Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Habari za Karibuni Kuhusu Njaa Ulimwenguni
“Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lakadiria kwamba takriban nusu ya watu katika mataifa yote—matajiri na maskini—hupatwa na utapiamlo wa aina moja au nyingine,” laripoti State of the World 2000. Inakadiriwa kwamba watu bilioni 1.2 ulimwenguni pote wanaathiriwa na ukosefu wa chakula cha kutosha au kinachofaa. Zaidi ya hayo, mabilioni kadhaa wanasemekana kuwa wanateseka kutokana na ‘njaa isiyoonekana,’ inayorejezea wale wanaoonekana kuwa wamelishwa vyakutosha lakini wamedhoofika kwa kukosa vitamini na madini muhimu. “Leo dhana isiyo ya kweli ni kwamba njaa husababishwa na upungufu wa chakula,” lasema shirika la Worldwatch Institute, ambalo hutayarisha ripoti ya kila mwaka ya State of the World. “Ukweli ni kwamba wanadamu ndio husababisha njaa . . . Kama watu watapata chakula cha kutosha au la hakutegemei kiasi halisi cha chakula kilicho nchini bali kwategemea hadhi wanayopewa wanawake, na kama serikali zinawajibika kwa raia zao.”
Visa vya Kujiua Nchini Ufaransa
“Asilimia 30 ya watu wazima huko Ufaransa wamefikiria kujiua,” laripoti gazeti Le Monde. Kati ya wale waliohojiwa katika uchunguzi huo wa kwanza uliopata kufanywa kuhusu visa vya kujiua katika Ufaransa, asilimia 13 walisema kwamba walikuwa wamefikiria kwa uzito kujiua na wengine asilimia 17 walikiri kwamba walifikiria kijuu-juu kufanya hivyo. Hata hivyo, kulingana na Michel Debout, profesa wa tiba inayoamriwa na mahakama kwenye hospitali ya chuo kikuu katika Saint-Étienne, idadi halisi ni kubwa zaidi, kwa sababu wengi huficha mawazo hayo kwa sababu ya kuhisi hatia. Idadi kubwa ya watu waliohojiwa huona kujiua kuwa “kitendo cha kukata tamaa” kinachosababishwa na matatizo ya jamii badala ya hali za familia. Kila mwaka, watu 160,000 hujaribu kujiua huko Ufaransa na takriban 12,000 hujiua.
Kuchagua Itikadi za Kidini Unazopenda
Uchunguzi uliofanywa na mtafuta-maoni George Gallup Jr., waonyesha kwamba watu wengi katika Marekani huona dini kuwa sawa na “kachumbari.” Badala ya kufuata “mifumo ya kale ya itikadi, Waamerika wa [Kaskazini] ‘huchagua kwa makini’ wanachotaka kuitikadi, mara nyingi wakichanganya mawazo mengi kutoka kwa dini moja au kuchanganya dini mbili au zaidi na kufanyiza mfumo wa itikadi wa kibinafsi,” laripoti gazeti la Kanada National Post. Uchunguzi huo pia waonyesha kwamba “kuna ukosefu dhahiri wa ujuzi kuhusu Biblia, mafundisho ya msingi na mapokeo ya dini ya mtu” na kwamba “mara nyingi watu wana imani ya kijuu-juu tu bila kujua wanachoamini au kwa nini,” lasema gazeti hilo. Reginald Bibby, profesa wa sosholojia katika Chuo Kikuu cha Lethbridge, Alberta, Kanada, asema hivi: “Watu wengi wanaendelea kufuata mapokeo yaliyoenea ya Katoliki na Protestanti, lakini wanachagua kwa makini itikadi, mazoea, na huduma za kitaalamu—kama vile ubatizo, arusi na maziko.”
Kahawa na Sumu
Kulingana na utafiti wa hivi majuzi, kahawa yaweza kuondoa kutoka kwenye maji ya mfereji “asilimia 78 hadi 90 ya metali nzito zilizoyeyuka, kama vile risasi na shaba, kwa sababu buni za kahawa, zenye molekuli zisizo na chaji au zilizo na chaji hasi, huvuta metali nzito zilizo na chaji chanya,” laripoti gazeti Australian. “Kadiri kahawa iwavyo na nguvu, ndivyo iondoavyo metali hizo vizuri zaidi,” akasema mwanakemia wa mazingira Dakt. Mike McLaughlin. Majaribio hayohayo yalifanywa kwa kutumia vifuko vya chai, lakini ingawa chai huondoa karibu thuluthi ya risasi, haikuwa na matokeo makubwa kwa shaba.
Je, Ni Halali Kujenga Sanamu ya Mtu ya Theluji Siku ya Sabato?
Kuanguka kwa theluji nyingi huko Israeli wakati wa majira ya baridi kali yaliyopita, kumezusha maswali tata kwa Wayahudi wa Kanisa la Othodoksi: Je, kurushiana vidonge vya theluji kunaruhusiwa siku ya Sabato? Vipi juu ya kutengeneza sanamu ya mtu ya theluji? Kulingana na shirika la habari la IsraelWire, aliyekuwa rabi mkuu wa Israeli Mordehai Eliyahu sasa ametokeza miongozo fulani kwa waamini wasio na hakika juu ya kinachoruhusiwa na kisichoruhusiwa. Rabi huyo alisema kwamba kutengeneza sanamu ya mtu ya theluji ni “kazi,” hata kama inafanywa kwa kujifurahisha
tu. Kwa hiyo kazi hiyo haipasi kufanywa siku ya Sabato. Kwa upande mwingine, kurushiana vidonge vya theluji hakuonwi kuwa kazi na hivyo kunaruhusiwa. Hata hivyo, kuna sharti moja. Lazima washiriki wote wakubali kupigana, bila kurushia wapita-njia vidonge vya theluji.Je, Ubongo wa Watu Wazima Hutokeza Chembe Mpya za Neva?
“Kwa miongo mingi, imedhaniwa kwamba watu walizaliwa na chembe zote za ubongo,” lasema The New York Times. Ijapokuwa huko nyuma mwaka 1965, majaribio yaliyofanywa kwa wanyama fulani yalionyesha kwamba ubongo wao ulikuwa ukitokeza chembe mpya za neva, wataalamu wengi wa neva waliamini kwamba haikuwa hivyo kwa wanadamu. Hata hivyo, katika mwongo uliopita, uthibitisho umeongezeka ambao unaonyesha kwamba ubongo hutokeza chembe mpya za neva na kwamba huenda unajifanya upya daima. Mwaka jana watafiti waligundua kwamba chembe mpya zilifanyizwa katika sehemu fulani ya ubongo wa binadamu inayohusiana na kumbukumbu la muda mfupi. Sasa wanasayansi fulani wanaamini kwamba “huenda ikawa ubongo unajifanya upya wakati wote.”
Mkazo Mkali Wahusianishwa na Kutendwa Vibaya Utotoni
“Wanawake ambao walitendwa vibaya kimwili au kingono wakati wa utotoni waweza kuteswa daima na itikio lenye kasoro kuelekea mkazo,” laripoti The Dallas Morning News. Watafiti katika Chuo Kikuu cha Emory huko Atlanta walilinganisha viwango vya homoni za mkazo na mipigo ya moyo ya wanawake waliotendwa vibaya hapo awali na vya wale ambao hawakutendwa vibaya, wanawake hao walipokuwa wakifanya kazi yenye mkazo. Wale ambao walikuwa wametendwa vibaya utotoni walikuwa na viwango vya juu vya homoni za mkazo na kuongezeka kwa mipigo ya moyo chini ya mkazo. Watafiti hao wanafikia mkataa kwamba “huenda kukawa na kasoro ya kikemia ya kudumu katika namna ambavyo miili yao huitikia na kudhibiti mkazo,” lasema gazeti hilo.
Mifuko Mizito Inayobebwa Mgongoni
Uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Marekani ya Madaktari-Wapasuaji wa Mifupa umeonyesha kwamba kuna uhusiano wa karibu kati ya maumivu ya mgongo na ya bega miongoni mwa watoto na mifuko mizito ambayo watoto fulani hubeba mgongoni. Baada ya kujaza vitabu vya shule, chakula na kinywaji, ala za muziki, na nguo safi za kubadilisha kwenye mifuko yao ya mgongoni, watoto fulani hubeba mizigo yenye uzito wa kilogramu 18. Madaktari wa magonjwa ya watoto wanatahadharisha kwamba huenda watoto wa shule wakapatwa na matatizo makubwa ya mgongo, kutia ndani kujipinda kwa uti, ikiwa watakuwa wakibeba mizigo ya namna hiyo kila siku wanapoenda shuleni. Wataalamu fulani wametoa mapendekezo kwa walimu-wakuu na walimu kwamba uzito wa mifuko inayobebwa mgongoni na wanafunzi isizidi asilimia 20 ya uzito wa mtoto au kwamba mifuko hiyo isafirishwe “kwa magurudumu, iwe na mishipi ya nyongani, na hata iwe na kitu laini mgongoni,” laripoti gazeti la Mexico City Excelsior.
Divai—Iliyodumu kwa Karne Tatu
Chupa mbili za divai zimepatikana katika vifusi vya jengo fulani la London lililoharibiwa mwaka 1682, laripoti The Times la London. Kizibo cha chupa moja kilikuwa kimeoza, na divai iliyokuwa ndani ilikuwa imebadilika na kuwa siki; lakini kizibo kile kingine kilichoshikiliwa na waya na nta, kilibaki kimefungika kabisa. Kwenye sherehe ya pekee ya kuonja divai iliyodhaminiwa na Jumba la Makumbusho la London, wataalamu wa divai walileta baadhi ya sampuli za divai hiyo ya karne nyingi zilizotolewa kutoka kwenye chupa kwa kutumia sirinji. Walifikia mkataa kwamba labda ilikuwa ni Madeira kavu, kisha wakasema kwamba ladha yake ilikuwa “ya asili, isiyoghushiwa, ilisisimua na kupendeza.”
Mito ya Ulimwengu Iko Hatarini
“Zaidi ya nusu ya mito mikuu ulimwenguni inakauka au inachafuliwa,” laripoti gazeti USA Today. Njia nyingi za majini “zimekaushwa na kuchafuliwa kabisa” kwa kutumiwa kupita kiasi na kutumiwa vibaya kwa ardhi na maji, yasema Tume ya Ulimwengu Kuhusu Maji kwa Ajili ya Karne ya 21. Kuchafuliwa kwa mali hizi za asili “kunatisha afya na riziki ya watu wanaoitegemea kwa ajili ya umwagiliaji-maji, kunywa na matumizi ya viwandani,” yasema tume hiyo. Inapendeza kwamba kati ya mito mikuu 500 ulimwenguni pote, miwili iliyo na “afya zaidi” ni Amazon ulioko Amerika Kusini na Kongo katika Afrika. Kwa sababu gani? “Yote miwili ina viwanda vichache karibu na kingo zake,” yasema ripoti hiyo.