faini mara kadhaa.

Hatimaye, katika mwaka wa 1993 mahakama ya ECHR ilitangaza kwamba Minos hakuwa na hatia na kwamba nchi ya Ugiriki ilikuwa imekiuka uhuru wa kidini wa Minos. Uamuzi huo ulipotolewa, Minos alikuwa na miaka 84. Mahakama hiyo iliagiza Minos alipwe fidia kwa sababu ya miaka mingi aliyokuwa ameteseka na pia kwa sababu ya gharama za kesi. Minos alihamia eneo la Crete na aliishi huko hadi alipokufa mwaka wa 1999 akiwa na umri wa miaka 90.

Hakimu De Meyer alisema kwamba Minos hakuwa mhalifu lakini “alifungwa kwa sababu tu alionyesha bidii kama hiyo, lakini hakuwa amefanya kosa lolote.”

Philip Brumley, Wakili Mkuu wa Mashahidi wa Yehova anasema hivi kuhusu umuhimu wa uamuzi huo wa kihistoria katika kesi nyingine: “Uamuzi wa Kokkinakis uliweka msingi wa haki ya mtu kuwaeleza wengine kuhusu imani yake kwa amani. Uamuzi huo wa ECHR ndio unaotajwa zaidi na kutegemewa zaidi inapohusu uhuru wa kidini, hata nje ya Ulaya.”

Tunamshukuru sana Yehova kwa ushindi huo mkubwa katika kesi ya Kokkinakis na kwa msingi mzuri unaoandaa kwa ajili ya kesi nyingine. Tunathamini hekima na mwongozo anaotupa tunapoendelea “kuitetea na kuithibitisha kisheria habari njema.”​—Wafilipi 1:7.