NOVEMBA 28, 2016
URUSI
SEHEMU YA 3
Wataalamu wa Kimataifa Watilia Shaka “Uchunguzi wa Wataalamu” wa Urusi wa Kutambua “Msimamo Mkali”
Hii ni Sehemu ya 3 ya mfuatano wa mahojiano ya pekee yaliyo na sehemu tatu pamoja na wasomi maarufu wa mambo ya dini, siasa, na soshiolojia na pia wataalamu wanaofahamu ule uliokuwa Muungano wa Sovieti na hali baada ya kuvunjika kwa Muungano wa Sovieti.
ST. PETERSBURG, Urusi—Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakifanyiwa uchunguzi pamoja na machapisho yao. Mahakama iliamuru uchunguzi huo ufanywe na Kituo cha Masomo ya Kitaalamu ya Jamii na Utamaduni jijini Moscow. Uchunguzi wa kwanza ulikamilika Agosti 2015 na kutumiwa kama msingi wa kesi inayoendelea dhidi ya Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Mashahidi, huku matokeo ya uchunguzi mwingine yakisubiriwa.
Wataalamu wanaoheshimiwa sana ndani na nje ya Urusi hawakubaliani na uchunguzi huo. Msomi mmoja, Dakt. Mark R. Elliott, mhariri wa kwanza wa East-West Church and Ministry Report, anasema hivi: “Wataalamu walioteuliwa na serikali kutoa ushahidi katika masuala ya kidini, kutia ndani wale ambao walipinga maandiko ya Mashahidi wa Yehova, hawana ustadi wala ustahili kwa kuwa wanatoa maoni yasiyo na msingi kuhusu masuala ya imani.”
Akikirejelea Kituo cha Masomo ya Kitaalamu ya Jamii na Utamaduni, Dakt. Roman Lunkin, mkuu wa Kituo cha Dini na Jamii kilicho katika Taasisi ya Ulaya ya Chuo cha Sayansi cha Urusi jijini Moscow, anasema kwamba, “wataalamu wote waliotumiwa hawakuwa na shahada katika masomo ya dini na wala hawayafahamu vizuri machapisho ya Mashahidi wa Yehova. Uchunguzi wao unahusisha manukuu yaliyotolewa kutoka katika habari walizopata kutoka kwa Kituo cha Irenaeus of Lyon, kikundi chenye msimamo mkali cha Kanisa Othodoksi kinachojulikana kwa kuwapinga Mashahidi wa Yehova, pamoja na dini nyingine nyingi.”
Dakt. Ekaterina Elbakyan, profesa wa soshiolojia na mipango ya maendeleo ya jamii katika Kituo cha Elimu ya Kazi na Mahusiano ya Kijamii cha Moscow anaeleza hivi: “Ninakubaliana na Dakt. Lunkin. Ni kweli kwamba mara nyingi uchunguzi wa masuala ya kidini nchini Urusi leo haufanywi na wataalamu, na wanafanya uchunguzi huo kama walivyoamriwa, kwa hiyo mtaalamu mwenyewe hana uhuru wa kueleza ukweli wa uchunguzi wake.”
Dakt. Elbakyan, aliyeshiriki katika kesi mbili zilizofanywa Taganrog na ambaye alikuwepo akiwa mtaalamu maalumu katika mahakama ya rufani huko Rostov-on-Don, anasema hivi: “Niliona kwa macho yangu mwenyewe video ambazo zilitumika kama msingi wa kuwashtaki Mashahidi wa Yehova kwamba wana msimamo mkali. Mara mbili nilitoa maelezo ya kina mahakamani nikieleza kwamba video hizo zilionyesha mkutano wa kawaida wa dini ya Kikristo na hakuna chochote kinachoonyesha kuwepo kwa msimamo mkali, lakini mahakama ilipuuza maoni ya mtaalamu. Inaonekana wazi kwamba huu ni ukandamizaji wa dini ulio wazi na ambao umepangwa. Kadiri mwelekeo huu unavyoendelea, kwa kweli, hakuna uhakikisho kwamba waumini hawataacha kuonwa kuwa wana ‘msimamo mkali’ kwa sababu ya imani yao.”
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, 1-718-560-5000
Urusi: Yaroslav Sivulskiy, 7-812-702-2691