Je, Twapaswa Kuonyesha Kihoro?
Je, Twapaswa Kuonyesha Kihoro?
KATIKA kitabu chake On Children and Death, Dakt. Elisabeth Kübler-Ross asema: “Watu wazima wengi sana huteseka kwa sababu hawakuwahi kutatua mafadhaiko waliyopata utotoni. Kwa hiyo watoto wapaswa kuruhusiwa kuonyesha kihoro bila kuitwa mliaji au kusikia usemi wenye dhihaka ‘Wavulana wakubwa hawalii.’”
Maoni hayo hutofautiana na falsafa katika nchi fulani ya kwamba mtu hapaswi kuonyesha hisia yoyote.
Simulizi la Mwelekezi wa Maziko
Tofauti hiyo yaelezwa na Robert Gallagher, mwelekezi wa maziko wa New York aliyehojiwa na Amkeni! Aliulizwa ikiwa aliona tofauti yoyote kuhusu namna wazaliwa wa Marekani na watu waliohamia Marekani kutoka nchi za Latini wanavyoonyesha kihoro.
“Bila shaka nimeona. Nilipoanza kazi hii miaka ya 1950, eneo letu lilikuwa na familia nyingi za wahamiaji kutoka Italia. Walikuwa na hisia-moyo nyingi sana. Sasa tunashughulika na watoto na wajukuu wao kwenye maziko, na hawana hisia-moyo nyingi sana. Hawaonyeshi hisia-moyo sana.”
Katika nyakati za Biblia Waebrania walionyesha kihoro na hisia-moyo zao. Ona jinsi Biblia inavyosimulia namna Yakobo alivyoitikia aliposadikishwa kwamba mwana wake Yosefu alikuwa amenyafuliwa na mnyama mkali: “Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake akamlilia.” (Mwanzo 37:34, 35; italiki ni zetu.) Naam, Yakobo hakuaibika kumlilia mwanawe aliyepotea.
Utamaduni Tofauti, Itikio Tofauti
Bila shaka, tamaduni hutofautiana. Kwa mfano, katika sehemu nyingi za Nigeria, ijapokuwa familia huwa na watoto wengi na kifo hutukia mara nyingi kwa sababu ya magonjwa mbalimbali, “kunakuwa na kihoro kingi sana mtoto afapo, hasa anapokuwa ni kifungua-mimba na hata zaidi ikiwa ni mvulana,”
akasema mwandishi aliyeishi Afrika kwa miaka 20. “Tofauti ni kwamba katika Nigeria kihoro huwa kingi tena cha muda mfupi. Hakiendelei kwa miezi na miaka mingi.”Katika Mediterania au nchi za Amerika ya Latini, watu wamelelewa katika mazingira ambamo maitikio ya asili huonwa kuwa ya kawaida. Huko, shangwe na huzuni huonyeshwa hadharani. Watu hawasalimiani kwa mikono tu; hukumbatiana kwa uchangamfu. Hali kadhalika, kwa kawaida kihoro huonyeshwa waziwazi kwa machozi na maombolezo.
Mwandishi Katherine Fair Donnelly, asema kwamba baba aliyefiwa “huvumilia si maumivu ya akilini tu ya kumpoteza mtoto wake lakini pia huhofu kupoteza sifa zake za kiume kwa kuonyesha kihoro hadharani.” Hata hivyo, asema kwamba “hasara ya kumpoteza mtoto ni kubwa kuliko sheria zinazohusu kuonyesha hisia-moyo. Hisia-moyo inayotoka ndani kabisa inayomfanya mtu atoe machozi mengi ya kihoro yafanana na kutoboa kidonda ili kuondoa ambukizo.”
Kwa hiyo ni jambo la kawaida kuonyesha kihoro katika nchi fulani kuliko ilivyo katika nyingine. Lakini kuonyesha kihoro na kutoa machozi hakupasi kuonwa kuwa ishara ya udhaifu. Hata Yesu Kristo ‘alitokwa na machozi’ kwa sababu ya kifo cha rafiki yake Lazaro, japo Yesu alijua angemfufua muda mfupi baada ya hapo.—Yohana 11:35.
[Blabu katika ukurasa wa 14]
Yakobo hakuaibika kumlilia mwanawe aliyepotea