Watangulizi Katika Tiba
Watangulizi Katika Tiba
AKIWA na umri wa miaka 61, José, Mbelgiji kutoka mji mdogo wa Oupeye, aliambiwa kwamba angehitaji kupandikizwa ini. “Hilo ndilo jambo lililonishtua zaidi maishani,” asema. Miongo minne tu iliyopita, lilikuwa jambo lisilofikirika kupandikizwa ini. Hata katika miaka ya 1970, kiwango cha kuokoka kilikuwa asilimia 30 hivi. Hata hivyo, leo kupandikiza ini hufanywa kwa ukawaida, kukiwa na kiwango kikubwa zaidi cha mafanikio.
Lakini bado kuna tatizo kubwa. Kwa kuwa upandikizaji wa ini mara nyingi huhusisha kuvuja damu nyingi kwa kawaida madaktari hutumia damu wakati wa upasuaji. Kwa sababu ya masadikisho yake ya kidini, José hakutaka damu. Lakini alitaka apandikizwe ini. Haiwezekani? Huenda wengine wakafikiri hivyo. Lakini daktari-mpasuaji mkuu alihisi kwamba yeye pamoja na wafanyakazi wenzake walikuwa na fursa nzuri ya kufanya upasuaji kwa mafanikio bila damu. Na hivyo ndivyo walivyofanya haswa! Siku 25 tu baada ya kupasuliwa, José alikuwa amerudi nyumbani akiwa pamoja na mke na binti yake. *
Kwa sababu ya ustadi wa watu ambao gazeti Time huwaita “mashujaa wa tiba,” sasa tiba na upasuaji bila damu umepata kuwa jambo la kawaida zaidi. Lakini kwa nini unatakwa na watu wengi? Ili kujibu swali hilo, acheni tuchunguze historia yenye matatizo ya utiaji-damu mishipani.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Mashahidi wa Yehova huona upasuaji wa kupandikizwa viungo kuwa jambo linalotegemea dhamiri ya mtu mmoja-mmoja.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Sasa ulimwenguni pote kuna madaktari zaidi ya 90,000 ambao wamesema wazi kwamba wako tayari kuwatibu Mashahidi wa Yehova bila damu