Hamia kwenye habari

APRILI 7, 2014
UJERUMANI

Richard Rudolph, Aliyeokoka Kambi za Mateso, Amekufa Akiwa na Miaka 102

Richard Rudolph, Aliyeokoka Kambi za Mateso, Amekufa Akiwa na Miaka 102

SELTERS, Ujerumani—Richard Rudolph, Shahidi wa Yehova aliyeokoka kambi tano za mateso za Wanazi na kufungwa gerezani chini ya utawala wa Kikomunisti, alikufa Januari 31, 2014. Alikuwa na umri wa miaka 102.

Baada ya Wanazi kuanza kutawala mwaka 1933, kazi ya Mashahidi wa Yehova ilipigwa marufuku katika maeneo mengi nchini Ujerumani. Kwa sababu hiyo, jumla ya Mashahidi 11,300 walifungwa na Wanazi, 4,200 kati yao wakifungwa katika kambi za mateso, kutia ndani Bw. Rudolph. Mashahidi 1,500 hivi walikufa. Chini ya utawala wa Wanazi, Bw. Rudolph alifungwa kwa miaka tisa na kuokoka kambi tano za mateso, kutia ndani kambi zilizojulikana kwa ukatili na mateso makali za Sachsenhausen na Neuengamme, ambapo watu 300,000 walifungwa humo na wengine 140,000 wakapoteza maisha yao.

Richard Rudolph (juu ya paa, mbali kulia) alikuwa mmoja wa wafungwa waliolazimishwa kujenga kambi ya mateso ya Neuengamme mwaka wa 1940.

Mwaka wa 1944, Bw. Rudolph alihamishwa na kupelekwa katika kambi ya Neuengamme, huko Salzgitter-Watenstedt. Kwa sababu ya imani yake ya kidini, alikataa kufanya kazi yoyote iliyohusiana na kutengeneza silaha, na jambo hilo lingefanya auawe. Hata hivyo, ofisa mmoja wa Hitler mwenye urafiki na aliyevutiwa na imani ya Rudolph, alimficha katika lori la kusafirishia chakula, na hivyo akaokoka.

Baada ya Vita vya Pili vya Ulimwengu, Rudolph aliendelea na shughuli zake za kidini akiwa Shahidi wa Yehova katika eneo lililodhibitiwa na Wasovieti (Soviet Occupation Zone), ambalo baadaye lilikuja kuitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani (GDR). Alikamatwa tena mwaka wa 1950 na kufungwa gerezani. Kwa ujumla, alifungwa kwa zaidi ya miaka 19 kwa sababu ya imani yake ya kidini.

Ann-Jacqueline Frieser na Richard Rudolph, ambaye simulizi lake la maisha lilishinda tuzo mwaka wa 2009.

Kwa miaka mingi, Richard Rudolph aliazimia kuwaambia wengine mambo aliyokuwa amejifunza katika Biblia, kutia ndani mambo aliyojifunza katika miaka ya hapo awali kuhusu athari za kuwabagua watu. Mwaka wa 2009, mwanafunzi kutoka Ujerumani anayeitwa Ann-Jacqueline Frieser, alishinda matuzo mawili kwenye Shindano la Historia la Rais wa Ujerumani (Federal President’s History Competition) kwa sababu ya kuandika simulizi la maisha la Richard Rudolph na mahojiano aliyofanya pamoja naye. Shindano hilo lilikuwa na kichwa “Mashujaa wa Kawaida Tu.” Ann-Jacqueline Frieser alitunukiwa nafasi ya kwanza katika jimbo la Rheinland-Palatinate na alikuwa miongoni mwa wanafunzi watatu walioshinda tuzo la Rais.

Wolfram Slupina, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Ujerumani, anasema hivi: “Richard Rudolph hakuwa rafiki mpendwa na mwamini mwenzetu tu bali pia alikuwa chanzo chenye thamani cha habari za kihistoria. Alituwekea kielelezo kizuri kwa kuonyesha imani ya pekee na ujasiri maishani.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Ujerumani: Wolfram Slupina, simu +49 6483 41 3110