Kuathiriwa na Kemikali Mbalimbali—Ugonjwa Usioeleweka
Kuathiriwa na Kemikali Mbalimbali—Ugonjwa Usioeleweka
Nyumba ya Pam ilikuwa katika eneo la makao lililozungukwa na mashamba ya pamba. Kwa kawaida ndege ziliyanyunyizia mashamba dawa za kuzuia magugu au kuwaua wadudu; na mara nyingi upepo uliyapeperusha mabaki ya kemikali hizo hadi nyumba zilizokuwa karibu, kutia ndani nyumba ya Pam.
PAM alianza kuhisi maumivu makali ya kichwa na kichefuchefu, na afya yake ikaharibika. Hatimaye, aliathiriwa na vitu visivyokuwa na uhusiano wowote na dawa za mimea: marashi, viondoa-harufu, mafuta ya kujipaka, sabuni, rangi, zulia jipya, moshi wa tumbaku, viondoa-harufu za hewa, na vinginevyo. Dalili za Pam ni dalili za hali mbaya ya afya isiyoeleweka vizuri iitwayo katika lugha ya Kiingereza, multiple chemical sensitivity (MCS), yaani hali ya kuathiriwa na kemikali mbalimbali. *
“Ninapokuwa katika mazingira yenye kemikali za kawaida, naanza kuhisi kwamba nimechoka sana au hata mwenye kuchanganyikiwa mawazo, mwenye kizunguzungu au kichefuchefu,” Pam alimweleza mwandishi wa Amkeni! “Mwili wangu huvimba, na mara kwa mara naanza kuhema, au napatwa na hofu ya ghafula pamoja na kulia kusikoweza kudhibitiwa, moyo wangu hupigapiga, au napatwa na ongezeko la kipigo cha mshipa wa damu, au majimaji yakusanyika mapafuni mwangu. Hali hiyo imesababisha hata nimonia.”
Ingawa dalili za MCS hutofautiana katika watu mbalimbali, baadhi ya dalili za tatizo hilo ni maumivu ya kichwa, uchovu, maumivu ya misuli au viungo, ukurutu, vipele, dalili za homa ya mafua, ugonjwa wa pumu, mchochota wa uwazi wa mfupa wa fuvu, wasiwasi, kushuka moyo, tatizo la kumbukumbu, kutoweza kukaza fikira, kupoteza usingizi, pigo lisilo la kawaida la moyo, kuvimba, kichefuchefu, kutapika, matatizo ya matumbo, au mtukutiko wa maungo. Bila shaka magonjwa mengine pia yaweza kusababisha dalili kama hizo.
MCS—Tatizo Linaloongezeka
Uchunguzi uliofanywa miongoni mwa jamii mbalimbali ya watu huko Marekani, waonyesha kwamba asilimia 15 hadi 37 ya watu wanajiona kuwa wenye kuathiriwa au wenye mzio wa kemikali za kawaida au harufu zake, kama vile moshi wa magari au wa tumbaku, rangi iliyopakwa juzi, zulia
jipya, au marashi. Hata hivyo, asilimia 5 tu au wachache zaidi, ikitegemea umri wa wale waliohojiwa, walisema kwamba wamepimwa na kupatikana kuwa na tatizo la MCS. Robo tatu ya hao walikuwa wanawake.Wengi walio na tatizo la MCS wanasema kwamba dawa za kuua wadudu au viyeyushi vilisababisha hali yao. Kemikali hizo mbili zimo katika mazingira yetu kwa wingi, hasa viyeyushi. Viyeyushi ni vivukivu (huvukiza kwa urahisi sana) navyo hutawanyisha na kuyeyusha vitu vingine. Viyeyushi hutumiwa kwa kutengeneza rangi, vanishi, gundi, dawa za kuua wadudu, sabuni za maji.
Katika makala yafuatayo, tutachunguza tatizo la MCS kwa kindani zaidi, tutazungumzia msaada unaopatikana kwa wale walio na tatizo hilo na kuona jinsi walio na tatizo hilo na wale wasio na tatizo hilo wanavyoweza kushirikiana kufanya maisha yawe yenye kufurahisha zaidi kwa wale wenye MCS.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Katika makala haya tumetumia jina “multiple chemical sensitivity” kwa sababu jina hilo lajulikana sana. Hata hivyo, kuna majina mengine mengi, kama vile “ugonjwa unaosababishwa na mazingira” au “dalili ya ugonjwa wa kuathiriwa sana na kemikali.” “Kuathiriwa” huku kwamaanisha kuathiriwa na kiasi kidogo cha kemikali kisichowaathiri watu walio wengi.