VIJANA HUULIZA
Nifanye Nini Wazazi Wangu Wakinizuia Kutumia Mitandao ya Kijamii?
Huenda rafiki zako wote wanatumia mitandao ya kijamii, na wanazungumza kuihusu kila wakati. Labda hata wanakudhihaki kwa sababu huna akaunti. Unahitaji kujua nini kuhusu hali hiyo? Na unaweza kufanya nini ikiwa unakabili hali hiyo?
Unachohitaji kujua
Vijana wengi wanakabili hali kama yako. Wazazi wengi hawawaruhusu watoto wao kutumia mitandao ya kijamii. Huenda kwa sababu wanatambua mitandao hiyo imehusianishwa na matatizo yafuatayo:
kushuka moyo na matatizo mengine ya afya ya akili.
kutazama ponografia, kutuma ujumbe mchafu (sexting), na kuonewa mtandaoni.
marafiki wanakosana bila sababu.
Vijana wengi wameamua kuacha kutumia mitandao ya kijamii. Walitambua kwamba mitandao hiyo ilikuwa ikiwaletea madhara mengi kuliko kuwafaidi. Fikiria mifano halisi ifuatayo:
Priscilla alitambua alikuwa akitumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii ambao angetumia kufanya mambo muhimu zaidi.
Jeremy aligundua kwamba asingeweza kuzuia habari zisizofaa zilizokuwa zikijitokeza katika mtandao wa kijamii aliokuwa akitumia.
Bethany alitambua kwamba alikuwa akikazia fikira kupita kiasi mambo ambayo watu wengine walikuwa wakifanya.
“Niliamua kufuta programu ya mtandao wa kijamii niliokuwa nikitumia, na ninafurahi kwamba nilifanya hivyo. Sihisi ninakosa chochote, na ninafurahia kuwa na muda mwingi zaidi wa kuzingatia mambo muhimu zaidi kwangu.”—Sierra.
“Sikupenda jinsi nilivyoanza kuwa mraibu wa mitandao ya kijamii na pia jinsi pindi fulani nilivyohangaika ikiwa watu wataonyesha wamefurahia mambo niliyoweka mtandaoni. Haikuwa rahisi kufuta akaunti yangu, lakini nilijihisi vizuri punde tu nilipofanya hivyo. Sasa nina amani zaidi.”—Kate.
Unachoweza kufanya
Heshimu sheria za wazazi wako. Waonyeshe kwamba wewe ni mkomavu kiasi cha kutosha kuishi kupatana na sheria zao bila kukasirika au kulalamika.
Kanuni ya Biblia: “Mpumbavu huonyesha hasira yake yote, bali mwenye hekima hujizuia.”—Mithali 29:11, Neno: Maandiko Matakatifu.
Huenda vijana wenzako wakakushauri utumie mitandao ya kijamii bila wazazi wako kujua au ufungue akaunti kisiri. Hilo linaweza kukuletea matatizo makubwa! Kujaribu kutumia ujanja huo kutakuacha ukiwa na wasiwasi na ukijihisi una hatia. Pia, utapata matatizo wazazi wako wakigundua, na bila shaka wataacha kukuamini.
Kanuni ya Biblia: “Tunataka kujiendesha kwa unyoofu katika mambo yote.”—Waebrania 13:18.
Jifanyie uamuzi. Kama vijana waliotajwa hapo juu, huenda ukafikiria kuhusu sababu nyingi za kuepuka mitandao ya kijamii. Ikiwa ni wazi mitandao ya kijamii inakuathiri vibaya, iepuke si kwa sababu tu ni uamuzi wa wazazi wako bali pia kwa sababu umejiamulia kufanya hivyo. Kwa njia hiyo, ikiwa rafiki zako watakuuliza, hutaona aibu—na matokeo ni kwamba huenda hawatakudhihaki.
Jambo kuu: Shirikiana na wazazi wako, na uone ni jambo gani unalokubaliana nalo ili uamuzi wao uwe uamuzi wako pia. Angalau kwa sasa unaweza kuishi bila kutumia mitandao ya kijamii.