Familia Inapokumbwa na Ugonjwa wa Kudumu
Familia Inapokumbwa na Ugonjwa wa Kudumu
FURAHA ya familia ya Du Toit ni yenye kuvutia. Upendo mchangamfu wanaoonyeshana hupendeza sana. Ukikutana nao huwezi kujua wamevumilia magumu mengi mno.
Kwanza, kifungua-mimba wao, Michelle, alipokuwa na umri wa miaka miwili, Braam na Ann waligundua kwamba alikuwa na maradhi ya kudumu aliyorithi ambayo hudhoofisha misuli.
“Kwa ghafula,” aeleza mama huyo, aitwaye Ann, “utahitaji kujifunza namna ya kukabiliana na ugonjwa wa kudumu wenye kulemaza. Unagundua kwamba maisha ya familia hayatakuwa sawa tena.”
Lakini baada ya mwana na binti mwingine kuzaliwa, familia hiyo ilikumbwa na msiba mwingine. Siku moja watoto hao watatu walipokuwa wakicheza nje, wasichana wangu wawili walikuja nyumbani wakikimbia. “Mama! Mama!” wakalia. “Njoo upesi. Neil ana tatizo fulani!”
Alipokimbia nje, Ann aliona kichwa cha Neil mwenye umri wa miaka mitatu kikinyong’onyea upande mmoja. Hangeweza kusimamisha kichwa chake wima.
“Nilishtuka sana,” akumbuka Ann, “na nilitambua tatizo papo hapo. Nilishuka moyo sana kuona kwamba mvulana huyu mdogo mwenye afya angekabili ugumu wa kuishi na maradhi yanayodhoofisha misuli kama dada yake mkubwa.”
“Punde si punde ile shangwe ya kuanzisha familia yenye afya,” asema baba yao, Braam, “ilimalizwa na magumu makubwa sana ambayo tumepata kukabili.”
Hatimaye Michelle alikufa kwa matatizo yaliyosababishwa na ugonjwa wake, licha ya matibabu bora kabisa aliyopokea hospitalini. Alikuwa na umri wa miaka 14 tu wakati huo. Neil anaendelea kupambana na athari za ugonjwa wake.
Hilo lazusha swali hili, Familia kama ile ya Du Toit huweza kukabilianaje na magumu ya kuwa na mshiriki mmoja wa familia aliye na ugonjwa wa kudumu? Ili kujibu swali hilo, acheni tuchanganue baadhi ya njia ambazo familia huathiriwa na ugonjwa wa kudumu.