Hamia kwenye habari

Ndugu Oleg Danilov

MACHI 31, 2021
URUSI

Ndugu Oleg Danilov Amehukumiwa Kifungo cha Miaka Mitatu Baada ya Kesi Iliyoharakishwa

Ndugu Oleg Danilov Amehukumiwa Kifungo cha Miaka Mitatu Baada ya Kesi Iliyoharakishwa

HABARI ZA KARIBUNI | Mahakama ya Urusi Yakataa Ombi la Rufaa la Ndugu Oleg Danilov

Mei 25, 2021, Mahakama ya Eneo la Krasnodar ilikataa ombi la rufaa katika kesi inayomhusu Ndugu Oleg Danilov. Hukumu yake ya awali ya kifungo cha miaka mitatu gerezani inaendelea kutumika.

Hukumu

Machi 30, 2021, Mahakama ya Wilaya ya Abinskiy katika Eneo la Krasnodar ilitangaza uamuzi katika kesi inayomhusu Ndugu Oleg Danilov. Alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani. Alipelekwa moja kwa moja gerezani kutoka mahakamani.

Maelezo Mafupi Kumhusu

Oleg Danilov

  • Alizaliwa: 1974 (Usolye-Sibirskoye, Siberia)

  • Maisha Yake: Katika mwaka wa 1958, Mashahidi wa Yehova waliokuwa wamepelekwa uhamishoni Siberia waliwafundisha babu na nyanya yake kile ambacho Biblia inafundisha. Alilelewa na wazazi Wakristo. Alibatizwa mnamo 1991

  • Alifunga ndoa na Nataliya mnamo 1995. Walizaa wana wawili. Familia yao inapenda kusafiri na kutumia muda pamoja wakitazama uumbaji

Historia ya Kesi

Nyumba ya Ndugu Danilov ilifanyiwa upekuzi Aprili 29, 2020 kwa mara ya kwanza. Maofisa wa usalama hawakupata machapisho yoyote yaliyopigwa marufuku lakini walichukua simu za mkononi za familia hiyo pamoja na mali zao nyingine. Ingawa hakukuwa na uthibitisho, kesi ya uhalifu ilifunguliwa dhidi ya Oleg mwezi wa Novemba 2020. “Uhalifu” alioshukiwa kufanya ulitia ndani kufundisha masomo ya dini, kutoa hotuba, na kushiriki katika mazungumzo ya Biblia.

Desemba 2, 2020, saa 12:00 asubuhi, maofisa wa usalama walivamia nyumba ya Oleg kwa mara ya pili na kufanya upekuzi wenye kina kuliko wa kwanza. Baadaye, Oleg alipelekwa kwenye kituo cha polisi na kuhojiwa.

Mahakama iliharakisha kesi ya uhalifu ya Oleg. Machi 23, 2021 alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza. Mpelelezi aliyeshughulikia kesi yake alikuwa O. I. Komissarov ambaye pia alikuwa akishughulikia kesi ya Ndugu Aleksandr Ivshin mwenye umri wa miaka 63. Mnamo Februari 2021, baada ya kesi iliyoharakishwa pia, Ndugu Ivshin alipewa hukumu kali zaidi kufikia leo, kifungo cha miaka saba na nusu gerezani.

Ingawa matukio yote hayo yametokeza hali ngumu kwa Oleg na familia yake, tunajua kwamba Mungu wetu, Yehova hatawahi kusahau kazi zao na upendo wanaoonyesha kwa ajili ya jina Lake.—Waebrania 6:10.