Kutafuta Chembe ya Urithi “Isiyokufa”
Kutafuta Chembe ya Urithi “Isiyokufa”
WATU wa ustaarabu mbalimbali wana hadithi na hekaya zinazojaribu kueleza hali ya kufa ya wanadamu. Kwa mfano, katika Afrika, kuna hekaya moja isemayo kwamba kinyonga alitumwa na Mungu apelekee wanadamu hali ya kutokufa, lakini akasafiri polepole sana hivi kwamba mjusi mwingine, aliyekuwa na ujumbe wa kifo, akamtangulia. Wanadamu wanaodanganyika kwa urahisi walikubali ujumbe wa mjusi huyo na hivyo wakapoteza hali ya kutokufa.
Hali kadhalika, kwa karne nyingi wanafalsafa wamejaribu kujibu swali, Kwa nini mwanadamu hufa? Katika karne ya nne K.W.K., mwanafalsafa Mgiriki Aristotle alifundisha kwamba ili mtu aendelee kuwa hai ilitegemea uwezo wa mwili wa kusawazisha joto na baridi. Alisema: “Kifo hutokea daima wakati joto linapokosekana kwa kiasi fulani.” Kwa upande mwingine, Plato alifundisha kwamba mwanadamu ana nafsi isiyoweza kufa ambayo huendelea kuishi mwili unapokufa.
Leo, licha ya maendeleo makubwa sana ya sayansi ya kisasa, wanabiolojia wameshindwa kabisa kujibu swali la kwa nini tunazeeka na kufa. Gazeti The Guardian Weekly la London lilisema: “Mojawapo ya mambo makubwa yasiyoeleweka ya sayansi ya kitiba halijawa kwa nini watu hufa kutokana na maradhi ya moyo au kansa: lilikuwa kwa nini watu hufa hata wasipokuwa na kasoro yoyote. Ikiwa chembe za mwanadamu hujigawanya, na kuendelea kujifanya upya kwa kujigawanya kwa miaka 70 au zaidi, kwa nini zote ziache kuongezeka kwa ghafula?”
Katika jitihada yao ya kufahamu kuzeeka, wataalamu wa chembe za urithi na wanabiolojia wa molekuli wameelekeza fikira zao kwa chembe. Wanasayansi wengi wanaona kwamba wanaweza kufahamu jinsi wanadamu wanavyoweza kuishi maisha marefu zaidi kwa kuchunguza chembe hizi zisizoonekana kwa macho. Mathalani, wengine wanatabiri kwamba kubadilisha maumbile ya chembe za urithi kutawaruhusu wanasayansi wakabiliane kwa mafanikio na kansa na maradhi ya moyo hivi karibuni. Lakini je, sayansi imekaribia kutimiza tamaa ya wanadamu ya kuishi milele?
Kufunua Siri za Chembe
Vizazi vilivyopita vya wanasayansi vilijaribu kufunua siri za chembe, lakini havikuwa na vifaa vinavyohitajika kwa kazi hiyo. Wanasayansi wameweza kuchunguza chembe kwa undani na kuona sehemu zake nyingi za msingi katika karne iliyopita tu. Wamepata nini? “Chembe,” asema mwandishi wa makala za sayansi Rick Gore, “imekuwa ulimwengu mdogo.”
Ili ufahamu jinsi chembe ilivyo tata kupindukia, fikiria kwamba kila moja imefanyizwa na matrilioni ya visehemu vidogo zaidi vinavyoitwa molekuli. Hata hivyo, wanasayansi wanapotazama muundo wa chembe, wanaona utaratibu wa ajabu na uthibitisho wa ubuni. Philip Hanawalt, profesa msaidizi wa elimu ya chembe za urithi na biolojia ya molekuli katika Chuo Kikuu cha Stanford, asema: “Ili chembe sahili zaidi iweze kukua kwa njia ya kawaida huhitaji makumi ya maelfu ya utendeano wa kemikali utukie kwa njia ya utaratibu.” Pia asema kwamba: “Mambo ambayo hutimizwa kwa njia ya silika na viwanda hivi vidogo mno vya kemikali
yapita kwa mbali uwezo wa mwanasayansi katika maabara yake.”Basi, wazia kazi yenye kutisha ya kujaribu kurefusha maisha ya binadamu kwa kutumia njia za asili. Ingehitaji si ufahamu wa kina tu juu ya vitu vinavyofanyiza chembe za urithi bali pia uwezo wa kuelekeza kwa ustadi chembe hizo! Acheni tuchunguze kwa ufupi chembe ya mwanadamu ili kueleza ugumu unaokabili wanabiolojia.
Chembe za Urithi Ndizo Huamua
Ndani ya kila chembe kuna kituo tata cha kuelekeza kinachoitwa kiini. Kiini huelekeza utendaji wa chembe kwa kufuata maagizo fulani yaliyopangwa. Maagizo hayo huhifadhiwa kwenye chembe-uzi.
Chembe-uzi zetu zimefanyizwa hasa kwa protini na asidi ya deoksiribonyukilia au kwa ufupi DNA. * Ijapokuwa wanasayansi wamejua DNA tangu mwisho-mwisho wa miaka ya 1860, walipata kufahamu muundo wake wa molekuli mwaka wa 1953. Ijapokuwa hivyo, ilichukua muda wa zaidi ya mwongo mmoja kabla wanasayansi hawajaanza kuelewa “lugha” inayotumiwa na molekuli za DNA ili kuwasilisha habari zinazohusu urithi.—Ona sanduku, kwenye ukurasa wa 22.
Miaka ya 1930, wataalamu wa elimu ya chembe za urithi waliona kwamba katika ncha ya kila chembe-uzi kuna mfuatano mdogo wa DNA unaosaidia kuimarisha chembe-uzi. Vijipande hivi vya DNA vinavyoitwa telomere kutokana na neno la Kigiriki teʹlos (mwisho) na meʹros (sehemu), hufanya kazi kama ncha inayolinda kamba ya viatu. Bila telomere, chembe-uzi zetu zingetengana na kuvunjika katika visehemu vifupi-vifupi, kushikamana, au zikose kuimarika.
Hata hivyo, baadaye watafiti waligundua kwamba katika chembe nyingi za aina mbalimbali, telomere zilifupika zaidi baada ya kila mgawanyo. Hivyo, baada ya kujigawanya mara 50 hivi, telomere za chembe zilipungua na kuwa chenga ndogo mno, kisha chembe hizo zikaacha kujigawanya na hatimaye zikafa. Katika miaka ya 1960 Dakt. Leonard Hayflick aliripoti kwa mara ya kwanza kwamba chembe hujigawanya hadi idadi fulani hususa kabla ya kufa. Hivyo, tukio hilo la kisayansi sasa hurejezewa na wanasayansi wengi kuwa kikomo cha Hayflick.
Je, Dakt. Hayflick aligundua kisababishi cha kuzeeka kwa chembe? Wengine walifikiri hivyo. Mwaka wa 1975 kichapo Nature/Science Annual kilisema kwamba wavumbuzi katika uwanja wa kuzeeka waliamini kwamba “viumbe wote walio hai wana utendanaji fulani wa kemikali ulioratibiwa sawasawa, ambao hudhoofika hatua kwa hatua mtu azeekapo.” Kwa kweli, kulianza kuwa na tumaini kwamba hatimaye wanasayansi walikuwa wanakaribia kugundua kinachosababisha uzee.
Katika miaka ya 1990, watafiti waliokuwa wakichunguza chembe zinazosababisha kansa katika mwanadamu waligundua kidokezi fulani cha maana kuhusu “saa ya chembe.” Waliona kwamba chembe zenye kuleta madhara kwa njia fulani zilijifunza kushinda “saa [zao] za chembe” na kujigawanya kwa muda usio dhahiri. Ugunduzi huo ulifanya wanabiolojia waelekeze
fikira tena kwenye kimeng’enya kisicho cha kawaida, kilichogunduliwa mara ya kwanza katika miaka ya 1980 na ambacho kilipatikana baadaye katika aina nyingi za chembe za kansa. Kimeng’enya hicho kinaitwa telomerase. Hufanya nini? Kwa njia sahili, telomerase yaweza kulinganishwa na ufunguo unaosawazisha “saa” ya chembe kwa kurefusha telomere zake.Je, Kuzeeka Kutakoma?
Punde si punde utafiti wa telomerase ukawa suala lenye kubishaniwa vikali katika uwanja wa biolojia ya molekuli. Ilidokezwa kwamba ikiwa wanabiolojia wangetumia telomerase kuzuia kunywea kwa telomere wakati chembe ya kawaida inapojigawanya, labda kuzeeka kungekomeshwa au kucheleweshwa kwa kiwango fulani. Kwa kupendeza, Geron Corporation News charipoti kwamba watafiti wanaochunguza telomerase katika maabara tayari wamedhihirisha kwamba chembe za kawaida za mwanadamu zaweza kubadilishwa na kuwa na “uwezo wa kuongezeka kwa muda usio dhahiri.”
Licha ya maendeleo hayo, hatuwezi kuwa na hakika kwamba wakati ujao karibuni, wanabiolojia watafahamu namna ya kurefusha maisha yetu kwa kutumia telomerase. Kwa nini isiwe hivyo? Sababu moja ni kwamba kuzeeka huhusisha mengi zaidi kuliko kudhoofika kwa telomere. Mathalani, yafikirie maelezo ya Dakt. Michael Fossel, mwandishi wa kitabu Reversing Human Aging: “Tukishinda uzee kama tuujuavyo sasa, bado tutazeeka kwa njia fulani mpya tusiyofahamu. Kwa kurefusha telomere zetu kwa muda usio dhahiri, twaweza kuepuka maradhi yanayoletwa na uzee, hata hivyo mwishowe tutazeeka na kufa.”
Kwa kweli, yaonekana kuna mambo fulani ya kibiolojia yanayochangia kuzeeka. Lakini kwa sasa wanasayansi hawawezi kupata majibu yake. Leonard Guarente wa Taasisi ya Tekinolojia ya Massachusetts asema: “Kwa sasa kuzeeka bado ni fumbo.”—Scientific American, Majira ya Kupukutika 1999.
Huku wanabiolojia na wataalamu wa elimu ya chembe za urithi wakiendelea kuchunguza chembe ili kuelewa ni kwa nini wanadamu huzeeka na kufa, Neno la Mungu hufunua sababu halisi. Husema hivi kwa njia sahili: “Kupitia mtu mmoja dhambi iliingia katika ulimwengu na kifo kupitia dhambi, na hivyo kifo kikasambaa kwa watu wote kwa sababu wote walikuwa wamefanya dhambi.” (Waroma 5:12) Naam, kifo cha kibinadamu hutokezwa na kisababishi ambacho sayansi haitaweza kamwe kuponya—dhambi iliyorithiwa.—1 Wakorintho 15:22.
Kwa upande mwingine, Muumba wetu anaahidi kutangua matokeo ya dhambi iliyorithiwa kwa kutumia dhabihu ya fidia ya Kristo. (Waroma 6:23) Tunaweza kuwa na hakika kwamba Muumba wetu ajua namna ya kukomesha kuzeeka na kifo, kwani Zaburi 139:16 husema: “Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; chuoni mwako ziliandikwa zote pia.” Ili kuhakikisha hilo, Yehova Mungu alianzisha msimbo wa chembe za urithi na kuuandika kwa njia ya kitamathali. Hivyo, kwa wakati wake uliowekwa, atahakikisha kwamba chembe zetu za urithi zitaruhusu wale wanaotii matakwa yake waiishi milele.—Zaburi 37:29; Ufunuo 21:3, 4.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 12 Kwa ufafanuzi kamili wa DNA, ona Amkeni!, Septemba 8, 1999, ukurasa wa 5-10.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
“LUGHA” YA DNA
Visehemu vya msingi, au “herufi,” za lugha ya DNA ni misombo ya kemikali inayoitwa misingi. Kuna aina nne za misingi: thymine, adenine, guanine, na cytosine, ambazo kwa kawaida hufupishwa kuwa T, A, G, na C. “Ione misingi hiyo minne kama herufi katika alfabeti ya herufi nne,” lasema gazeti National Geographic. “Kama vile sisi hupanga herufi za alfabeti na kutokeza maneno yenye maana, herufi A, T, G, na C ambazo hufanyiza chembe zetu za urithi hupangwa katika ‘maneno’ yenye herufi tatu yanayoweza kusomwa na chembe.” Kisha “maneno” ya chembe ya urithi hufanyiza “sentensi” ambazo huiambia chembe jinsi ya kutengeneza protini mahususi. Mfuatano na muungano wa herufi za DNA huamua ikiwa protini itatengeneza kimeng’enya kitakachokusaidia kumeng’enya mlo wako wa jioni, kinga-mwili ya kupigana na ambukizo, au yoyote kati ya maelfu ya protini zilizo mwilini mwako. Basi haishangazi kwamba kitabu The Cell hurejezea DNA kuwa “programu ya msingi ya uhai.”
[Picha katika ukurasa wa 21]
Ncha za chembe-uzi (zinazoonyeshwa hapa zikiwaka) huruhusu chembe ziendelee kujigawanya
[Hisani]
Courtesy of Geron Corporation