Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Nchi Inayotumia Tumbaku Zaidi Ulimwenguni
China ndiyo “nchi inayozalisha na kutumia tumbaku zaidi ulimwenguni,” laripoti The Journal of the American Medical Association. “Kati ya Wachina bilioni 1.2, zaidi ya wanaume milioni 300 na wanawake milioni 20 ni wavutaji-sigareti.” Madaktari kutoka Taasisi ya China ya Dawa za Kuzuia Magonjwa na Shirika la China la Uvutaji-Sigareti na Afya, huko Beijing, pamoja na madaktari wa nchi za Magharibi wamechapisha matokeo ya uchunguzi wa nchi nzima wa watu zaidi ya 120,000 waliohojiwa. Walifikia mkataa gani? China inakabiliana na “ongezeko la mapema la ghafula la tumbaku,” na “angalau Wachina milioni 50 wanaovuta sigareti leo wanatarajiwa kufa mapema.” Wastani wa umri wa watu wanaoanza kuvuta sigareti katika China umepungua kwa miaka mitatu hivi tangu 1984, kutoka watu wenye umri wa miaka 28 hadi 25, yasema ripoti hiyo. Ni wachache tu waliotambua kwamba uvutaji-sigareti waweza kusababisha kansa ya mapafu na maradhi ya moyo.
Wazazi Wanapojali
“Sasa wanasayansi wanasema kwamba siri ya kufanikiwa kwa mtoto ni kuwa na mzazi anayejali masomo yake—na anayeonyesha hivyo,” lasema gazeti The Toronto Star. Tangu 1994 mashirika ya Takwimu ya Kanada na Uboreshaji wa Rasilimali za Kibinadamu yamefuatia kwa pamoja maendeleo na afya ya watoto Wakanada 23,000 wenye umri wa kati ya miaka 4 hadi 11. Yaonekana, wazazi wengi Wakanada hupendezwa kikweli na elimu ya watoto wao, hasa wanapokuwa katika madarasa ya kwanza-kwanza. Ripoti hiyo yasema kwamba “asilimia 95 ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 10 na 11 husema kwamba wazazi wao huwatia moyo wafanye vizuri shuleni karibu wakati wote” na kwamba asilimia 87 ya wazazi “husoma na watoto wao kila siku wanapokuwa Darasa la 1 hadi la 3.” Mary Gordon, msimamizi wa programu za wazazi za Baraza la Shule la Toronto, asema: “Sasa twajua kwamba si lazima uwe tajiri au umeelimika ili kuwa mzazi mzuri bali wapaswa kuwepo, kuwa macho na kuonyesha upendezi.” Aongezea hivi: “Uhusiano wa kielimu ndio hukuza ubongo, nao hutukia kwanza nyumbani.”
Vijana na Simu
Vijana wanajulikana sana kwa kuzungumza kwa simu. “Wao huchukua simu ili kujifurahisha au wakati wanapochoka,” lasema gazeti la Poland la kila juma Przy-jaciółka. Hata hivyo, huenda wengi wasitambue muda wanaotumia kwenye simu au gharama ya kupiga simu. Suluhisho ni gani? Gazeti hilo lapendekeza kwamba vijana waombwe kulipia angalau kiasi fulani cha bili ya simu. Linapendekeza vijana wakumbushwe kwamba “watu wengine wangependa kutumia simu pindi fulani-fulani.”
Mbawakavu Ambaye Hurusha Risasi
“Picha zinazopigwa kwa kasi sana zimewawezesha wanasayansi kuelewa mbinu ambayo hufanya mbawakavu aina ya bombardier kuwa mlenga-shabaha asiyekosea na aliye na silaha yenye matokeo zaidi miongoni mwa wadudu,” laripoti gazeti Independent la London. Akitumia jozi inayofanana na ngao ya kuelekeza maji upande mwingine kwenye ncha ya fumbatio lake, mbawakavu huyo aweza kumrushia adui asidi moto bila kukosea na kuipoesha kwa muda unaopungua sekunde moja. Kwa kuwa mbawakavu huyo haathiriwi na umajimaji huo, aweza pia kujilinda kwa kujirushia asidi hiyo kwenye sehemu hususa za mwili wake mwenyewe, kutia ndani mgongo wake, anaposhambuliwa na kundi kubwa la wadudu, kama vile chungu. Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Cornell, huko Ithaca, New York, waliompiga picha mbawakavu huyo akirusha asidi, wasema: “Ijapokuwa ilijulikana kwamba mbawakavu aina ya bombardier wanaweza kulenga manyunyu yao kwa kuzungusha ncha ya fumbatio lao, haikuwa imejulikana jinsi wanavyolenga shabaha yao kwa usahihi.”
Hasira Kali Jikoni
“Kuongezeka kwa vifaa vya nyumbani vya hali ya juu kunachochea ‘hasira kali jikoni,’” laripoti gazeti Independent la London. Wenye nyumba waliofadhaika “hugundua kwamba hawawezi kupasha joto kikombe cha supu kwenye wimbi-mikro, kufua soksi au kutumia mashine ya kusaga matunda na kukoroga unga bila kutumia saa nyingi wakisoma kwa makini kitabu cha maagizo.” Wanasaikolojia wanasema kwamba tekinolojia ya kisasa huruhusu watengenezaji kuwa na mashine yenye vitu chungu nzima, na wanataja mashine ya kawaida ya vidio kuwa mfano
mmoja wa kifaa kinachotatanisha zaidi. Cary Cooper, profesa wa saikolojia kwenye Chuo Kikuu cha Manchester, aeleza hivi: “Watu hukabiliana na tekinolojia mpya mahali pao pa kazi, na wanapofika nyumbani wanataka maisha sahili ambayo hayatawakumbusha kazi.”Hatari ya Miche Inayochipuka
Baada ya kuongezeka kwa visa vya magonjwa yanayosababishwa na chakula, Shirika la Marekani la Usimamizi wa Chakula na Dawa limewashauri wanunuzi kwamba mtu yeyote anayetaka kupunguza hatari za ugonjwa unaosababishwa na chakula apaswa kuepuka kula miche inayochipuka ambayo haijapikwa, laripoti gazeti FDA Consumer. Watu wengi hufurahia kula alfalfa, klova, au miche ya maharagwe isiyopikwa. Hata hivyo, katika nchi kadhaa mimea hiyo imehusianishwa na maambukizo ya bakteria, lasema The New York Times. Watoto wadogo, wazee-wazee, na wale ambao mfumo wao wa kinga ni dhaifu ndio wanaoweza kuathiriwa hasa. Watafiti walijaribu njia mbalimbali za kuzuia bakteria hizo, kutia ndani kuosha miche kwa klorini au kwa alkoholi, lakini hakuna yoyote ambayo imefaulu kabisa. Walieleza kwamba “unyevu na halijoto ya kiwango cha juu wakati wa kuchipuka hufaa kwa ajili ya ukuzi wa viumbe hao,” lasema Times.
Lugha za London
Watoto wa shule huko London, Uingereza, huzungumza angalau lugha 307, laripoti gazeti la jiji hilo The Times. Dakt. Philip Baker, mmojawapo wa waandishi wa kwanza wa uchunguzi wa lugha zinazozungumzwa sasa katika London, alishangazwa na jinsi zinavyotofautiana. Alisema: “Sasa tuna hakika kwamba London ndilo jiji lenye lugha nyingi zaidi ulimwenguni, hata kushinda New York.” Idadi hiyo ya 307 haitii ndani mamia ya lahaja na hata huenda ikawa ni ya chini. Ni thuluthi mbili tu za watoto wa shule 850,000 ambao huzungumza Kiingereza nyumbani. Kikundi kikubwa zaidi cha wanaosema lugha za kigeni hutoka bara Hindi. Angalau lugha 100 za Kiafrika huzungumzwa. Katika shule moja tu, wanafunzi huzungumza lugha 58.
Kushambuliwa na Kuvu!
Ugonjwa wa choa ya miguu, ambao husababishwa na ambukizo kali la kuvu kwenye vidole na wayo wa miguu, unashamiri haraka huko Ujerumani, laripoti gazeti Der Spiegel. Mjerumani mmoja kati ya 5 ana ugonjwa huo, na katika nchi nyingine za Ulaya, umeenea kwa kiwango kikubwa hata zaidi. Ni rahisi sana kuambukizwa mahali ambapo watu hutembea miguu mitupu katika eneo lililozingirwa—kama vile kwenye bafu za mvuke, vidimbwi vya kuogelea, au hata kwenye majengo fulani ya kidini. Kwa kuwa vijimbegu vya kuvu ni sugu sana, mashine za kupulizia dawa ya kuua viini kwenye miguu au beseni—mara nyingi husambaza zaidi ugonjwa wa choa ya miguu badala ya kuuzuia. Unaweza kulindaje miguu yako? Mtaalamu wa kuvu Dakt. Hans-Jürgen Tietz apendekeza kutumia sapatu katika sehemu zote ambazo watu hukanyaga. Jambo muhimu zaidi ni kukausha miguu yako. Kuikausha kikamili, hasa katikati ya vidole, huzuia kuvu isisitawi na kuongezeka.
Kuondoa Chumvi Kwenye Maji ya Bahari
Maji ya bahari yanageuzwa kuwa maji ya kunywa kwenye kiwanda kimoja cha kuondoa chumvi katika kisiwa kidogo kilicho karibu na pwani ya Australia Kusini, laripoti gazeti The Australian. Ingawa kuondoa chumvi si jambo jipya, “tekinolojia hiyo imesifiwa kuwa hatua ya maendeleo katika kuondoa chumvi kwa sababu haihitaji kemikali zozote,” yasema ripoti hiyo. Ili kuwapa maji wakazi 400 wa Penneshaw, katika Kisiwa cha Kangaroo, “maji hutolewa baharini na kupitishwa ndani ya mpira wenye kanieneo kubwa ili kuondoa chumvi. Kisha maji yaliyosalia yenye chumvi nyingi, hurudishwa baharini.” Ingawa kuna matumaini makubwa ya kutumiwa sana kwa mfumo huo, bado ni ghali, ijapokuwa ni wa gharama ya chini kuliko njia za kawaida za kusafishia maji, lasema The Australian.
“Yumo Mkutanoni”
Katika uchunguzi uliohusisha makarani 148 wanaofanyia kazi wakubwa au makampuni makubwa, asilimia 47 walisema kwamba wakubwa wao walikuwa wamewaomba wawadanganye watu pindi kwa pindi, laripoti The Wall Street Journal. Karani mmoja, msaidizi katika idara ya uuzaji huko Texas, alisema kwamba ili adumishe kazi yake kwa muda wa miaka 30, amehitaji kuwaambia watu wanaopiga simu kwamba mkubwa wake alikuwa “mkutanoni,” hata wakati ambapo alikuwa peke yake ofisini. Uwongo fulani waweza kusababisha jeuri hasa, kama vile kumwambia mke kwamba hujui mahali alipo mumewe. Karani mmoja alipigwa kalamu baada ya kumwambia ukweli mtu mmoja aliyepiga simu kwamba cheki iliyochelewa haikuwa imetumwa.