Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mua—Mmea mkubwa Katika Jamii ya Nyasi

Mua—Mmea mkubwa Katika Jamii ya Nyasi

Mua—Mmea mkubwa Katika Jamii ya Nyasi

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

TUNGEFANYA nini pasipo sukari? Ingekuwa kutilia chumvi kusema kwamba ulimwengu ungekwama—lakini milo mingi ingelihitaji kubadilishwa kabisa endapo sukari ingelikosekana. Naam, leo katika sehemu nyingi ulimwenguni, utumiaji wa sukari umekuwa jambo la kawaida, na hilo limefanya uzalishaji wa sukari uwe biashara ya ulimwenguni pote.

Mamilioni ya watu, kutoka Kuba hadi India na kutoka Brazili hadi Afrika, hukuza na kuvuna miwa. Hata, wakati mmoja uzalishaji wa sukari ulikuwa biashara kubwa zaidi na yenye faida sana ulimwenguni. Twaweza kusema kwamba ni mimea michache sana ambayo imebadili ulimwengu kama mua.

Je, ungependa kujifunza mengi kuhusu mmea huu wa pekee? Basi jiunge nasi tuzurupo jimbo moja katika Queensland, Australia, ambako miwa hukuzwa. Ijapokuwa eneo hili hukuza kiasi cha kadiri cha miwa, mbinu bora za kilimo na za uzalishaji zimelifanya liwe mojawapo ya maeneo yanayoongoza katika uuzaji wa sukari-guru ulimwenguni.

Kuzuru Nchi Inayokuza Miwa

Hewa ina mvuke wa joto kali. Jua kali mno la kitropiki laangazia shamba la miwa iliyokomaa. Mashine kubwa inayofanana na trekta kubwa ya kuvunia ngano inasonga taratibu kwenye miwa hiyo mirefu, inavuna kwa kufyeka vikonyo vya miwa na kuvitia kwenye trela inayokokotwa. Muda si muda maji ya sukari yanachiririka kutoka kwenye miwa hiyo iliyovunwa, na harufu tamu ya ukuvu yasambaa hewani. Maji hayo muhimu yatokayo kwa nyasi hizo za pekee ndipo tu yameanza kutayarishwa kutoka shambani hadi yanapokuwa sukari unayotumia nyumbani mwako.

Miaka michache iliyopita, miwa ilivunwa kwa miundu na ilikuwa kazi ngumu sana hapa Australia kama ilivyo katika nchi nyingi ambako miwa huvunwa. Hebu wazia inavyokuwa. Wafanyakazi wanakata miwa kwa miundu. Safu ya wakataji-miwa wanaotiririkwa na jasho wanasonga taratibu kwenye shamba hilo la miwa. Kwa usahihi mkubwa, wafanyakazi hao wanakusanya vishada vya miwa vilivyonyooka kwa mkono mmoja kisha wanaviinamisha upande mmoja ili mashina yake yaonekane. Miundu yashuka na kukata chapu chapu! Wafanyakazi hao wanyanyua na kushusha miundu kwa nguvu na kuvikatia vikonyo shinani. Wasonga mbele kwenye kishada cha miwa kifuatacho, huku wakiirusha miwa kandokando kwa safu laini. Hali hiyo inabadilika hatua kwa hatua ulimwenguni pote, kwa kuwa nchi nyingi zaidi zinaanza kuvuna kwa mashine.

Huko Australia miwa hupandwa hasa kwenye mwambao wa pwani wenye umbali wa kilometa 2,100, ambao kwa sehemu kubwa unapakana na lile Tumbawe Kuu lililo mashuhuri. (Ona makala “A Visit to the Great Barrier Reef,” katika toleo la Amkeni! la Juni 8, 1991, Kiingereza.) Eneo hilo huwa na tabia-nchi ya hewa yenye mvuke wenye joto mwaka mzima, hali ambayo inafanya miwa isitawi, na wakulima wapatao 6,500 humiliki mashamba madogo ya familia ambayo yamesambaa katika pwani kama vichala vya zabibu kwenye mzabibu.

Baada ya kusafiri kwa muda mrefu, twaona kwa mbali jiji lililo mashuhuri kwa uzalishaji wa sukari la Bundaberg, katika pwani ya kati ya Queensland. Tuteremkapo kilima twaona mandhari yenye kuvutia sana—miwa mingi kupindukia ikitikiswa na upepo! Twaona rangi nyingi kama nini! Mashamba mbalimbali ya miwa yamefikia hatua mbalimbali za ukomavu, kwa hiyo yanafanyiza mandhari inayoshabihi viraka vya rangi mbalimbali za kijani kibichi na dhahabu vilivyopangwa taratibu, huku maeneo yasiyolimwa mwaka huu au yaliyofyekwa karibuni yakiwa na rangi ya kahawia.

Julai ni mwezi wenye baridi kuliko yote, na msimu wa kuvuna na kusindika umeanza punde. Utaendelea hadi Desemba kadiri miwa inavyokomaa. Sasa tuna hamu ya kuzuru kiwanda cha sukari ili tuone kinachotukia kwa miwa iliyovunwa. Lakini inapendekezwa kwamba kabla ya kwenda huko tujifunze mambo fulani kuhusu miwa. Kwa hiyo twaamua kuanza kwenye kituo cha utafiti wa sukari kilichojengwa katika eneo hilo. Wanasayansi hutumia kituo hicho kukuza aina mpya ya miwa na kufanya utafiti wa kuboresha kilimo na ukuzaji wa miwa.

Chanzo Chake na Ukuzaji

Katika kituo cha utafiti wa sukari, mtaalamu mmoja wa kilimo mwenye shauku afurahi kutufundisha habari fulani kuhusu miwa na namna inavyokuzwa. Mua ambao ulianza katika misitu ya mvua ya Kusini-mashariki ya Asia na New Guinea ni mmea mkubwa katika jamii ya nyasi, inayotia ndani nyasi mbalimbali kama vile nyasi laini ya bustani, nafaka, na vichaka vya mianzi. Mimea hiyo yote hutengeneza sukari katika majani yake kwa utaratibu unaoitwa usanidi-nuru. Lakini miwa ni tofauti sana kwa sababu hutengeneza sukari nyingi sana kisha huhifadhi maji hayo matamu ya sukari katika vikonyo vyake vyenye nyuzinyuzi.

Ukuzaji wa miwa ulienea sana katika India ya kale. Waandishi katika jeshi la Aleksanda Mkuu lililoshambulia India mwaka wa 327 K.W.K., waliona wakazi wa huko “wakitafuna tete za ajabu, zilizotokeza aina fulani ya asali bila kusaidiwa na nyuki.” Ukuzaji wa miwa ulienea kasi katika karne ya 15, wakati uvumbuzi na ufanisi wa ulimwengu ulipopamba moto. Leo kuna maelfu ya jamii za miwa, na zaidi ya nchi 80 huchangia takriban tani bilioni moja za miwa zinazovunwa kila mwaka.

Katika nchi nyingi ulimwenguni, upandaji wa miwa ni kazi ngumu sana. Vikonyo vikomavu vya miwa hukatwa kwa vitawi vyenye urefu wa meta 0.4 hivi na kupandwa katika mitaro iliyoachana kwa meta 1.5 hivi. Kila kitawi hutokeza kishada chenye vikonyo 8 hadi 12 hivi vya miwa, ambavyo hukomaa kwa muda wa kati ya miezi 12 hadi 16. Kutembea katikati ya vichaka vya miwa mikomavu kwaweza kutisha sana. Vikonyo vya miwa na majani mengi hukua kufikia kimo cha meta 4 hivi. Je, ni upepo tu unaosababisha mchakacho wa majani tusikiao, au labda ni nyoka au mnyama-mgugunaji? Kama tahadhari, huenda ikawa vyema kwetu kuelekea kwenye uwanja ulio wazi na salama!

Utafiti wa kutafuta mbinu za kukomesha wadudu na magonjwa yanayoshambulia miwa ungali unafanywa. Umefanikiwa kwa kadiri fulani, ijapokuwa si kabisa. Kwa mfano, mnamo 1935, wenye mamlaka walileta vyura wa miwa wa Hawaii kaskazini mwa Queensland, ili wakomeshe kabisa mbawakavu msumbufu wa miwa. Jambo la kusikitisha ni kwamba vyura hao wa miwa waliamua kula vyakula vingine mbalimbali badala ya mbawakavu wa miwa, sasa vyura hao waliozaa kwa wingi wamekuwa wanyama-wasumbufu kotekote kaskazini-mashariki mwa Australia.

Unateketeza Kabla ya Kuvuna?

Baadaye, giza likisha ingia, twatazama kwa mshangao wakati mkulima mmoja anapochoma moto shamba lake lenye miwa mikomavu. Baada ya sekunde chache moto mkubwa wateketeza shamba hilo dogo huku miali yake ikipaa juu katika anga la usiku. Kuteketeza shamba la miwa huondoa majani yasiyotakikana na vitu vingine vinavyoweza kuvuruga uvunaji na usindikaji. Lakini siku hizi, mtindo unaozidi kupendwa na wengi ni kuvuna bila kuteketeza kwanza mashamba kwa moto mkubwa. Uvunaji huo huitwa uvunaji wa miwa ya kijani-kibichi. Mbali na kuboresha uzalishaji wa sukari, njia hiyo huacha majani yanayohifadhi unyevu ardhini, na kuzuia pia magugu na mmomonyoko wa udongo.

Ijapokuwa nchi nyingi zinazokuza miwa leo bado huvuna zao hilo kwa miundu, sasa nchi nyingi zaidi zinavuna kwa mashine kubwa za kuvunia miwa. Trekta hizo kubwa kupindukia hupitia kwenye miwa mirefu, zikikata ncha zake na kuondoa matawi yasiyotakikana kisha huikata kwa vipande vifupi, tayari kwa usindikaji kiwandani. Mvunaji mmoja wa miwa aweza kuvuna kwa wastani tani tano za miwa kila siku kwa kutumia mikono yake, lakini mashine za kuvunia miwa zaweza kuvuna kwa urahisi tani 300 hivi kwa siku. Mashamba ya miwa yaweza kuvunwa kwa miaka kadhaa kabla ya kupungua kwa mavuno halafu miwa mingine hupandwa na ya kale kung’olewa.

Baada ya miwa kuvunwa, ni lazima ishughulikiwe haraka iwezekanavyo, kwa kuwa sukari iliyo katika miwa iliyovunwa huharibika upesi. Ili kurahisisha usafirishaji wa miwa hadi kiwandani, reli nyembamba za tramu hufikia umbali wa kilometa zipatazo 4,100 katika maeneo ya Queensland yanayokuza miwa. Magari moshi hayo madogo yanayotumia reli hizo huvutia sana yanapopitia mashambani, yakikokota mabehewa mengi yaliyojaa miwa pomoni.

Kuzuru Kiwanda cha Sukari

Kuzuru kiwanda cha sukari ni jambo la kuvutia sana. Kwanza waona mlolongo wa mabehewa yenye miwa yakisubiri kupakuliwa. Mashine kubwa za kuponda na micheduara huponda-ponda miwa hiyo, na maji ya sukari huchiririka kutoka kwenye nyuzinyuzi zake. Machicha yabakiyo, hukaushwa na kutumiwa kama fueli ya kuendesha kiwanda chote. Watengenezaji wa karatasi na vifaa vya ujenzi hununua machicha yanayosalia ili wayatumie kutengenezea bidhaa zao.

Uchafu ulio katika maji ya sukari huondolewa, na maji safi ya sukari husalia. Uchafu huo ulioondolewa hutumiwa kutengenezea mbolea. Zaotuka jingine, molasi hutumiwa kama mlo wa mifugo au katika usafishaji wa pombe kali na ethanoli inayotumiwa viwandani. Kwa kweli matumizi mbalimbali ya miwa na utaratibu rahisi wa kuisindika huvutia ajabu.

Maji hayo ya sukari hufanywa mazito kwa kuchemsha ili kuondoa maji ya ziada, kisha hugandishwa kwa fuwele ndogo za sukari. Fuwele hizo hukua hadi zifikiapo ukubwa unaotakikana. Kisha huchujwa na kukaushwa. Hufanyiza sukari-guru isiyosafishwa. Sukari-guru hiyo husafishwa zaidi na kuwa sukari nyeupe ya kawaida inayotumiwa na wengi mezani.

Yamkini chai au kahawa yako itakuwa na ladha tamu zaidi baada ya ziara hii yenye kuvutia na kuelimisha katika nchi inayokuza miwa. Endapo una ugonjwa wa sukari, basi huna budi kutotumia sukari na labda kutumia kibadala.

Kwa kweli, tumevutiwa na uwezo mbalimbali na ujuzi wa Yule aliyebuni na kutokeza mmea huo maridhawa wenye kustaajabisha, mua—kwa kweli ni mmea mkubwa katika jamii ya nyasi!

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Je, Ni Kiazisukari au Ni Mua?

Sukari hutengenezwa kutokana na mimea miwili muhimu ulimwenguni. Miwa hukuzwa hasa katika maeneo ya kitropiki na hutokeza angalau asilimia 65 ya sukari ulimwenguni pote. Asilimia 35 inayosalia hutokana na viazisukari vinavyokuzwa katika maeneo yenye baridi, kama vile Ulaya Mashariki na Magharibi na Amerika Kaskazini. Sukari hizo zina kemikali zilezile.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mashine ya kuvunia miwa. Trekta yakokota trela

[Picha katika ukurasa wa 23]

Miwa yateketezwa kabla ya kuvunwa

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

Picha zote kwenye ukurasa wa 21-24: Queensland Sugar Corporation