JUNI 26, 2019
URUSI
Nchi ya Urusi Yalenga Mashahidi wa Yehova Wenye Umri Mkubwa, Kutia Ndani Kadhaa Wenye Umri wa Miaka Zaidi ya 70
Mei 2019, wenye mamlaka wanaotoka mikoa ya Arkhangel’sk na Volgograd nchini Urusi walifungua kesi za uhalifu dhidi ya dada zetu wawili wenye umri mkubwa. Dada Kaleriya Mamykina mwenye umri wa miaka 78, anayeonekana hapo juu, na Dada Valentina Makhmadgaeva mwenye umri wa miaka 71, wanafanyiwa uchunguzi ili kujua ikiwa wao ni miongoni mwa watu “wenye msimamo mkali” kwa sababu tu wao ni Mashahidi wa Yehova.
Aprili 2018, wenye mamlaka jijini Vladivostok walimshutumu Dada Yelena Zayshchuk mwenye umri wa miaka 84, na Mashahidi wengine wanne. Sasa jumla ya ndugu na dada zetu 10 wenye umri wa miaka zaidi ya 70 wanakabili mashtaka ya uhalifu kwa sababu ya kuabudu kwa amani nchini Urusi.
Licha ya kwamba hakuna hata mmoja kati yao aliyewekwa mahabusu, bila shaka hali hiyo inawapa mkazo sana. Ikiwa uchunguzi huo utaendelea na mahakama iwahukumu kuwa na hatia, basi wanaweza kupigwa faini kubwa au kufungwa gerezani.
Kufikia Juni 17, 2019, idadi ya ndugu zetu ambao wamekabili isivyo haki mashtaka ya uhalifu imefika 215. Na idadi yao inazidi kuongezeka. Acheni tuendelea kuwataja ndugu na dada zetu katika sala, na ikiwezekana tutaje majina yao hususa. Tuna uhakika kwamba Yehova ataendelea kuwaimarisha “kwa nguvu zote kwa uwezo wake wenye utukufu” ili ‘wavumilie kikamili kwa subira na shangwe.’—Wakolosai 1:11.