NOVEMBA 19, 2019
URUSI
Hakimu Nchini Urusi Aagiza Ndugu Dmitriy Barmakin Aachiliwe Baada ya Kukaa Mahabusu kwa Siku 447
Oktoba 18, 2019, Ndugu Dmitriy Barmakin alihamishiwa kwenye kifungo cha nyumbani baada ya kukaa mahabusu kwa siku 447. Sasa anafurahi tena kuwa pamoja na mke wake, Yelena, ambaye walifunga ndoa miaka 13 iliyopita.
Ndugu Barmakin alikamatwa Julai 28, 2018. Polisi waliofunika nyuso zao na waliokuwa na silaha walivamia nyumba ya nyanya wa mke wake mwenye umri wa miaka 90 na kumkamata Ndugu Barmakin. Alishtakiwa kwa kosa la kushiriki katika utendaji wa kidini wa Mashahidi wa Yehova. Mahakama ya Wilaya ya Pervorechenskiy huko Vladivostok, iliagiza kwamba Ndugu Dmitry Barmakin awekwe mahabusu kwa miezi miwili. Katika pindi nane mfululizo mahakama hiyo imeongeza muda wake wa kukaa mahabusu.
Wakati fulani kesi yake ilipokuwa ikisikilizwa, mahakama ilitaja kuwa ibada yenye amani ya Ndugu Barmakin ni “uhalifu dhidi ya misingi ya utaratibu wa katiba na usalama wa nchi.” Madai hayo ya uwongo yanapingana na kile kinachotajwa waziwazi na Kifungu cha 28 cha Katiba ya Shirikisho la Urusi inayosema kwamba kila mtu ana “uhuru wa kuchagua, kuwa na, na kuwaambia wengine kuhusu imani ya kidini na imani nyingine na kutenda kulingana nayo.
Tunafurahi kwamba Hakimu Stanislav Salnikov wa Mahakama ya Wilaya ya Pervorechenskiy huko Vladivostok aliagiza Ndugu Barmakin aachiliwe kutoka mahabusu, ijapokuwa uamuzi huo hausitishi upelelezi wa uhalifu unaoendelea dhidi yake.
Tuna uhakika kwamba Yehova ataendelea kuwaimarisha na kuwatia moyo ndugu na dada zetu nchini Urusi, hasa wale ambao wako gerezani na katika vifungo vya nyumbani. Wote hao, kama Ndugu Barmakin, ni mifano bora ya ujasiri na ushikamanifu kwa undugu wa ulimwenguni pote.