TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HISTORIA
Alhazen
HUENDA hujawahi kumsikia Abū ‘Alī al-Ḥasan ibn al-Haytham. Katika nchi za Magharibi anafahamika kwa jina la Kilatini Alhazen, linalotokana na jina lake la kwanza la Kiarabu, al-Hasan. Iwe unamfahamu au la, unanufaika kutokana na kazi zake. Ametajwa kuwa “mmoja wa watu muhimu sana na wenye mchango mkubwa katika historia ya sayansi.”
Alhazen alizaliwa Basra, eneo lililo nchini Iraq, katika miaka ya 965 W.K. Alipendezwa na mambo mengi kutia ndani elimu ya mwanga, nyota, kemia, hesabu, tiba, muziki, fizikia, na ushairi. Tunapaswa kumshukuru hasa kwa jambo gani?
BWAWA LA MTO NILE
Hadithi kumhusu Alhazen imeenea tangu zamani. Hadithi hiyo inahusu mpango wake wa kudhibiti mtiririko wa maji ya Mto Nile karibu miaka 1,000 kabla ya mradi huo kutekelezwa huko Aswân mwaka wa 1902.
Kulingana na hadithi hiyo, Alhazen alikuwa na mpango kabambe wa kumaliza tatizo la mafuriko na ukame nchini Misri kwa kuutengenezea Mto Nile bwawa. Mtawala wa Kairo, Khalifa al-Hakim, aliposikia wazo la Alhazen, alimwita nchini Misri ili ajenge bwawa hilo. Hata hivyo, alipofika na kuuona mto kwa macho yake mwenyewe, Alhazen alitambua kwamba mradi huo ulikuwa nje ya uwezo wake. Kwa sababu ya kuogopa adhabu kutoka kwa mtawala huyo mkorofi na asiyetabirika, Alhazen alijifanya mwendawazimu mpaka Khalifa al-Hakim alipokufa mwaka wa 1021, miaka 11 hivi baadaye. Katika kipindi hicho, Alhazen alikuwa na muda mwingi ambao aliutumia kufanya mambo mengine yaliyompendeza, mahali alipokuwa amefungiwa.
KITABU KUHUSU TABIA YA MWANGA
Kufikia wakati alipoachiliwa, Alhazen alikuwa ameandika sehemu kubwa ya mabuku saba ya kitabu chake (Book of Optics), ambacho kimetajwa kuwa “kati ya vitabu muhimu sana kwenye historia ya fizikia.” Katika kitabu hicho ameelezea tafiti mbalimbali kuhusu tabia ya mwanga, kutia ndani jinsi unavyotawanyika na kutokeza rangi zake za msingi, jinsi unavyoakisiwa na vioo, na jinsi unavyojipinda unaposafiri kutoka kwenye kitu kimoja kwenda kingine.
Pia alichunguza uwezo wa kuona na muundo wa jicho na jinsi linavyofanya kazi.Kufikia karne ya 13, kitabu cha Alhazen kilikuwa kimetafsiriwa katika lugha ya Kilatini kutoka kwenye Kiarabu, na kwa karne zilizofuata, wasomi mbalimbali barani Ulaya walikirejelea katika machapisho yao. Mambo ambayo Alhazen aliandika kuhusu tabia za lenzi yaliweka msingi ambao ulitumiwa na watengenezaji wa miwani barani Ulaya ambao, kwa kutazama lenzi moja kupitia nyingine waliweza kuvumbua hadubini na darubini.
KAMERA YA KALE
Alhazen aligundua kanuni za msingi kuhusu upigaji wa picha alipotengeneza kitu tunachoweza kukiita kamera ya kwanza katika historia. Alitengeneza chumba chenye giza ambacho kiliruhusu mwanga upite kupitia tundu dogo sana, na hivyo kutokeza picha iliyogeuka ya vitu vilivyokuwa nje katika ukuta wa ndani wa chumba.
Katika miaka ya 1800, mabamba ya kupigia picha yalianza kutumiwa pamoja na uvumbuzi wa Alhazen ili kunasa picha na kuzitunza. Matokeo? Kamera. Kamera zote za kisasa, na hata macho yetu, hutumia kanuni zilezile za msingi kama za chumba chenye giza cha Alhazen. *
MBINU YA KISAYANSI
Jambo moja la pekee kuhusu kazi za Alhazen ni jinsi alivyofanya utafiti wa vitu vya asili kwa umakini na utaratibu wa hali ya juu. Watu katika siku zake hawakuwa wakitumia mbinu kama alizotumia. Alikuwa kati ya watu wa kwanza kuchunguza ukweli wa nadharia mbalimbali kwa kuzifanyia utafiti, na hakukubaliana tu moja kwa moja na mambo yaliyokubaliwa na wengi ikiwa hakukuwa na uthibitisho ulioyaunga mkono.
Kanuni moja inayowaongoza wanasayansi leo inasema: “Thibitisha kile unachoamini!” Baadhi ya watu humwona Alhazen kuwa “baba ya mbinu ya kisasa ya kisayansi.” Kwa msingi huo, tuna sababu nyingi za kumshukuru.
^ fu. 13 Watu wa nchi za Magharibi hawakuelewa jinsi utendaji wa jicho unavyofanana na wa kamera hadi ufafanuzi huo ulipotolewa na Johannes Kepler katika karne ya 17.