Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mnyama Mwenye Mbeleko Anayerukaruka

Mnyama Mwenye Mbeleko Anayerukaruka

Mnyama Mwenye Mbeleko Anayerukaruka

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

“KILA siku niliporejea nyumbani kutoka shuleni, Joey, kangaruu mnyama-kipenzi wangu, alikuwa akiketi na kunisubiri langoni,” akumbuka John. “Mara baada ya kufungua lango, angenirukia na kunikumbatia kwa miguu yake ya mbele, nami ningemkumbatia. Tungewasiliana kwa ishara zilizosema, ‘Nimeterema kukuona!’ Kisha Joey angekimbia huku na kule meta kadhaa kwenye njia inayoelekea nyumbani kama mbwa mwenye msisimuko, na kuendelea hadi tulipofika kwenye nyumba.”

Watu wanaoishi karibu na vichaka vya Australia wanaruhusiwa na sheria ya nchi kumiliki kangaruu vipenzi, kama familia ya John ilivyofanya. Kwa kawaida, kangaruu hao huwa yatima waliookolewa wakiwa wachanga baada ya mama zao kuuawa, labda walipokuwa wakivuka barabara. Hata ingawa John alimwita kangaruu wake, “joey” kwa kweli, hilo ni jina la kawaida la kangaruu mchanga katika Kiingereza.

Bila shaka, familia inayomtunza kangaruu mchanga yataka kumfanya astarehe upesi. Kwa hiyo, jambo la kwanza wanalofanya ni kumtafutia mbeleko. Wanateua mahali palipofunikwa—mbali ifaavyo na meko—na hapo wanaangika mfuko mgumu wa nguo wenye tundu linaloshabihi mbeleko ya mama kangaruu. Kisha wao humtia kangaruu huyo mchanga ndani ya mbeleko na kupewa chupa ya maziwa ya pekee, yaliyo vuguvugu. Kupitia njia hii kangaruu wengi wachanga huwezeshwa kuokoka. Muda si muda wao huzoea mbeleko yao mpya, wakitumbukia ndani kwa kichwa, kana kwamba ni mbeleko ya mama yao.

Kangaruu Ni Mnyama wa Aina Gani?

Wanyama wanaolea watoto wao katika mbeleko huitwa marsupial kwa Kiingereza. Kuna jamii 260 za wanyama wenye mbeleko, kutia ndani kangaruu, koala, wombat, bandicoot, na opossum, jamii pekee zinazoishi katika Amerika Kaskazini. Yaeleweka kwamba wavumbuzi wa kale walishindwa kuwaeleza watu nyumbani kuhusu wanyama hawa wa ajabu hasa kangaruu. Aliyekuwa wa kwanza kuandika jina “kangaruu” katika Kiingereza alikuwa mvumbuzi Mwingereza Kapteni James Cook. Alimlinganisha mnyama huyo na ‘mbwa-mwindaji anayeruka kama sungura au kulungu.’ Kangaruu aliye hai alipoonyeshwa baadaye huko London, aliwasisimua sana watu.

Kangaruu wana masikio makubwa yanayozunguka kwenye kichwa kama cha kulungu. Miguu yao midogo ya mbele lakini yenye nguvu inashabihi mikono ya mwanadamu, hasa kangaruu anaposimama wima. Kangaruu pia wana nyonga kubwa zenye misuli yenye nguvu; mkia mrefu, mnene, wenye mapindi; na bila shaka, miguu mikubwa—ambayo imewapa jina jingine, “Macropodidae,” linalomaanisha “miguu mirefu.”

Jamii 55 za wanyama wenye miguu mirefu huwa na ukubwa mbalimbali kutoka kwa ukubwa wa mwanadamu hadi kufikia ukubwa wa panya. Wanyama wote wa jamii hiyo huwa na miguu mifupi ya mbele na miguu mirefu ya nyuma ya kurukaruka. Kangaruu wekundu, kangaruu wa kijivu, na wallaroo, au euro, ndio wakubwa zaidi ya wote. Kangaruu mmoja mwekundu wa kiume alikuwa na uzito wa kilogramu 77 na urefu wa zaidi ya meta mbili kuanzia pua yake hadi ncha ya mkia wake. Jamii zenye kangaruu wadogo zaidi huitwa wallabie.

Je, umewahi kusikia au kuona kangaruu anayeishi mtini? Amini usiamini, kuna “tumbili” katika jamii ya kangaruu—kangaruu wa mtini. Wanyama hawa wepesi, wenye miguu mifupi huishi katika misitu ya kitropiki ya mvua huko New Guinea na kaskazini-mashariki mwa Australia, nao waweza kuruka umbali wa meta tisa kutoka mti mmoja hadi mwingine. Wao hushuka chini msituni ili kula hasa mimea na funza wakati wa usiku.

Wenye Kasi, Madaha na Wepesi

Wanaposonga polepole, kangaruu huonekana kuwa wazito na wasio stadi. Mkia wao na miguu mifupi ya mbele hutegemeza uzito wao wanaporuka kwa miguu ya nyuma. Lakini wao hukimbia kwa madaha. Wanaporuka mbele kwa mwendo wa kilometa 50 hivi kwa saa, wao hutumia mkia wao mkubwa kujisawazisha. Kitabu cha The World Book Encyclopedia, chasema kwamba wanaweza “kufikia mwendo wa kasi sana wa zaidi ya kilometa 60 kwa saa.” Kangaruu mkubwa anaporuka hatua moja kwa mwendo wa kasi aweza kufikia umbali wa meta 9 hadi meta 13.5—mruko unaokaribia kupuruka!

Licha ya kuruka kasi, kangaruu huhifadhi nishati yao pia. Profesa Uwe Proske, wa Chuo Kikuu cha Monash huko Melbourne, Australia, asema kwamba kangaruu hutumia nishati kidogo zaidi anaporukaruka kwa mwendo wa kasi kuliko anaporukaruka polepole. Proske aligundua pia kwamba “kangaruu anayeruka kwa mwendo wa kilometa 20 au zaidi kwa saa, hutumia kiasi kidogo cha nishati kuliko [mnyama mkomavu mwenye miguu minne kama mbwa au kulungu] mwenye uzito sawa na anayekimbia kwa mwendo huohuo.” Kangaruu aweza kusafiri mwendo wa mbali bila kuchoka kwa sababu ya kutumia kiasi kidogo cha nishati anapokimbia. Lakini kangaruu huweza kukimbiaje kwa kutumia kiasi kidogo cha nishati?

Ni kwa sababu ya kano ndefu zinazounganisha misuli ya Shavu la Mguu. “Ni kana kwamba kangaruu wanarukaruka juu ya springi mbili,” asema Proske. Kano zinazounganisha misuli ya shavu la mguu wa kangaruu hunyooka anapotua na kubana anaporuka sawa na zile zinazounganisha misuli ya mwanadamu ya shavu la mguu. Kangaruu hurukaruka mara zilezile kwa sekunde (miruko miwili hivi kwa kangaruu mwekundu) katika mwendo mbalimbali. Wao huruka hatua ndefu zaidi wanapoenda kasi. Kangaruu hutenda tofauti anaposhtuliwa. Wakati huo yeye hukimbia ghafula kwa hatua fupi nyingi, ili asonge kwa kasi.

Kangaruu ni waogeleaji hodari pia. Mbali na kutumia miguu ya nyuma yenye nguvu kujisogeza mbele wao pia hujisukuma kwa kutikisa mkia wao. Wanaposhambuliwa na mbwa, kangaruu wana sifa ya kutumia ustadi wao majini kwa kujitumbukiza katika kidimbwi au mto. Kangaruu humzamisha mara moja mbwa yeyote anayemfuata majini akitumia miguu yake ya mbele yenye nguvu na nyayo zenye vidole vitano vyenye kucha kali. John, aliyetajwa mwanzoni, alikuwa na mbwa wawili ambao nusura wazamishwe na kangaruu dume mwenye hasira alipopambana nao katika tangi dogo la maji la familia yake.

Maajabu ya Uzazi ya Wanyama Wenye Mbeleko

Ingawa kangaruu wakomavu huwa wenye afya na nguvu, wao huzaliwa pasina kukomaa nao huhitaji uangalifu mkubwa sana. Wao huzaliwa bila manyoya, vipofu, na viziwi nao hushabihi mnyoo wa rangi ya waridi mwenye urefu wa inchi moja hivi na uzito unaopungua aunsi moja. Ingawa hivyo, “mnyoo” huo mdogo hutambaa kwa silika katika manyoya ya mama yake hadi kwenye mbeleko kwa kutumia miguu ya mbele yenye kucha inayokomaa upesi na pia uwezo wa kunusa. Awapo ndani ya mbeleko, mtoto huyo hunyonya mojawapo ya matiti manne. Na mara moja chuchu huvimba kama mpira mdomoni mwa huyo mtoto mchanga, na kumshikilia kwa nguvu kwa majuma kadhaa. Mshiko wa nguvu unafaa kwa sababu ya njia ya mama yake ya kusafiri! Kwa kweli, mshiko huo ni thabiti sana hivi kwamba wachunguzi wa awali walidhani mtoto huyo mchanga alikua kutoka kwa titi hilo!

Bila shaka, kangaruu huyo mchanga atakua na kufikia hatua ya kuondoka kwenye mbeleko hatimaye, ingawa anatoka kwa muda mwanzoni. Hata hivyo, yeye hutoka kabisa kwenye mbeleko baada ya miezi saba hadi kumi anapoacha kunyonya. Acheni turudi nyuma hadi wakati kangaruu mchanga alipojishikilia kwenye titi ili tuone jambo jingine la kustaajabisha la uzazi wa kangaruu.

Siku chache baada ya kangaruu mchanga kujishikilia kwenye titi, mamaye huanza tena kujamiiana. Kiinitete kinachotokana na kujamiiana hukua kwa juma moja hivi, halafu kinakuwa bwete—tuseme ni kipindi cha kungoja—huku ndugu yake mchanga akiendelea kukua kwenye mbeleko. Yule kangaruu wa kwanza anayenyonya bado atokapo kwenye mbeleko, kiinitete kilicho katika tumbo la uzazi huanza kukua tena. Baada ya siku 30 za ujauzito, kangaruu huyo mchanga sana hujishikilia pia kwenye titi tofauti na lile linalonyonywa na nduguye mkubwa.

Utaratibu huo waonyesha jambo jingine la kustaajabisha kuhusu kangaruu. Mama humnyonyesha kangaruu mchanga zaidi maziwa tofauti na yule mkubwa. Kikigusia jambo hili, kichapo cha Scientific American chasema: “Maziwa hayo aina mbili yanayotokezwa na matiti mbalimbali hutofautiana sana katika kiasi na mfanyizo. Jinsi ambavyo hilo huwezekana chini ya homoni zilezile ni jambo linalotatanisha.”

Mahali pa Kuona Kangaruu

Ukitaka kuona kangaruu katika mazingira yao ya asili, lazima uzuru vichaka katika sehemu za mashambani za Australia mbali na miji. Kangaruu huweza kuonekana wakila nyasi na mimea wakiwa mmojammoja au katika vikundi vidogo au vikubwa vinavyosimamiwa na kangaruu dume wakubwa wanaoitwa boomer. Wakati unaofaa wa kuwaona ni alfajiri na mapema au wakati wa machweo kwa sababu kangaruu hupenda kula usiku na kupumzika kivulini (wasikoonekana) wakati wa mchana jua liwapo kali. Lakini huelekea kuwa na bidii siku nzima isiyo na jua kali. Vyovyote vile, hakikisha kwamba unabeba lenzi-darubini na darubini—kangaruu wa mwituni ni wanyama wenye haya mno.

Bila shaka, unaweza pia kuona kangaruu katika bustani nyingi za wanyama, hifadhi za wanyama wa pori, na mbuga za kitaifa kotekote katika Australia na katika nchi nyinginezo pia. Kangaruu hao si waoga sana kwa sababu wamewazoea wanadamu, na hivyo unaweza kupiga picha ukiwa karibu, labda hata kumpiga picha kangaruu mchanga akichungulia kutoka kwenye mbeleko ya mama. Watoto wakubwa wa kangaruu husisimua wanapotumbukia kwa kichwa ndani ya mbeleko, huku miguu mirefu ya nyuma ikichomoza nje bila utaratibu, na kumfanya mama kangaruu ashabihi mfuko wa ununuzi uliojaa pomoni. (Kangaruu wachanga huonekana wakiwa na miguu mikubwa mno!) Kangaruu dume mwenye kuvutia aweza hata kusimama wima kwa fahari karibu nawe. Nani ajuaye? Huenda hata ukaona kangaruu dume wakubwa wakisimama kadiri ya uwezo wa miguu yao myepesi na kupigana ndondi—pambano halisi la ndondi la kangaruu!

Lakini watu wengi huvutiwa kuona kangaruu dume mwekundu au wa kijivu akiruka na kwenda kwa mwendo wa kasi sana. Ingawa wanyama wengine waweza kukimbia kasi zaidi au kuruka juu zaidi, lakini hakuna mnyama mwingine yeyote mwenye sifa maridhawa kama nguvu, madaha, na uwezo wa kurukaruka kwa miguu miwili thabiti kama kangaruu.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kano ndefu zinazounganisha misuli ya Shavu la Miguu ndizo humwezesha kurukaruka