Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Kahawa Inaongeza Kiasi cha Kolesteroli Mwilini Mwako?

Je, Kahawa Inaongeza Kiasi cha Kolesteroli Mwilini Mwako?

Je, Kahawa Inaongeza Kiasi cha Kolesteroli Mwilini Mwako?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI

WATAFITI katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Wageningen, Uholanzi, wanasema kwamba kunywa kahawa isiyochujwa kunaongeza kiasi cha kolesteroli mwilini mwako.

Jambo kuu ni “isiyochujwa.” Kwa nini? Kijarida cha Research Reports, cha Shirika la Uholanzi la Utafiti wa Kisayansi, chasema kwamba buni huwa na cafestol inayoongeza kolesteroli mwilini. Maji moto yanapomwagwa kwenye unga wa buni, hutokeza cafestol. Ndivyo inavyokuwa kahawa laini inapochemshwa majini mara kadhaa, sawa na kahawa tamu, au wakati kichujio cha chuma kinapotumiwa badala ya kichujio cha karatasi, kama vile katika kisindiko chenye kichujio. Kichujio cha karatasi kisipotumiwa cafestol huchanganyika na kinywaji.

Kikombe kimoja cha kahawa isiyochujwa, chaweza kuwa na miligramu nne za cafestol, na chaweza kuongeza kiasi cha kolesteroli mwilini kwa asilimia 1 hivi. Spreso huwa na cafestol pia, kwa kuwa inatayarishwa pasipo kichujio cha karatasi. Hata hivyo, uwezo wake wa kuongeza kolesteroli hupungua unapotumia kikombe kidogo. Kiasi kidogo cha spreso huwa na cafestol chache—labda miligramu moja au mbili tu kwa kila kikombe. Hata hivyo, kijarida cha Research Reports chaonya kwamba kunywa vikombe vitano vya spreso kwa siku kwaweza kuongeza kiasi cha kolesteroli mwilini kwa asilimia 2.

Jambo muhimu ni kwamba kahawa iliyotayarishwa kwa kichujio cha karatasi haina cafestol.