JULAI 3, 2023
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE
Mradi wa Makao Makuu ya Ramapo
Mradi wa Ujenzi wa Ramapo Umepata Idhini Muhimu ya Kuendelea na Kazi
Juni 28, 2023, mradi wa ujenzi wa Ramapo, New York, Marekani, ulipata idhini muhimu sana. Washiriki wote wa Kamati ya Mipango ya Mji wa Ramapo walitoa idhini baada ya kuona ramani na mipango ya ujenzi huo. Ingawa kuna baadhi ya mambo ambayo bado yatahitaji kufuatiliwa, idhini hiyo inatuwezesha kuendelea na mradi huo.
Inapendeza kwamba wakaaji wa eneo hilo pamoja na wenye mamlaka hawakupinga wala hawakuwa na shaka yoyote kuhusu ujenzi huo katika kikao cha Kamati ya Mipango. Ndugu Keith Cady, ambaye ni mshiriki wa Halmashauri ya Mradi wa Ujenzi wa Ramapo (CPC) alisema: “Tulitumia miezi kadhaa kutayarisha ramani na mipango ya ujenzi ili tuiwasilishe mbele ya kamati hiyo tukiwa na uhakika kwamba tumefuata sheria zote zinazohusika. Lengo letu lilikuwa kuwarahisishia kazi ili wapitishe ombi letu.” Kamati hiyo ilitambua jitihada zetu na washiriki wote walipitisha maazimio yote, moja baada ya lingine. Ndugu David Soto, mshiriki mwingine wa CPC alisema: “Mazungumzo hayo hadi kufikia uamuzi uliotolewa yalifanyika kwa muda usiozidi saa moja! Tunaishukuru Kamati ya Mipango kwa kazi yao ngumu, bidii yao, na kwa ushirikiano wao. Tunatazamia kwa hamu kuendelea kushirikiana na idara hiyo ya mipango ya mji.”
Kwa kuwa tumepata idhini hii, sasa baadhi ya kazi zinaweza kuanza Ramapo. Ndugu Cady alisema: “Mara tu miti iliyokatwa itakapoondolewa wajenzi wanaweza kuanza kazi. Hili linamaanisha kwamba tutahitaji wajitoleaji wengi zaidi kufikia mwishoni mwa mwaka ujao. Sote tuliokuwa katika kikao hicho tulifurahi sana tuliposikia kwamba tumepata idhini ya kuanza kazi hiyo hivi karibuni.”
Tukiwa kama tengenezo la ulimwenguni pote, tunamshukuru Yehova kwa kutolewa kwa idhini hiyo. Tunasali kwamba aendelee kuwabariki wote walioshiriki mradi huu kwa kuwa “[wanaimarishana] ili kufanya kazi hiyo njema” iliyo mbele yao.—Nehemia 2:18.