Uwezo wa Kustaajabisha wa Membe wa Aktiki
KWA muda mrefu ilifahamika kwamba membe wa aktiki husafiri umbali wa karibu kilometa 35,200, kuanzia eneo la Aktiki kwenda Antaktika na kurudi. Hata hivyo, utafiti wa hivi karibuni unafunua kuwa ndege hao husafiri umbali mrefu zaidi.
Kifaa kidogo kinachoweza kutambua mahali ndege alipo kilifungwa katika baadhi ya ndege. Kifaa hicho cha pekee chenye uzito unaokaribiana na wa pini ya karatasi, kilifunua kwamba baadhi ya membe walisafiri wastani wa kilometa 90,000 katika mzunguko mzima wa safari, umbali mrefu zaidi ukilinganisha na wanyama wengine. Ndege mmoja alisafiri karibu kilometa 96,000! Kwa nini makadirio hayo yalirekebishwa?
Bila kujali mahali walipoanzia, membe wa aktiki hawakwenda moja kwa moja, bali walizunguka. Kama inavyoonekana kwenye picha, njia waliyopitia kwenye Bahari ya Atlantiki inafanana na herufi S. Kwa nini? Kwa sababu ndege hao hutumia mkondo wa upepo wa bahari.
Katika muda wa maisha yao yote karibu miaka 30 hivi, membe wanaweza kuwa wamesafiri zaidi ya kilometa milioni 2.4. Huo ni umbali unaolingana na safari tatu au nne za kwenda mwezini na kurudi! Mtafiti mmoja alisema hivi: “Hilo ni jambo la kushangaza sana kwa ndege mwenye uzito wa gramu 100 hivi kutimiza.” Zaidi ya yote, kitabu Life on Earth: A Natural History kinasema kwamba membe huona “mwangaza wa mchana muda mrefu zaidi kwa mwaka kuliko kiumbe kingine chochote,” kwa sababu wao huishi katika majira ya kiangazi wakiwa Aktiki na Antaktika.