Twiga—Warefu, Wenye Miguu Mirefu, na Wenye Fahari
Twiga—Warefu, Wenye Miguu Mirefu, na Wenye Fahari
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA
MAJABALI ya matale yenye rangi ya kijivu yalikuwa na unyevu na ubaridi wakati wa alfajiri. Tulikaa kwa starehe miongoni mwa miamba hiyo, tukiwa na kikombe cha chai moto mikononi huku tukikazia macho mbuga ya Afrika kule chini. * Subira yetu ilithawabishwa. Katika mwangaza hafifu wa mapambazuko, kundi la twiga—warefu, wenye miguu mirefu, na wenye fahari—walivuka uwanda. Walitembea polepole, wakipiga hatua ndefu kwa miguu yao mirefu kama mironjo, huku shingo zao ndefu zilizopinda zikiyumbayumba kama milingoti ya meli upeponi. Karibu tuliacha kupumua. Mandhari hiyo ilipendeza sana!
Bila kujali kuwapo kwetu, twiga wote waligeuka kwa pamoja na kuelekea kwenye kijisitu cha mikakaya na kujinyosha hadi matawi ya juu yenye miiba. Kwa uangalifu, majitu hayo yenye upole yalichuma majani madogo ya kijani kibichi kwa ndimi zao ndefu. Kule juu, yaliingiza vichwa vyao katikati ya viota vya jamii ya ndege aina ya mnana na kuendelea kula majani kwa utulivu. Ndege hao walikaripia kwa kelele kubwa wavamizi hao wenye shingo ndefu. Twiga walishtushwa na kelele hizo, wakaondoka polepole kwa hadhi kuelekea miti mingine.
Mwenye Kasi na Mwenye Fahari
Mtu ambaye amewaona viumbe hao wakitokeza vichwa vyao katika kizimba cha bustani ya wanyama, huenda akaona vigumu kuwazia uzuri na fahari yao wanapokuwa katika mazingira yao ya asili wakiwa huru kabisa katika pori la Afrika. Mwendo wa twiga ni mwepesi na wa fahari. Wanapovuka shoti uwanda wa mbuga, waonekana wanyonge na dhaifu kana kwamba watajikwaa na kuanguka kwa sababu ya kikwazo kidogo tu. Kinyume cha hilo, twiga wa kiume mwenye uzito wa kilogramu 1,300 ni mkimbiaji mwepesi asiyeanguka kwa
urahisi awezaye kukimbia kwa mwendo wa kilometa 60 hivi kwa saa.Kiumbe huyu mwenye kuvutia hupatikana Afrika pekee. Upole na utulivu wake wamfanya awe mwenye kuvutia sana. Uso wa twiga wenye masikio marefu membamba na pembe mbili zinazofunikwa kwa manyoya meusi laini, waweza kutajwa kuwa wa kipekee na wa kufurahisha. Macho yake ni makubwa na meusi, na hukingwa na kope ndefu zenye kupindapinda. Twiga anapotazama mbali, uso wake unaonyesha udadisi usio na ubaya wowote.
Siku za kale, twiga alipendwa na kuthaminiwa kwa sababu ya sura yake ya kupendeza na yenye haya, utulivu wake, na upole wake. Watawala na wafalme walipewa twiga wachanga kama zawadi ili kuonyesha amani na urafiki kati ya mataifa. Leo picha zilizochakaa za twiga bado zapatikana katika michoro ya kale kwenye miamba ya Afrika.
Mrefu
Twiga ni mrefu kushinda wanyama wengine wote. Kutoka kwato hadi pembe, twiga wa kiume aliyekomaa aweza kufikia urefu wa meta tano na nusu. Katika maandishi ya picha ya Misri ya kale, picha ya twiga iliwakilisha kitenzi “kubashiri” au “kutabiri,” kwa sababu ya urefu wake wa kutisha na uwezo wake wa kuona mbali.
Anaposimama katikati ya makundi ya punda milia, mbuni, swalapala, na wanyama wengine wa mbuga za Afrika, twiga ni kama mnara wa mlinzi. Urefu wake na macho yake mazuri humwezesha kuona mbali na kutambua mapema hatari yoyoteinayokaribia.Kwahiyo, bila shaka kuwapo kwake huwafanya wanyama wengine wawe salama kwa kadiri fulani.
Uumbaji wa Ajabu
Twiga ameumbwa kwa njia bora sana ili aweze kutafuna matawi ya juu ya miti mirefu, ambayo hayafikiwi na wanyama wengine isipokuwa ndovu. Umbo la kipekee la mdomo wa juu wenye uwezo wa kushikilia kitu na ulimi unaonyumbulika
humwezesha kuchuma majani kutoka matawi yenye vishore na miiba mikali kama sindano.Twiga wanaweza kula kilogramu 34 hivi za majani kila siku. Ijapokuwa wanaweza kula mimea mbalimbali, hasa hupenda mikakaya ambayo imetapakaa katika mbuga za Afrika. Twiga wa kiume aweza kunyoosha ulimi wake kwa umbali wa sentimeta 42 anapotafuta chakula. Shingo ya twiga hunyumbulika isivyo kawaida. Hilo humwezesha twiga kugeuza kichwa chake kirefu pande zote akipitiapitia kwa uangalifu matawi ya juu ya miti.
Kufikia matawi ya juu ni jambo rahisi kwa twiga, lakini kunywa maji ni tatizo. Anapokaribia dimbwi, twiga huhitaji kupanua miguu ya mbele polepole na kupiga magoti ili ayafikie maji. Katika hali hii isiyovutia, twiga hunyosha kabisa shingo yake ili anywe maji. Jambo zuri ni kwamba twiga hahitaji kunywa maji mara nyingi, kwa kuwa anapata unyevu wa kutosha kutokana na majani yenye utomvu ambayo anakula.
Shingo na mabavu ya twiga yamechorwa mistari myeupe maridadi inayofanyiza mapambo yanayofanana na yale ya majani. Rangi yake ni ya hudhurungi hadi kahawia iliyoiva na hata nyeusi. Twiga azeekapo, rangi yake huzidi kuwa nyeusi.
Maisha ya Jamaa
Twiga hupenda kukaa na twiga wenzake, na wanaishi katika makundi yaliyo mbalimbali yenye wanyama 2 hadi 50. Twiga wa kike hubeba mimba kwa muda wa siku 420 hadi 468, kisha huzaa ndama mwenye kimo cha meta mbili. Wakati anapozaliwa, ndama huanguka kwa kichwa kwa umbali wa meta mbili hadi chini! Lakini baada ya dakika 15 mtoto, asiye na jeraha, anasimama kwa miguu isiyo imara, akiwa tayari kunyonya. Baada ya majuma mawili au matatu, ndama huyo aanza kutafuna-tafuna matawi machanga ya mkakaya na muda si muda hupata nguvu ya kutosha kwenda kwa mwendo sawa na mama yake.
Twiga mchanga afanana kabisa na wazazi wake. Ijapokuwa yeye ni mfupi akilinganishwa na twiga aliyekomaa, bado ni mrefu kuliko watu wengi. Kumwona ndama asiyeogopa na mwenye udadisi anayesimama wima kando ya mama yake mrefu aliye macho kwavutia sana.
Katika majira ya kuzaa, twiga wachanga hukusanyika pamoja katika vikundi na wanatumia wakati huo kupumzika, kucheza na kutazama mambo yanayoendelea. Ndama mchanga anakua haraka sana. Anaweza kukua kwa meta moja kwa muda wa miezi sita, na anaweza kukua kwa meta mbili katika mwaka wake wa kwanza. Katika juma moja tu ndama huenda akakua kwa sentimeta 23! Twiga wa kike humlinda sana mtoto wake, na hata ingawa anamruhusu kutembea mbali, uwezo wake mzuri wa kuona unamwezesha kumtazama.
Kwa sababu ya ukubwa, wepesi, na pia uwezo wake bora wa kuona, twiga hana adui wengine porini mbali na simba. Hata hivyo, mwanadamu amewawinda na kuwaua twiga wengi sana. Ameuawa bila huruma kwa sababu ya ngozi yake maridadi, nyama yake tamu, na nywele ndefu nyeusi za mkia wake—ambazo baadhi ya watu wanaamini zina nguvu za
kimizungu—na kwa sababu hizo wanyama hao watulivu wanaelekea kutoweka. Zamani za kale twiga walikuwa wengi sehemu mbalimbali za Afrika, siku hizi wanakaa salama tu katika mbuga za pekee na katika hifadhi za wanyama.Leo wageni wanaotalii Afrika bado waweza kusisimuka kuwaona twiga wenye shingo ndefu wakikimbia kwa uhuru katika nyanda pana sana zenye nyasi. Huko wanaweza kuwaona wakila matawi ya juu ya mkakaya ama wakitazama tu mbali kama wanavyozoea twiga. Mnyama huyo mwenye fahari, mwenye umbo maridadi la kustaajabisha na mpole, kwa kweli ameumbwa kwa njia ya ajabu sana—ni uthibitisho mwingine wa uwezo wa kubuni na utu usio na kifani wa Mungu mweza yote, Yehova.—Zaburi 104:24.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Vilima vidogo vyenye mawemawe vinavyotapakaa katika mbuga ya Afrika vyaitwa katika lugha ya Kiingereza kopje.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]
MWUJIZA WENYE SHINGO NDEFU
Umbo la ajabu la mwili wa twiga na ukubwa wake yamkini hutokeza matatizo—huenda mtu akadhani. Kuzungusha damu ili ifike sehemu zote za mwili kungeonekana kuwa jambo lisilowezekana kwa sababu ya urefu wake na shingo yake ndefu. Kwa mfano, wakati twiga anapoinamisha kichwa chake chini, nguvu za uvutano zingeelekeza damu yote kichwani, na kufurika ubongo. Twiga anapoinua kichwa chake, damu yote ingerudi kasi moyoni na kumfanya mnyama huyo azimie. Hata hivyo, hayo yote hayatukii. Kwa nini?
Mfumo wa mzunguko wa damu wa twiga kwa kweli umeumbwa kwa njia ya ajabu, na unafaa kabisa umbo la pekee la mwili wa mnyama huyo na ukubwa wake. Moyo wake ni mkubwa isivyo kawaida, na huhitaji kusukuma damu kwa nguvu hadi kwenye ubongo, ulio umbali wa meta tatu na nusu juu ya moyo. Moyo wake hupiga mara 170 kwa dakika, na moyo huo wenye kuta za misuli zenye unene wa sentimeta saba hutokeza msukumo unaozidi ule wa moyo wa mwanadamu kwa mara tatu hivi. Ili kustahimili msukumo huo wenye nguvu, mshipa upelekao damu ubongoni, na mshipa wa shingoni urudishao damu moyoni, lazima iwe mikubwa. Ndivyo ilivyo, kipenyo cha mishipa hiyo ya damu ni sentimeta 2.5 na imeimarishwa na tishu ngumu inayonyumbulika, ili iwe yenye kunyumbulika na yenye nguvu.
Twiga anapoinamisha kichwa chake, vilango vilivyo katika mshipa wa shingoni huzuia damu isiteremke kasi ubongoni. Chini tu ya ubongo, mshipa upelekao damu ubongoni unaingia katika kiungo ambacho kimeumbwa kwa njia ya ajabu ambacho huitwa utando wa pekee. Hapo msukumo wa nguvu wa damu kuelekea kwenye ubongo unaotokea wakati twiga anapoinamisha kichwa chake hupunguzwa kwa kuelekeza damu katika utando wa pekee wa mishipa midogo ya damu ambayo hudhibiti msukumo wa damu na kuzuia damu isiingie ubongoni kwa wingi na kwa nguvu. Utando huo wa pekee hupanuka kichwa kinapoinamishwa, na hupunguka twiga anapoinua kichwa chake, na hivyo kukabiliana na msukumo wa damu uliopungua sana na hatari ya kuzimia.
Shingo ya twiga pia ni ya ajabu. Wanasayansi walishangaa kugundua kwamba idadi ya mapingili ya uti wa mgongo katika shingo ndefu ajabu ya twiga ni sawa na ile ya shingo ya panya au karibu wanyama wengineo wote! Hata hivyo, tofauti na wanyama wengine wengi, mapingili ya uti wa mgongo wa twiga yamerefushwa kwa mpangilio wa kipekee wa mpira na tundu, ambao huifanya shingo yake inyumbulike. Kwa hiyo, twiga aweza kupinda shingo yake ili kusafisha manyoya ya kila sehemu ya mwili wake au kunyosha shingo hadi matawi ya juu kabisa ya mti ili kujilisha.