Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Ngozi ya Chungu wa Sahara—Mwavuli Unaomkinga na Joto

Ngozi ya Chungu wa Sahara—Mwavuli Unaomkinga na Joto

CHUNGU wa rangi ya fedha anayeishi katika jangwa la Sahara (Cataglyphis bombycina) ni mmoja kati ya viumbe wenye uwezo mkubwa wa kuvumilia joto kali. Wakati wa mchana eneo la Sahara huwa na jua kali sana hivi kwamba wanyama ambao ni adui za chungu hulazimika kutafuta kivuli, kwa hiyo chungu hutumia mwanya huo wa pekee kutoka shimoni na kujitafutia chakula. Kipindi hicho kinafaa kwani yeye hupata mizoga ya wadudu wengine waliokufa kutokana na joto kali.

[50] μm

Jambo la kufikiria: Ngozi ya chungu wa rangi ya fedha imefunikwa na vinyweleo vya pekee upande wa juu na pembeni, lakini tumboni hakuna vinyweleo. Vinyweleo (1, 2), ambavyo humfanya chungu huyo ang’ae, ni vyembamba na vina umbo la pembe tatu (3). Pande mbili za vinyweleo hivyo zina matuta madogo madogo, wakati upande ule mwingine ni laini. Muundo huu wa pekee hutimiza mambo mawili muhimu. Kwanza, huwezesha vinyweleo kuakisi miali ya jua yenye joto. Pili, humwezesha chungu kutawanya joto la mwili wake. Wakati huohuo, sehemu ya chini ya mwili wake isiyo na vinyweleo, huakisi joto la mchanga wa jangwa. *

[10] μm

Ngozi ya chungu wa Sahara ni kama mwavuli ambao humkinga na joto, na hivyo kudumisha kiwango cha joto ambacho anaweza kustahimili, yaani, chini ya nyuzi joto 53.6. Kwa sababu ya kumchunguza mdudu huyo mdogo, watafiti wanajaribu kuunda njia ya pekee ambayo inaweza kutumiwa kupunguza joto bila kutumia feni.

Una maoni gani? Je, ngozi ya chungu wa Sahara mwenye rangi ya fedha ilitokea kwa njia ya mageuzi? Au ilibuniwa?

^ fu. 4 Vitu vingine vya pekee katika chungu hao ni protini ya miili yao ambayo haiwezi kuvunjwavunjwa na joto kali, miguu mirefu inayomfanya awe juu anapotembea kwenye mchanga wa moto na pia kumwezesha kukimbia kwa kasi, na ustadi wa kutambua njia fupi zaidi ambao humwezesha kukimbia kwa kasi na kurudi katika shimo lake.