Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuzuia “Busu” la Kifo

Kuzuia “Busu” la Kifo

Kuzuia “Busu” la Kifo

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA BRAZILI

Akukaribia usiku wa manane, ukiwa umelala fofofo. Hakuamshi. Wala huhisi chochote unapopewa “busu” lake lenye madhara.

MGENI huyu anayeingia usiku bila kukaribishwa ni mbawakavu aina ya barber ambaye husitawi Amerika Kusini—aitwaye pia mdudu abusuye. Mdudu huyo aweza kuendelea “kukubusu” kwa muda wa robo saa, huku akikunyonya damu polepole. “Busu” lenyewe halitakudhuru. Lakini kinyesi anachoacha ngozini mwako chaweza kuwa na kijiumbe kiitwacho Trypanosoma cruzi, au kwa ufupi T. cruzi. Kimelea hicho kikiingia mwilini mwako kupitia macho, mdomo, au kidonda, chaweza kusababisha maradhi ya American trypanosomiasis ambayo yajulikana kama maradhi ya Chagas.

Maradhi ya Chagas yanapokomaa, dalili yake iliyo rahisi zaidi kutambua ni kuvimba kwa jicho moja. Uchovu, homa, kupoteza hamu ya chakula, au kuhara kwaweza kufuata. Hatimaye, baada ya mwezi mmoja au miwili, dalili hizo hupotea—hata bila matibabu. Lakini hali mbaya zaidi huenda ikaja baadaye. Miaka 10 hadi 20 baada ya kuambukizwa maradhi hayo, mgonjwa huenda akapatwa na matatizo ya moyo, kutia ndani matatizo ya mpigo wa moyo, au hata moyo kushindwa kufanya kazi kama kawaida. *

Imekadiriwa kwamba watu milioni 18 wameambukizwa maradhi ya Chagas, na watu 50,000 hufa kila mwaka kwa sababu ya maradhi hayo. Ugonjwa huo hauambukizwi kwa kuumwa tu na mdudu huyo. Kwa mfano, baadhi ya walioambukizwa ni watoto walionyonyeshwa, ambao waliambukizwa na mama zao wenye ugonjwa huo. Mwanamke mjamzito hata aweza kumwambukiza mtoto wake tumboni, au kumwambukiza anapojifungua. Njia nyingine za kuambukizwa ni kupitia kutiwa damu mishipani au kula chakula kisichopikwa ambacho kimechafuliwa kwa kijiumbe cha T. cruzi. *

Ni nini kinachofanywa ili kukomesha maradhi ya Chagas? Dawa za kuua wadudu zimetumiwa kwa mafanikio kupunguza idadi ya mbawakavu aina ya barber. Hata hivyo kupiga dawa nyumbani kila baada ya miezi sita si jambo lenye kupendeza. Chuo Kikuu cha Serikali cha Rio de Janeiro kimevumbua kibadala—rangi yenye dawa ya kuua wadudu. Nyumba 4,800 zilipakwa rangi hiyo kama jaribio. Matokeo yakawa nini? Baada ya miaka miwili asilimia 80 ya nyumba hizo bado hazikuwa na wadudu wowote! Pia watafiti wamegundua kwamba majani ya mti uitwao neem, au mti wa cinamomo wa Brazili, yana dawa (Azadirachtin) isiyo na sumu na inayoweza kuvundishwa na bakteria. Dawa hiyo huponya mbawakavu wenye kimelea cha maradhi hayo, pia huwazuia mbawakavu ambao hawajaambukizwa, wasiambukizwe.

Msaada kwa Walioambukizwa

Je, kuna tumaini lolote kwa mamilioni ya watu ambao wameambukizwa maradhi ya Chagas? Lipo. Kikundi cha kimataifa cha wanasayansi kinajitahidi kuelewa muundo wa chembe za urithi 10,000 za T. cruzi. Huenda uchunguzi huo utawezesha kutengenezwa kwa vyombo vya kupima maradhi hayo, chanjo, na dawa zenye nguvu zaidi.

Mnamo Julai 1997, wanasayansi walipeleka mojawapo za protini muhimu za T. cruzi angani kwa chombo cha angani cha Columbia ili waweze kuchunguza muundo wake mahali penye kiasi kidogo sana cha nguvu za uvutano. Hiyo ni hatua ya kwanza katika kutokeza dawa zenye muundo kama wa T. cruzi. Kutafuta dawa mpya ni muhimu, kwa sababu dawa zipatikanazo leo hazitibu maradhi hayo yanapokomaa kabisa. *

Alipotambua umuhimu wa kuanza matibabu mapema, mwanabiolojia Constança Britto wa Brazili alivumbua aina ya upimaji wa utendanaji-mfuatano uitwao polymerase, ambao unawezesha kutambulisha maradhi hayo siku mbili tu baada ya kuambukizwa. Kwa kusikitisha, walio wengi hata hawajui kwamba wameambukizwa maradhi hayo hadi yanapokomaa.

Kuzuia Ni Bora

Mwishowe, unawezaje kujihadhari iwapo unaishi mahali ambapo pana mbawakavu aina ya barber?

▪ Iwapo unalala katika nyumba ya udongo au ya nyasi, jaribu kutumia chandalua ya kuzuia wadudu.

▪ Piga dawa za kuua wadudu. Hupunguza hatari ya kuambukizwa.

▪ Ziba mashimo na nyufa katika kuta na dari, kwani mbawakavu aina ya barber waweza kuzalia humo.

▪ Weka nyumba yako safi, kutia ndani nyuma ya picha za ukutani na fanicha.

▪ Mara kwa mara, anika magodoro na mablanketi juani.

▪ Kumbuka kwamba wanyama wote—wa mwituni na wa kufugwa— waweza kuwa na vimelea vya ugonjwa huo.

▪ Iwapo washuku kwamba mdudu ni mbawakavu aina ya barber, mpeleke kwenye kituo cha afya cha karibu ili achanganuzwe.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Dalili zatofautiana, na baadhi ya dalili za maradhi ya Chagas ni dalili za maradhi mengine pia. Kwa hiyo, dalili hizo ni za jumla wala hazikusudiwi kutumiwa ili kutambulisha ugonjwa huo. Watu wengi hawana dalili zozote hadi maradhi yafikiapo hatua ya kudumu.

^ fu. 6 Vitovu vya Kudhibiti na Kuzuia Maradhi vya Marekani vyataarifu kwamba katika nchi kadhaa damu haipimwi kwa ukawaida ili kuhakikisha kwamba haina maradhi ya Chagas.

^ fu. 10 Madaktari hutumia dawa ya nifurtimox kutibu T. cruzi, lakini mara nyingi hiyo huwa na athari mbaya sana.

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

Kugunduliwa kwa Maradhi ya Chagas

Mnamo mwaka wa 1909, daktari mmoja Mbrazili, Carlos Chagas alifanya kazi katika Jimbo la Minas Gerais nchini Brazili, ambamo malaria ilizuia ujenzi wa reli. Aliona kwamba wagonjwa wengi walikuwa na dalili za ugonjwa ambazo hazikuwa dalili za maradhi yoyote yaliyojulikana wakati huo. Aliona pia kwamba nyumba za sehemu hiyo zilijaa wadudu waitwao mbawakavu aina ya barber, ambao hula damu. Chagas alipochunguza kinyesi cha mdudu huyo aligundua kijidudu kipya. Alikiita Trypanosoma cruzi, kwa heshima ya rafiki yake, mwanasayansi Oswaldo Cruz. Kwa kufaa, maradhi hayo mapya yalipewa jina la Carlos Chagas kwa sababu ya uchunguzi kamili aliofanya, uliosababisha kugunduliwa kwa ugonjwa huo.

[Picha katika ukurasa wa 12, 13]

Mara nyingi nyumba za mashambani hujaa mbawakavu aina ya “barber”

[Hisani]

Picha: PAHO/WHO/P. ALMASY