Hamia kwenye habari

MEI 30, 2017
URUSI

Mashahidi wa Yehova Wamekata Rufaa Dhidi ya Uamuzi Usio wa Haki wa Mahakama Kuu ya Urusi

Mashahidi wa Yehova Wamekata Rufaa Dhidi ya Uamuzi Usio wa Haki wa Mahakama Kuu ya Urusi

Mashahidi wa Yehova nchini Urusi walikata rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ambao ulipiga marufuku ibada yao. Uamuzi wa Aprili 20 uliotolewa na Hakimu Yuriy Ivanenko, ulizuia utendaji wote wa mashirika ya kisheria ya Mashahidi nchini kote. Jopo la majaji watatu katika Mahakama Kuu ya Rufaa litasikiliza rufaa hiyo Julai 17, 2017.

Katika rufaa hiyo Mashahidi wanaomba hukumu hiyo ibatilishwe kabisa. Wamekazia kwamba hukumu hiyo haikuzingatia uthibitisho halisi na kwamba Mashahidi wa Yehova hawana hatia ya kufanya utendaji unaochochea msimamo mkali kwa njia yoyote ile. Pia, rufaa hiyo inaeleza wazi kwamba mashtaka yaliyosababisha uamuzi huo wa Mahakama Kuu ni yaleyale ambayo wenye mamlaka walitumia kama msingi wa kuwatesa Mashahidi wakati wa Muungano wa Sovieti. Baadaye mashtaka hayo yaliondolewa. Isitoshe, rufaa hiyo inasisitiza kwamba uamuzi huo unapingana na uhuru wa ibada unaotolewa na Katiba ya Urusi na mikataba yake ya kimataifa.

Uamuzi huo tayari umewaathiri Mashahidi katika njia zilezile kama walipokandamizwa katika utawala wa Kikomunisti. Wenye mamlaka wanawatesa baadhi ya Mashahidi kwa madai ya kushiriki “utendaji wenye msimamo mkali,” waajiri wamewafuta kazi Mashahidi, walimu wamewatisha wanafunzi ambao ni Mashahidi mbele ya wanafunzi wengine, na watu wenye ubaguzi wameharibu Majumba ya Ufalme na kuchoma kabisa nyumba mbili za Mashahidi.

Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanatumaini kwamba Mahakama Kuu ya Rufaa ya Urusi itaona ukosefu huo wa haki unaotokana na uamuzi uliotolewa awali na kuubatilisha, hivyo kulinda uhuru wa ibada na usalama wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi.