Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Wahasiriwa wa Mateso Asanteni sana kwa kuchapisha makala “Msaada kwa Wahasiriwa wa Mateso.” (Januari 8, 2000) Ufahamu wenye kina na hisia-mwenzi zilizoonyeshwa katika makala hiyo zilinisaidia kuhusianisha habari hiyo na matatizo yangu binafsi.
B. R., Marekani
Nilipata ujumbe kutoka kwa rafiki yangu mmoja. Alisema tu: ‘Makala hiyo inanihusu. Tafadhali isome.’ Ujumbe huo ulinihuzunisha, kwa kuwa yeye ndiye aliyejifunza nami Biblia mapema katika miaka ya 1970. Sikujua kamwe kwamba alikuwa mhasiriwa wa mateso. Nimetulizwa kwa kuwa mlichapisha habari ya wazi kuhusu mvurugiko wa hisia wa wahasiriwa ambao wameteswa na wengine ulimwenguni pote.
L. W., Marekani
Wimbo Unaostahili Kukumbukwa Asanteni kwa makala fupi “Wimbo Asioweza Kuusahau.” (Desemba 22, 1999) Wimbo huo mzuri sana kwa kweli humsifu Yehova na kufanya machozi yatiririke. Franz Schubert hakuhofu kutumia jina kuu la Yehova.
K. C., Marekani
Twataka kuwafahamisha wasomaji wetu kwamba wimbo “Die Allmacht” (Opus 79, No. 2), ingawa waonekana kuwa wa kidini, haukutungwa kwa ajili ya kanisa. Yasemekana kwamba Schubert aliutunga kwa sababu alivutiwa na fahari ya milima alipokuwa Austria.—Mhariri.
Ubuni wa Asili Nimekuwa msomaji wa Amkeni! kwa muda wa miaka zaidi ya 30, lakini ninasukumwa kutoa shukrani yangu kwa ajili ya mfululizo wa makala “Uhai—Umetokana na Ubuni.” (Januari 22, 2000) Kwa kawaida sipendezwi sana na habari za kisayansi, lakini nilipendezwa mno na makala hizo zilizoeleweka kwa urahisi.
T. E., Marekani
Makala hizo ziliongeza upendo na uthamini wangu kwa Yehova. Sasa naweza kuona kwamba kuishi milele katika Paradiso hakutachosha kamwe. Sikuzote kutakuwapo mambo mapya ya ajabu ya kujifunza kuhusu Muumba wetu. Kujifunza hakutakoma kamwe.
J.R.A., Brazili
Katika ukurasa wa 7 inaonekana kana kwamba kuna kosa, mzungumziapo giaboksi ya nzi. Je, mlimaanisha kwamba giaboksi “huunganisha mabawa”?
P. S., Marekani
La, hatukumaanisha hivyo. Twaomba radhi. Tulitaka kusema kwamba huunganisha “injini” na mabawa—“injini” yarejezea misuli katika kifua ambayo hutumiwa kupigapiga mabawa.—Mhariri.
Nimefanya kazi katika idara ya utafiti ya kampuni moja kubwa ya kompyuta kwa miaka mingi, na nimependezwa kuiga ubuni upatikanao katika uumbaji. Lakini sikujua kwamba kuna sayansi maalumu inayoshughulikia jambo hilo, yaani biomimetics. Ni jambo la kusikitisha kwamba wengi wanaoiga ubuni tele ulio katika uumbaji hawamsifu Mbuni wa awali.
P. G., Marekani
Makala hiyo iliandikwa kwa njia bora ajabu. Baadhi ya watu ambao niliwapa makala hiyo walitoa maoni yanayofaa kuhusu jinsi Mungu anavyoweza kufanya kila kitu kwa ukamilifu bila uchafuzi. Asanteni kwa kazi yenu, mlifanya habari ngumu isomeke kwa urahisi.
R.D.S., Italia
Hatari za Internet Makala “Vijana Huuliza . . . Naweza Kuepukaje Hatari Katika Internet?” (Januari 22, 2000) ilionyesha maoni yaliyosawazika juu ya hatari za Internet na manufaa yake. Mimi ni mmojawapo wa wale wanaotumia Internet kila siku katika kazi yangu, nami huona hatari zake waziwazi. Jinsi ilivyo muhimu kuepuka hatari hizo!
J. L., Marekani