Simulizi la Mito Miwili
Simulizi la Mito Miwili
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA INDIA
Mito miwili iliyo muhimu kwa uhai katika bara Hindi, huandaa riziki kwa mamia ya mamilioni ya watu. Kila mto huanzia kwenye maeneo ya barafu ya safu ya milima mirefu zaidi ulimwenguni, na kutiririka taratibu kwa umbali wa zaidi ya kilometa 2,400 kupitia nchi mbili. Mito hiyo huishia katika bahari mbili tofauti. Kila mto ulikuwa chimbuko la ustaarabu wa kale. Kila mto ulihusiana na kuanza kwa dini kuu. Kila mto huthaminiwa na wanadamu kwa sababu ya faida zake, na mmoja unaabudiwa, hata leo. Inaitwaje? Mto Indus na Ganges, huo wa mwisho huitwa Ganga hapa India.
USTAARABU wa kale ulianzia karibu na mito kwa sababu maji ni muhimu kwa uhai na usitawi wa mwanadamu. Mambo hakika ya kale yaweza kufichwa na hekaya kwa sababu nyakati nyingine mito ilionwa kuwa miungu ya kiume na miungu ya kike. Ndivyo ilivyo kuhusu historia ya Mto Indus na Ganga, ambao pia huitwa Ganga Ma (Mama Ganga) hapa India.
Mlima Kailash wenye urefu wa meta 6,714 na Ziwa Manasarovar lililo karibu, huonwa na Wahindi na Wabudha kuwa makao ya miungu. Kwa muda mrefu, iliaminika kuwa mito mikubwa minne ilitiririka kutoka kwenye vinywa vya wanyama ziwani. Indus ulikuwa mto wa simba, na Ganga ulikuwa mto wa tausi.
Watibet hawakuwakaribisha wavumbuzi wageni. Hata hivyo, mnamo mwaka wa 1811, daktari Mwingereza aliye mpasuaji wa mifugo ambaye aliajiriwa na East India Company alivinjari nchini kwa kujificha. Aliripoti kwamba hakuna mito yoyote iliyotiririka kutoka kwa Manasarovar, ingawa vijito kadhaa kutoka milimani viliingia ndani yake. Vyanzo vya Mto Indus na Ganga vilivumbuliwa mwanzoni mwa karne ya 20 tu. Mto Indus huanzia Tibet, kaskazini ya Milima ya Himalaya, na Ganga huanzia kwenye pango la barafu katika miteremko ya milima ya Himalaya kaskazini mwa India.
Chimbuko la Ustaarabu wa Kale
Yaaminika kwamba wakazi wa kale zaidi wa bara Hindi walielekea upande wa mashariki na kuingia katika Bonde la Indus. Waakiolojia wamevumbua magofu ya ustaarabu wa hali ya juu sana katika eneo la Harappa na Mohenjo-Daro humo bondeni. Uvumbuzi huo uliofanywa katika miongo ya mapema ya karne ya 20, ulibadili maoni ya kwamba masetla wa awali huko India walitoka kwa makabila yasiyostaarabika ya wahamaji. Zaidi ya miaka 4,000 iliyopita, Ustaarabu wa Indus ulikuwa sawa na, au hata bora kuliko ule wa Mesopotamia. Masalio ya barabara zilizopangwa taratibu, nyumba za orofa na majengo makubwa ya makazi, mabomba na matangi bora ya maji machafu, maghala makubwa mno ya nafaka, mahekalu, na mabwawa ya kujitakasia kidesturi vyote vyathibitisha kwamba ulikuwa mji uliostaarabika kwelikweli. Pia kuna uthibitisho wa kuwapo kwa shughuli za kibiashara kati yake na Mesopotamia na Mashariki ya Kati, huku bidhaa kutoka umbali wa mamia ya kilometa barani zikisafirishwa kupitia Indus hadi Bahari ya Arabia.
Yaonekana kwamba kadiri karne zilivyopita misiba ya asili—labda matetemeko ya ardhi au mafuriko makubwa ya mito—iliharibu ustaarabu wa mjini wa Bonde la Indus. Hivyo wakawa dhaifu sana wasiweze kuzuia uvamizi mkubwa wa makabila ya wahamaji ya Asia ya Kati,
ambao kwa kawaida huitwa Waarya. Waliwafukuza wakazi wengi wa mji kutoka mtoni, hivi kwamba utamaduni wa kale uliokuwa umesitawi kuzunguka Indus ukaelekea kusini mwa India, ambako leo kuna Wadravidi, mojawapo ya makabila yenye watu wengi huko India.Makabila fulani ya Kiarya yalielekea mashariki mwa India na kuishi katika uwanda wa Mto Ganga. Hivyo wakazi Waarya wa barani walianzisha utamaduni wao wa pekee kaskazini mwa India, ulioshirikishwa hasa na Mto Ganga, na ungalipo leo.
Mito Miwili na Dini Mbili
Vitu vya kiakiolojia huonyesha ulingano baina ya dini katika Bonde la Indus na dini za Mesopotamia. Baadhi ya kumbukumbu za Uhindu, ambao ulidhaniwa kwa muda mrefu kuwa dini ya Waarya, zimevumbuliwa katika magofu ya miji ya Indus. Dini ya Kihindu ilitokana na mchangamano wa miungu ya kale, na miungu na itikadi za Waarya. Mwanzoni Waarya waliona Mto Indus kuwa mtakatifu, lakini walipoelekea upande wa mashariki na kuanza kuishi kandokando ya Ganga, walianza kuabudu mto huo. Kadiri karne zilivyopita, miji kama vile Haridwar, Allahabad, na Varanasi ilisitawi kandokando ya Mto Ganga. Ilitegemea dini ya Kihindu. Leo mamia ya mahujaji humiminika kwenye vituo kama hivyo ili wajitumbukize kwenye maji ya Ganga, ambayo wanasema yanaponya na kutakasa.
Huku Uhindu ukianzia karibu na Mto Indus, Ubudha ulianzia karibu na Mto Ganga. Siddhārtha Gautama aitwaye Buddha, alianza mahubiri yake ya kwanza katika Sarnath, karibu na Varanasi. Yasemekana kwamba aliogelea na kuvuka sehemu pana ya Mto Ganga alipokuwa na umri wa miaka 79.
Mito Hiyo Ikoje Leo?
Maji ya mto ni muhimu sana leo kuliko yalivyokuwa miaka 4,000 iliyopita, watu walipohamia kwenye kingo za Mto Indus na Ganga ili kujiruzuku. Ni sharti mito hiyo isimamiwe kwa uangalifu ili iweze kuruzuku wakazi wengi wa India, Pakistan, na Bangladesh. (Ona ramani kwenye ukurasa wa 16-17.) Mikataba ya kimataifa imehitaji kufanywa kwa kuwa mito hiyo hupita katika nchi kadhaa. Miongoni mwa miradi mingine, Pakistan imejenga Bwawa la Tarbela lenye urefu wa kilometa tatu na kina cha meta 143 kwa ajili ya kilimo cha kumwagilia maji. Ni mojawapo ya mabwawa makubwa zaidi ulimwenguni, limejazwa dhiraa meta 148,500,000 za ardhi. Boma la Farakka, kwenye Mto Ganga, huhifadhi maji ya kutosha kwa ajili ya kuongezeka kwa usafiri wa meli karibu na Bandari ya Calcutta.
Sawa na mito mingine, uchafuzi ni tatizo kubwa kwenye Mto Ganga. Hivyo, mnamo 1984 Mpango madhubuti wa Kuhifadhi Mto Ganga ulianzishwa na serikali ya India. Ulikazia kufanyiza mbolea au biogesi kutokana na maji machafu, kuzuia maji machafu yanayoingia mtoni, na kutengeneza viwanda vya kuondoa uchafu wa kemikali.
Hata hivyo, yaonekana kwamba mashirika ya wanadamu hayana uwezo wa kuirejesha mito iliyo duniani kwenye hali yake ya awali maridadi na safi. Lakini Mungu atatatua tatizo hilo hivi karibuni. Chini ya utawala wa Ufalme wake, ‘mito itapiga makofi’ dunia yote iwapo paradiso.—Zaburi 98:8.
[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 16, 17]
Mto Indus Wenye Nguvu
Kumekuwa na ubishi kuhusu chanzo cha Mto Indus kwa sababu vijito vingi huungana na kufanyiza mto huo. Lakini hapana shaka kwamba mto huo mkubwa huanzia kwenye milima ya Himalaya. Hutiririka kuelekea upande wa kaskazini-magharibi na kuungana na vijito vingine njiani, na kusonga kwa umbali wa kilometa 320 kupitia uwanda wa juu wa Tibet, “kilele cha ulimwengu.” Mto huo ukaribiapo mpaka wa India katika jimbo la Ladakh, hujipinda-pinda milimani, na kupenya majabali na hufanyiza mfereji kati ya safu ya milima ya Himalaya na Karakoram. Kisha huingia nchini India na kuporomoka kwa kina cha meta 3,700 hivi kwa umbali wa kilometa 560. Huporomoka na kuelekea kaskazini halafu hupiga kona kali kwenye pembe ya magharibi ya Himalaya, ambapo huungana na Gilgit, mto mkubwa utokao Hindu Kush. Halafu mto huo hutiririka kusini hadi Pakistan. Mto Indus hupenya katikati ya milima, ukijipinda-pinda na kusonga kwa nguvu nyingi hadi uwandani na kutiririka kupitia Punjab. Jina hilo lamaanisha “Mito Mitano,” mito mikubwa inayojiunga nao—Beas, Sutlej, Ravi, Jhelum, na Chenab—hutiririka kama vidole vilivyosambaa vya mkono mkubwa na kuingia kwenye Mto Indus kisha husonga taratibu hadi mwisho kwa umbali wa zaidi ya kilometa 2,900.
Mto Ganga Unaoheshimiwa Sana
Mto Ganga wenye urefu wa zaidi ya kilometa 2,500 huanzia upande wa kusini wa chanzo cha Mto Indus umbali wa kilometa 100 hivi kwenye milima ya Himalaya, nao hutiririka hadi kwenye Ghuba ya Bengal. Kwenye mwinuko wa zaidi ya meta 3,870, chemchemi ya kijito kinachoitwa Bhagirathi hububujika kutoka kwenye kilima cha barafu kinachoshabihi kinywa cha ng’ombe, ambacho huitwa kwa Kihindi Gaumukh. Huungana na kijito kingine kiitwacho Alaknanda, huko Devaprayag zapata kilometa 214 hivi kutoka kwenye chanzo chake. Vijito hivyo viwili pamoja na Mandakini, Dhauliganga, na Pindar hufanyiza Mto Ganga.
Mto Ganga uelekeapo kusini-mashariki na kuvuka bara hilo, huungana na mito mingine mikubwa kama vile Yamuna katika Allahabad huko India kisha Brahmaputra wenye nguvu huko Bangladesh. Huku ukiwa umesambaa kama feni, Mto Ganga na mito midogo inayoingia ndani yake hueneza maji kwenye robo ya eneo lote la India, katika uwanda wenye rutuba wa Ganga. Mfumo huo wa mito hukusanya maji kutoka kwenye eneo la kilometa 1,035,000 za mraba na hutegemeza theluthi ya watu wote India, ambao idadi hiyo sasa inapita bilioni moja, katika mojawapo ya maeneo yaliyosongamana zaidi ulimwenguni. Hupanuka sana ufikapo Bangladesh, mfano wa bahari iliyo barani, huwa na vyombo vya usafiri wa majini vya kila namna. Kisha Mto Ganga hugawanyika na kutokeza mito kadhaa muhimu na vijito vingi na kuwa mojawapo ya delta kubwa zaidi ulimwenguni.
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Tibet
PAKISTAN
Indus
Jhelum
Chenab
Sutlej
Harappa
Mohenjo-Daro
INDIA
Ganga
Yamuna
Brahmaputra
Allahabad
Varanasi
Patna
Calcutta
BANGLADESH
NEPAL
BHUTAN
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha]
Wahindu waogelea katika Mto Ganga
[Hisani]
Copyright Sean Sprague/Panos Pictures