Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

TATIZO

Mambo Yanayohatarisha Usalama Duniani

Mambo Yanayohatarisha Usalama Duniani

“Kizazi hiki ndicho kilichoendelea zaidi kiteknolojia, kisayansi, na kiuchumi . . . Hata hivyo, inaonekana kizazi hikihiki ndicho ambacho huenda kitaporomosha kabisa mifumo [ya siasa, uchumi, na mazingira].”​—The Global Risks Report 2018, World Economic Forum.

KWA NINI WATU WENGI WANAHANGAISHWA NA HALI YETU YA WAKATI UJAO NA JINSI DUNIA ITAKAVYOKUWA? ACHENI TUCHUNGUZE BAADHI YA CHANGAMOTO TUNAZOKABILI.

  • UHALIFU WA MTANDAONI: “Kila siku inazidi kuwa hatari kutembelea vituo vya intaneti. Intaneti imekuwa uwanja wa watu walio na tamaa ya kufanya ngono na watoto, watu wakorofi, watu wanaochochea mabishano, na wezi wa taarifa mtandaoni.” Kutumia jina, namba ya siri, au namba ya kadi ya mtu mwingine bila ridhaa yake ili kujinufaisha, “ni aina ya uhalifu inayokua kwa kasi zaidi ulimwenguni. . . . Vilevile, kwenye intaneti watu hupata fursa ya kuonyesha roho ya kikatili, moja ya sifa mbaya zaidi za wanadamu.”—Gazeti The Australian.

  • PENGO KATI YA MATAJIRI NA MASKINI: Ripoti ya karibuni ya shirika la Oxfam inaonyesha kwamba, mali zinazomilikiwa na watu nane walio matajiri zaidi duniani ni sawa na mali za watu bilioni 3.6 walio maskini zaidi. Kulingana na shirika hilo, “uchumi wetu unaelekeza mali kwa matajiri wakubwa kwa njia inayowadidimiza watu maskini zaidi katika jamii, wengi wao wakiwa ni wanawake.” Baadhi ya watu wanahofu kwamba huenda pengo hilo linalozidi kuongezeka litasababisha machafuko katika jamii.

  • VURUGU NA UNYANYASAJI: Ripoti ya 2018 ya Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi inasema: “Hatujawahi kushuhudia idadi kubwa ya watu wanaokimbia eneo moja kwenda lingine kama tunayoona sasa.” Zaidi ya watu milioni 68 wamelazimika kukimbia makazi yao, hasa kwa sababu ya vurugu au unyanyasaji. Ripoti hiyo inaendelea kusema: “Inakadiriwa kwamba kila baada ya sekunde mbili, mtu mmoja hulazimika kuhama.”

  • KUHARIBIWA KWA MAZINGIRA: Ripoti moja ya mwaka wa 2018, inasema kwamba “wanyama na mimea wanatoweka kwa kiwango kikubwa sana, . . . na uchafuzi wa hewa na bahari unazidi kuhatarisha afya ya wanadamu.” Pia, idadi ya wadudu inazidi kuporomoka katika baadhi ya nchi. Kwa sababu wadudu huchavusha mimea, wanasayansi wanahofu kwamba hivi karibuni mifumo ya asili itaangamia. Matumbawe nayo yako hatarini. Wanasayansi wanakadiria kwamba nusu ya matumbawe duniani imetoweka katika miaka 30 iliyopita.

Je, tuna uwezo wa kufanya mabadiliko yanayohitajika ili ulimwengu uwe salama zaidi? Baadhi ya watu wanahisi kwamba njia moja ya kuleta mabadiliko hayo ni kutoa elimu. Ikiwa ndivyo, ni aina gani ya elimu inayohitajika? Makala zinazofuata zitajibu maswali hayo.