Saa ya Pekee Huko Prague
Saa ya Pekee Huko Prague
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA CHEKI
Wachuuzi wa barabarani wajitahidi kuvutia watalii wanaopita. Vicheko, mazungumzo katika lugha mbalimbali, na mvumo wa muziki umesambaa barazani. Ngoja kidogo! Mbona umati unakimya? Saa yakaribia kugonga, na wote wanakodolea macho madirisha mawili ya buluu kwenye mnara wa jengo la baraza la mji. Kwa ghafula madirisha hayo yafunguka, na mifano inayowakilisha mitume wa Kristo yatokea. Petro akiwa na ufunguo mkubwa ndiye anayeongoza mlolongo huo. Mifano 12 inapoibuka dirishani, miwili-miwili, yaonekana ni kana kwamba inachunguza umati ulioko chini.
TUNATAZAMA tamasha ya saa ya falaki kwenye Jengo la Kale la Baraza la Mji huko Prague, katika Jamhuri ya Cheki. Mtambo huo wa ajabu huanza kufanya kazi kila saa inapogonga toka saa mbili asubuhi hadi saa mbili usiku. Mbali na mlolongo wa mitume, mifano mingine husogea kwenye saa yenyewe. Hiyo huwakilisha mambo waliyohofu
sana wakazi wa Prague. Upande mmoja, una mtu Mchoyo anayepima uzito wa kibeti chake kwa mikono, anawakilisha pupa. Karibu naye kuna Ubatili—mtu anayejiangalia katika kioo. Mchoyo na Ubatili wainama kwa majivuno. Upande mwingine wa saa una gofu la mtu—Kifo—ambaye anapiga kengele kwa mkono mmoja wenye mifupa mitupu na kuinamisha shisha kwa ule mwingine. Wakati wote huo, gofu hilo hufungua na kufunga taya zake zenye meno na kumwinamia Mturuki—anayewakilisha mashambulizi—ambaye amesimama karibu naye. Mturuki huyo anatikisa kichwa chake, huku akikataa kuambatana naye.Kuna hadithi juu ya mbayuwayu aliyeruka na kutumbukia kinywani mwa gofu hilo kilipofungika mwishowe. Mbayuwayu huyo asiyekuwa na la kufanya alifungiwa kinywani kwa saa moja kabla gofu hilo halijafungua kinywa tena! Ikiwa watu wanaoishi katika enzi ya kisasa ya kompyuta huvutiwa sana na mtambo huo wa kustaajabisha, sembuse watu walioishi mamia ya miaka iliyopita?
Kuichunguza kwa Umakini Saa Hiyo
Kwa kawaida watalii hukazia fikira mno mifano inayosogea, ambayo iliongezwa kwenye saa hiyo karne zilizofuata baada ya kubuniwa. Lakini sehemu bora zaidi na ya kale zaidi ya saa hiyo ni uso wake wa falaki. Waweza kutufunza nini? Kwanza, wakati. Duara nyeusi iliyo pembeni ina tarakimu nene za dhahabu zinazotokana na mfumo wa kale wa Wacheki wa kugawanya siku kwa saa 24 kuanzia wakati wa machweo. Duara hiyo huzunguka hivi kwamba sikuzote saa ya 24 husadifiana na machweo, bila kujali msimu. Tarakimu za Kiroma zilizo katika duara ya nje hugawanya siku katika vipindi viwili vya saa 12 kila kipindi, huku saa sita mchana ikiwa juu na saa sita usiku ikiwa chini. Vidole vya akrabu ya dhahabu huashiria saa.
Uso wa falaki huwa pia na bamba kubwa la dhahabu linalozunguka kuashiria mzingo wa jua, ilhali tufe dogo huonyesha sura za mwezi. Pete ndogo ya katipande yenye ishara za makundi-nyota huashiria mwendo wa dunia katika anga lenye nyota. Tufe la dunia lenye mistari ya kutoka kaskazini hadi kusini, mistari sambamba, na pembe za dunia liko katikati ya uso wake, nayo Prague iko katikati. Uso huo una duara tatu zinazowakilisha ikweta na Tropiki ya Kansa na ya Kaprikoni. Hivyo uso wa saa hiyo huonyesha mahali barabara pa dunia, mwezi, jua, na nyota kwa mwaka wote. Chini tu ya uso huo kuna bamba la kalenda, lenye mandhari mbalimbali zinazoonyesha kila mwezi katika mwaka. Bamba la kalenda huonyesha tarehe kwa kusonga
hatua moja kati ya hatua 365 saa sita kila usiku, isipokuwa usiku mmoja tu mwaka unapokuwa mrefu.Mtambo wa saa hiyo una mfumo tata wa magurudumu makubwa kwa madogo. Mtambo huo tata hutunzwa na fundi, anayeuchunguza kikamili kila juma.
Historia ya Saa ya Falaki
Kuna hekaya chungu nzima juu ya saa ya Prague ya falaki. Hekaya moja husema kwamba mtu fulani Mahiri aitwaye Hanuš ndiye aliyeitengeneza. Saa hiyo ilikuwa bora hivi kwamba wakuu wa mji walihofia kutengenezwa kwa saa nyingine kama hiyo kwingineko, na hivyo kuharibu sifa ya Prague. Ili kumzuia kufanya hivyo, walikodi watu wamshambulie na kumpofusha Hanuš aliye Mahiri. Hekaya hiyo hufikia tamati wakati Hanuš anayekabili kifo anapojinyoosha na kushika magurudumu ya saa hiyo na kuiharibu.
Lakini, hii ni hadithi iliyotiwa chumvi. Ijapokuwa hivyo, Hanuš alikuwa mtu halisi, fundi wa saa huko Prague tokea mwaka wa 1475 hadi 1497. Kwa miaka mingi wataalamu waliamini kwamba yeye ndiye aliyetengeneza saa ya falaki. Hata hivyo, utafiti wa karibuni huonyesha kwamba Mikuláš kutoka Kadaň ndiye aliyetengeneza saa hiyo mapema mwaka wa 1410. Hanuš aliitengeneza upya mnamo 1490. Tangu karne ya 16, mtambo wa saa hiyo umerekebishwa na kutengenezwa upya mara kadhaa. Lakini nyingi za sehemu zake zingalipo tangu ilipotengenezwa upya mwaka wa 1865.
Vita ya Ulimwengu ya Pili ilipokoma, majeshi ya Wanazi yaliteketeza Jengo la Kale la Baraza la Mji yalipokuwa yakiondoka Prague. Saa hiyo ya falaki iliharibiwa vibaya sana. Baada ya vita mapendekezo mawili muhimu ya kutengeneza upya saa hiyo yalifikiriwa—kuirejesha kwenye hali yake ya kwanza au kuitia uso mpya na mifano mipya yenye maana tofauti. Katika Prague, dhana ya kutoamini kuwapo kwa Mungu ilikuwa inaenea kasi, na viongozi Wakomunisti hawakupendelea mifano ya mitume. Hata hivyo, kabla ya kubadili umbo lake, mafundi stadi watatu wa saa walithibitisha kwamba saa hiyo ingeweza kurekebishwa, na kwa hiyo ikarejea umbo lake la kabla ya vita. Kwa hiyo, leo bado kuna mchoyo, gofu la mtu, Mturuki, na mitume badala ya, tuseme, seremala, mwashi, mshonaji, na dobi wa kike.
Jogoo Awika Hatimaye
Mitume 12 waandamana katika saa ya falaki, lakini mambo fulani si ya Kibiblia. Mahali pa Yuda Iskariote na Yakobo mwana wa Alfayo pamechukuliwa na Paulo na Barnaba, ambao hawakuwa miongoni mwa wale 12 wanaotajwa katika Biblia. (Matendo 1:12-26) Kichwa cha kila mtume kimezingirwa na duara ya mwangaza—ishara ya kipagani ambayo haikutumiwa na Wakristo wa mapema.
Baada ya mfano wa mwisho wa mtume kupita, jogoo aliyefunikwa kwa dhahabu aliye juu ya madirisha anawika. Kengele yalia saa igongapo, madirisha yafunga, na umati waanza kutawanyika. Je, ungependa kuona tamasha hiyo tena? Tutahitaji kusubiri kwa saa nyingine nzima. Kwa sasa, twaweza kuchunguza uso wa hiyo saa, ambao umekuwa ukivutia watalii wengi kuzuru Jengo la Kale la Baraza la Mji wa Prague kwa miaka 600 hivi.
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 17]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
USO WA FALAKI
Hivi sasa ni saa 6:57 alasiri
Machweo saa 11:21 jioni
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 18]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
BAMBA LA KALENDA
Tarehe ionyeshwayo ni Januari 1
[Picha katika ukurasa wa 16]
Ubatili na Mchoyo
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kifo na Mturuki