Safiri Salama!
Safiri Salama!
“Kushusha wasafiri kutoka katika ndege kwa sababu ya onyo la hatari kwafanywa karibu kila juma,” yasema ripoti moja katika gazeti la USA Today. Ijapokuwa mara nyingi wasafiri hushushwa kwa sababu ya hitilafu ndogo au maonyo ya hatari yasiyo ya kweli, kushuka kutoka katika ndege kutakuwa rahisi ukifuata madokezo yafuatayo:
● VAA MAVAZI YAFAAYO. Vaa mavazi yenye kustarehesha na yasiyobana. Mavazi yapaswa kufunika sehemu kubwa ya mwili wako. Suruali ndefu, na nguo zenye mikono mirefu zapendekezwa. Vaa mavazi ya vitambaa vyenye nyuzi za asili, kama vile pamba, sufu, denimu, na ngozi. Mavazi ya sanisia, kama rayoni, poliesta, au nailoni (hasa soksi, fulana na kadhalika), yaweza kuyeyuka, na kuchoma vibaya mwili na miguu.
● JITAYARISHE AKILINI. Wazia utakachofanya wakati wa dharura. Baada ya kuketi, chunguza ilipo milango ya dharura, mbele yako na nyuma yako pia. Sikiliza maelezo ya usalama yatolewayo na mhudumu wa ndege kabla ya kuanza safari. Pitia kijitabu cha maelezo ya usalama kuhusu jinsi ya kushuka kutoka katika ndege wakati wa dharura.
● USIHOFU. Hali ya dharura ikitokea, tulia na ufuate maelekezo ya wahudumu wa ndege. Ikiwa ni lazima ushuke kutoka katika ndege, nenda kwa mlango wa dharura uliopo karibu nawe, acha mali yako.
● SHUKA KUTOKA KATIKA NDEGE KWA UANGALIFU. Ruka ndani ya daraja-telezi, wala usiketi ili kuteleza. Kunja mikono kifuani. Toa viatu vyenye visigino vyenye ncha kali, na uweke miguu pamoja. Unapofika chini, nenda mbali na ndege, huku ukiwa macho kupata magari ya dharura.
Je, kufuata miongozo hiyo kwaweza kupunguza idadi ya vifo katika aksidenti? Ndiyo! “Si aksidenti zote za ndege ambazo husababisha kifo,” chasema kijarida Intercom cha Shirika la Serikali Linalosimamia Vyombo vya Angani. Kisha chasema hivi: “Asilimia 50 ya watu wanaokufa katika aksidenti za ndege za abiria, wangeweza kunusurika kwa sababu aksidenti hizo si mbaya sana.”