Kudhibiti Mdudu Mharibifu
Kudhibiti Mdudu Mharibifu
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Kanada
HUNYEMELEA msitu, akipuuza miti michanga na kushambulia iliyozeeka. Mharibifu huyo ni mdogo sana akilinganishwa na chakula chake. Yeye husonga kasi bila kuchoka hadi anapoharibu kabisa msitu wote. Mti hupambana kufa na kupona na mshambuliaji huyo. Hatimaye mshambuliaji hushinda.
Adui huyo ni nani? Mshambuliaji huyo ni mdudu aitwaye mountain pine beetle aliye mdogo sana, naye huishi magharibi mwa Amerika Kaskazini. Yeye hushambulia msonobari mkubwa aina ya lodgepole unaopatikana katika jimbo la British Columbia, Kanada.
Takriban asilimia 35 ya eneo la msitu katika jimbo hilo limefunikwa na misonobari aina ya lodgepole—mahali bora pa kuzalia pa mdudu aina ya mountain pine beetle, mwenye umbo la mcheduara na ukubwa wa milimeta 3 hadi 8 tu. Mwanzoni yeye hushambulia misitu ya misonobari dhaifu iliyozeeka. Hata hivyo, wadudu hao waongezekapo, huanza kushambulia miti yenye afya iliyokomaa. (Ona sanduku “Duru ya Maisha ya Mountain Pine Beetle.”) Hivi karibuni wadudu hao wameangamiza misonobari milioni 30 kwa muda wa mwaka mmoja tu katika British Columbia. Inakadiriwa kwamba beetle wengi wanaweza kutoka kwa mti ulioshambuliwa na kuangamiza miti miwili yenye ukubwa sawa mwaka unaofuata.
Wadudu waitwao mountain pine beetle ni viumbe wa kawaida katika mazingira, wao pamoja na mioto ya misitu husafisha upya misitu ya lodgepole pine iliyokomaa. Hata hivyo, kuingilia kati kwa wanadamu katika kupunguza mioto hiyo kumehifadhi misitu mikubwa ya miti iliyokomaa na kuzeeka. Ingawa kuingilia kati huko kumelinda mazingira ya wanyama wa porini na njia za viumbe wanaohama kutia ndani misitu inayotumiwa kwa tafrija na shughuli za viwanda, pia kumetokeza uhitaji wa kudhibiti mountain pine beetle. Hata hivyo, wadudu hao wadogo waharibifu hutafutwaje na kunaswa kwenye nyika kubwa sana? Je, kuna hatua yoyote inayoweza kuchukuliwa ili kuzuia uharibifu wao mkubwa?
Kuwatafuta na Kuwafuata
Ni sharti mountain pine beetle watafutwe walipo kwanza ndipo wadhibitiwe. Msitu huo mkubwa hukaguliwa kutoka hewani ili kutambua miti iliyobadilika na kuwa myekundu kileleni. Miti ya namna hiyo huwa imeshambuliwa na huonekana kwa urahisi kati ya miti mingine mingi ya kijani-kibichi. Mfumo wa vikao wa tufeni (GPS) huonyesha idadi ya miti myekundu na eneo lililoshambuliwa. Habari hurekodiwa na kuhifadhiwa kwa uangalifu katika kompyuta ya mkononi.
Baadaye habari hiyo pamoja na ramani kamili za eneo la msitu lenye majani huingizwa katika kompyuta ya kawaida kwa kutumia mifumo yenye nguvu ya habari za kijiografia. Kila eneo lenye wadudu hupewa nambari, na orodha inayoonyesha vituo vya kila eneo hutayarishwa. Kazi hiyo ni muhimu kwa wachunguzi walio msituni waliotumwa kuthibitisha kiwango cha shambulio.Hata hivyo, hatari kubwa kwa msitu si miti iliyogeuka na kuwa myekundu bali miti ya kijani-kibichi inayoshambuliwa sasa. Miti hiyo hutambuliwa kwa sababu ya utomvu unaozingira tundu lililotobolewa na beetle na unga wa mbao uliomwagika chini ya mti. Miti yote iliyoshambuliwa hufungiliwa utepe wa plastiki na kuandikwa nambari kwa rangi. Mandhari ya nchi na idadi ya miti iliyoshambuliwa huchunguzwa, vilevile habari nyingineyo inayohitajiwa na mashirika yanayohusika ili yaamue hatua inayohitaji kuchukuliwa ili kudhibiti kuenea kwa wadudu hao waharibifu.
Mbinu za Kudhibiti
Ikiwa eneo lililoshambuliwa na wadudu ni kubwa kiasi cha kustahili kukata miti, kikundi kingine hutumwa ili kuchora ramani ya eneo hilo. Plani ya kukata miti hupelekwa kwa Idara ya Misitu ili itoe kibali. Kampuni inayokata miti pia huwa na wajibu wa kupanda miti mingine na kutunza miche hiyo hadi inapokomaa vyakutosha. Utaratibu huu mbali na kuruhusu matumizi ya miti pia hudhibiti kuenea kwa wadudu waharibifu na huendeleza upandaji wa miti mipya.
Hata hivyo, isipofaa kukata miti, yapendekezwa kutunza mti mmojammoja. Hilo laweza kutia ndani kuichoma sindano yenye viuadudu au kukata na kuchoma miti iliyoambukizwa katika eneo hilo. Njia hiyo ya mwisho ya kudhibiti wadudu, inayofanywa mwisho wa majira ya baridi kali au mapema katika masika kabla ya beetle kuibuka, ni yenye matokeo sana ila tu inahusisha kazi nyingi. Dale, mtaalamu wa kutambua na kudhibiti mashambulizi ya wadudu, aeleza Amkeni! ratiba ya kazi ya siku moja.
“Hatua ya kwanza ni kusafiri kwa ustadi kwenye barabara nyembamba zilizojipinda ambazo hutumiwa na malori makubwa yanayobeba miti mikubwa. Kwa ajili ya usalama twatumia redio ya mawasiliano ili kuchunguza utendaji barabarani. Tufikiapo mwisho wa barabara, twapakua magari na vitoroli vya kutelezea juu ya theluji kisha twapenya ndani kabisa ya msitu kwa miguu. Mfumo wetu wa GPS na dira zetu zimepakiwa kwa uangalifu, pamoja
na misumeno ya minyororo, petroli, mafuta, shoka, redio, viatu vya theluji, na vifaa vya huduma ya kwanza. Twavuka vinamasi, maeneo yenye majimaji, vijia vinavyopitia vichakani na kusafiri kwa kilometa nyingi. Magari yetu ya theluji yanapokwama, twavaa viatu vya theluji, vinavyotuwezesha tutembee japo kwa shida kwenye theluji yenye kina cha meta 1.2 hivi katika sehemu nyingine.“Ni kazi ngumu kubeba vifaa vya kazi vyenye uzito wa kilogramu 15 hivi kupitia sehemu zisizojulikana. Mioyo yetu yadunda-dunda kwa sababu ya uchovu. Twafurahi kama nini tufikapo mwisho wa safari yetu! Lakini sasa kazi halisi yaanza. Mfanyakazi aliyezoezwa hukata miti iliyoshambuliwa na wadudu kwa ustadi. Kisha, wafanyakazi wengine hukatakata miti hiyo vipande-vipande na kuichoma. Sharti ganda lake lichomeke kabisa ili kuua mabuu. Uwadiapo wakati wa mlo wa mchana, twafurahia kuota moto kwa sababu ya halijoto ya nyuzi Selsiasi –20. Twauzingira moto na kupasha moto mikate yetu yenye nyama iliyoganda. Kisha twarudi kazini. Hata hivyo, muda si muda utusitusi walifunika anga la majira ya baridi kali, hivyo twaamua kurejea nyumbani.”
Kufanya Kazi Nyikani
Kazi ya wafanyakazi wa msitu ni ngumu. Watu hawa wenye ustadi hukabiliana na magumu, na kufurahia uumbaji unaowazunguka. Hiyo yatia ndani mandhari yenye kuvutia na visa vya kusisimua vya kukutana na wanyama wa pori. Wanyama wengine hawadhuru, kwa mfano wakati kwale anapopuruka akipiga kelele kutoka kwenye theluji chini ya miguu yako au kuchakuro aliyeshtuka anapotoka mbio shimoni na kuingia katika mguu wa suruali ya mfanyakazi, na kumtia wasiwasi mwingi. Hata hivyo, visa vingine vyaweza kuwa hatari sana—mtu aweza kufukuzwa na dubu mkubwa mkali au dubu mweusi. Lakini kwa kawaida, hatari zaweza kupunguzwa kupitia elimu na mazoezi, na wafanyakazi wanaweza kufurahia mazingira ya nyikani pasipo woga.
Maendeleo makubwa ya kitekinolojia yanafanywa ili kudhibiti mali-asili za dunia zenye thamani. Watu wengi wenye kudhamiria wanajitahidi kulinda na kuhifadhi miti yetu yenye thamani kwa kudhibiti wadudu kama vile mountain pine beetle. Bila shaka, kuna mengi zaidi ya kujifunza kuhusu misitu yetu yenye kuvutia sana. Twatamani wakati ambapo tutaweza kutunza misitu kupatana na ubuni wake wa asili.
[Sanduku[Mchoro katika ukurasa wa 22]
Duru ya Maisha ya Mountain Pine Beetle
Katika kizio cha kaskazini beetle wa kike mkomavu atoboa tundu katika ganda la msonobari aina ya lodgepole hadi kufikia sehemu laini mtini. Baada ya kujamiiana na wa kiume, yeye hutaga mayai 75 hivi. Wakati huohuo yeye humwaga kuvu ya buluu katika sehemu laini za mti huo ili kuzuia mtiririko wa utomvu unaoweza kuua wadudu hao. Kisha mayai hayo huangua mabuu yafananayo na funza ambaye hutafuna (tishu tata) ya mti. Mti huo hufa juma moja baada ya kushambuliwa na beetle, kwa sababu ya kuvurugika kwa usafirishaji wa maji na lishe. Mabuu huibuka wakati wa kiangazi kisha huruka na kushambulia miti mipya na kurudia duru hiyo.
[Mchoro]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mdudu aliyekomaa
Mayai
Buu
Pupa
[Picha katika ukurasa wa 22, 23]
Picha iliyopigiwa karibu ya mti ulioharibiwa
Miti iliyoathiriwa
Mifereji ya utomvu