Hamia kwenye habari

Ndugu Vadim Kutsenko na mke wake, Ekaterina, mwaka wa 2018

FEBRUARI 18, 2020
URUSI

Maofisa Wamtesa Ndugu Vadim Kutsenko Huko Chita, Urusi

Maofisa Wamtesa Ndugu Vadim Kutsenko Huko Chita, Urusi

Wenye mamlaka huko Chita, Urusi, walimtesa Ndugu Vadim Kutsenko, ambaye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, usiku wa Februari 10, 2020. Maofisa hao walimpiga tena na tena Ndugu Kutsenko, wakamnyonga na kuunganisha nyaya za umeme kwenye tumbo na miguu yake. Walipokuwa wakifanya hivyo, walimwamuru Ndugu Kutsenko awape habari kuhusu Mashahidi wenzake.

Asubuhi ya siku hiyo, maofisa wa Federal Security Services (FSB) walifanya msako katika nyumba 40 hivi za Mashahidi huko Chita, kutia ndani nyumba ya Ndugu Kutsenko. Saa tano kamili asubuhi, polisi wa kitengo maalumu nchini Urusi walimkamata akiwa nyumbani kwa mama-mkwe wake. Maofisa hao walimfunga pingu, wakamfunika kichwa, na kumpeleka kwenye msitu ulio hapo karibu ambapo walimtesa. Ndugu Kutsenko alikataa kabisa kutoa habari zozote kuhusu Mashahidi wenzake. Walipotambua kwamba mbinu zao hazifanikiwi, maofisa hao walimpeleka kwenye ofisi ya ofisa-mpelelezi ili kuendelea kumhoji.

Baada ya hapo Ndugu Kutsenko aliwekwa kwenye kizuizi cha muda pamoja na ndugu wengine watatu waliokamatwa baada ya msako huko Chita—Ndugu Sergey Kirilyuk, Pavel Mamalimov, na Vladimir Yermolayev.

Siku mbili baadaye, Mahakama ya Wilaya ya Ingodinskiy iliamua kwamba Ndugu Kutsenko, Kirilyuk, na Mamalimov wawekwe kizuizini kwa saa 72. Mahakama ilimwachilia Ndugu Yermolayev kutoka kizuizini na kumweka kwenye kifungo cha nyumbani.

Februari 15, Ndugu Vadim Kutsenko na wale ndugu wengine wawili waliachiliwa kwa sababu mpelelezi hakuwa na ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka. Mpelelezi huyo aliwaachilia akina ndugu hao bila kuendesha kesi mahakamani na bila kuwawekea vizuizi vyovyote.

Tunasali kwamba Ndugu Kutsenko na ndugu zetu nchini Urusi waendelee kuwa “jasiri na imara kabisa,” wakiwa na uhakika kabisa kwamba Yehova anawaunga mkono katika majaribu yao yote.—Yoshua 1:7, 9.