Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Waingereza na Anasa
Katika mwaka wa 1999, Waingereza kwa mara ya kwanza walitumia kiwango kikubwa zaidi cha pesa kila juma kununua vitu vya anasa na katika starehe kuliko walichotumia kwa “chakula, nyumba au uhitaji mwingine wowote wa familia,” laripoti gazeti Times la London. Katika mwaka wa 1968, ni asilimia 9 tu ya jumla ya pesa za matumizi ya familia iliyotumiwa kwa anasa ikilinganishwa na asilimia 17 inayotumiwa sasa. Mshauri wa wateja Martin Hayward asema hivi: “Kwa sababu ufanisi wa sasa unapita kwa mbali ule wa miaka 30 iliyopita, vitu vilivyoonekana pindi moja kuwa vya anasa sasa vyaonwa na watu wengi kuwa vya lazima. Kwenda likizo sasa kwaonwa na wengi kuwa ‘uhitaji wa lazima’ badala ya ‘starehe.’ Watu fulani hata huona kwenda likizo mara tatu katika mwaka kuwa uhitaji wa lazima.” Kiasi cha pesa kinachotumiwa na familia kununua vidio na vyombo vya sauti, televisheni, na kompyuta kimezidi kwa mara nne walichotumia kwa mambo hayo katika mwaka wa 1968. Kwa hakika, familia moja kati ya kumi inatumia Internet, na familia moja kati ya tatu ina kompyuta.
Kulala Kidogo Kunakoburudisha
Ile tabia ya kunywa kahawa ili kupambana na kusinzia wakati wa adhuhuri huenda ikawa na madhara, kulingana na gazeti la The New York Times. “Baada ya kunywa kahawa hali ya kuhisi uchovu hufuata,” anasema Dakt. James Maas, mtaalamu wa usingizi katika Chuo Kikuu cha Cornell. “Kiwango cha usingizi kinachohitajiwa na mwili wako hakipunguzwi na vichangamshi.” Badala ya kunywa kahawa wakati wa pumziko, Maas apendekeza kulala kidogo, ambako anasema “huchangia sana uwezo wa kukazia fikira mambo madogomadogo na uwezo wa kufanya maamuzi muhimu.” Kulala kidogo wakati wa adhuhuri, kwa muda usiozidi dakika 30, kwaweza kumtia mtu nguvu bila kumfanya aone ugumu wa kuamka wala kumfanya apoteze usingizi wakati wa usiku, lasema gazeti la Times. “Kulala kidogo hakupasi kupuuzwa,” asema Maas. “Kwapasa kuonwa kuwa sawa na mazoezi ya kila siku.”
Pamba Humea Mgongoni mwa Kondoo?
Kulingana na uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na Kamati ya Wakulima Chipukizi Katika Ulaya, “asilimia 50 ya watoto katika Jumuiya ya Ulaya hawajui sukari hutoka wapi, watatu kati ya wanne . . . hawajui pamba hutoka wapi, na zaidi ya robo yao wanaamini kwamba pamba hukuzwa mgongoni mwa kondoo.” Kwa kuongezea, asilimia 25 ya watoto wa umri wa kati ya miaka 9 na 10 katika Uingereza na Uholanzi wanaamini kwamba machungwa na zeituni hukuzwa katika nchi zao. Watoto hawaoni bidhaa za kilimo mashambani bali katika duka kuu, nao hujifunza mambo yanayohusu kilimo hasa shuleni. Hii huenda ikawa moja ya sababu kwa nini watoto wengi katika Ulaya hawapendelei kuwa wakulima. Kamati hiyo yaeleza kwamba “kwa wastani ni asilimia 10 tu ya watoto katika Jumuiya ya Ulaya ambao ‘wangependa sana’ kuwa wakulima wakati ujao.”
Urafiki Mashakani
Kufanya kazi kwa saa nyingi zaidi, safari nyingi za kibiashara, na vitumbuizo kwa njia ya elektroni “ambavyo hutuunganisha na mambo mengi isipokuwa watu” vinaathiri vibaya mahusiano ya kirafiki kati ya watu, laripoti jarida la The Wall Street Journal. Jarida hilo laendelea kusema kwamba “kuwa pamoja na marafiki kumepuuzwa na kuonwa kuwa jambo lisilo la lazima lenye kukatiza ratiba yenye shughuli nyingi.” Mwanasosholojia Jan Yager asema kwamba wale wanaopuuza marafiki huenda wakagundua kwamba hawana “mtu wa kuwaliwaza,” familia zao zipatwapo na msiba. Kwa upande mwingine, yaonekana uchunguzi unadokeza kwamba wale ambao wana marafiki wazuri kwa kawaida hawaathiriwi sana na mikazo na magonjwa na huenda wakaishi muda mrefu zaidi. Jarida hilo la Journal, laendelea kusema kwamba “ufunguo ni kutambua kwamba kudumisha urafiki hutaka jitihada sawa na ilivyo katika kusawazisha kazi na familia.”
Watoto Wanene Kupita Kiasi
Dakt. Chwang Leh-chii, mkuu wa shirika la wataalamu wa ulaji la huko Taipei, Taiwan aonya kuwa “kunenepa ni mojawapo ya matatizo makubwa zaidi ya kiafya yanayokabili vijana katika Asia.” Gazeti la Asiaweek laripoti kwamba kuna watoto wengi wanene kupita kiasi katika maeneo mengi ya Asia hasa miongoni mwa wavulana na watoto katika majiji. Uchunguzi wa hivi karibuni katika Beijing ulionyesha kwamba zaidi ya asilimia 20 ya watoto katika shule za msingi na za sekondari katika sehemu hiyo ni wanene kupita kiasi. Yaonekana kwamba vijana katika Asia wanatumia wakati mwingi zaidi na zaidi wakitazama televisheni
na kucheza michezo ya vidio, yasema ripoti hiyo. Ni nini laweza kufanywa? Kulingana na Asiaweek, suluhisho si kupunguza kiasi cha chakula kinacholiwa na watoto, badala yake, linalohitajika ni kufanya mazoezi ya kimwili kwa ukawaida na kula chakula chenye kufaa—chenye matunda na mboga nyingi badala ya makumbwe yenye mafuta mengi. Dakt. Chwang aliendelea kusema kwamba kufanya mazoezi ya kimwili yafurahishe kutasaidia sana. Ripoti hiyo yasema kwamba iwapo hawatabadili mazoea yao, huenda watoto wanene kupita kiasi wakapata ugonjwa wa shinikizo la damu, ugonjwa wa ini, ugonjwa wa sukari, na matatizo ya kiakili.Sinema na Kanisa
“Kwa vijana, sinema kama vile Terminator 2, Titanic na Star Wars huwapa uradhi mkubwa wa kiroho kuliko makanisa ya kawaida,” laripoti gazeti The Independent la London. Dakt. Lynn Clark, wa kitengo cha utafiti wa vyombo vya habari katika Chuo Kikuu cha Colorado, aliwauliza vijana 200 ni sinema gani iliyofanana na itikadi zao za kidini. Wengi wao walitaja Terminator 2, ambayo huonyesha vita kati ya mema na mabaya, huku mwigizaji mkuu akionyeshwa akiwa kwenye mandhari ya wakati uliopita, akifanya bidii kuokoa kitoto chenye kudhaniwa kuwa Mesiya. Akizungumza kwenye mkutano mmoja huko Edinburgh, Scotland, Dakt. Clark alimalizia kwa kusema hivi: “Vijana sasa wanamtazamia Darth Vader [mwigizaji mwovu sana katika Star Wars] na sinema ya X Files kutoa majibu kwa maswali kuhusu maana ya uhai. Sinema ya X Files huvutia sana kwa sababu huchunguza wazo lote la kuwapo kwa kani isiyojulikana inayoongoza ulimwengu wote. Hudokeza swala la kwamba kuna mambo ambayo hayajafafanuliwa na sayansi na ambayo hayashughulikiwi ifaavyo na dini.”
Uvutaji wa Sigareti Hufupisha Maisha
“Kila sigareti anayoivuta mtu hufupisha maisha kwa dakika 11,” charipoti kijarida cha University of California Berkeley Wellness Letter. Kulingana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Bristol, Uingereza, kuvuta katoni moja ya sigareti kungefupisha maisha ya mtu kwa siku moja na nusu, na kila mwaka anaovuta pakiti moja kwa siku, maisha yake yanapungua kwa miezi miwili hivi. Wanasayansi walipata takwimu hizo kwa kulinganisha miaka ambayo watu wanaovuta sigareti na wasiovuta sigareti wanatarajiwa kuishi. Watafiti hao walisema hivi: “Takwimu hizo zinaonyesha gharama kubwa inayotokana na uvutaji wa sigareti kwa njia inayoweza kueleweka na kila mtu.”
Tembo “Wasanii”
Huko Ottapalam, India, tembo wachanga wanafundishwa kuchora picha kwa kutumia mkonga wao kushika burashi. Wahifadhi wa mazingira wameanzisha Mradi wa Usanii na Hifadhi ya Tembo wa Asia ili kuchangisha pesa za kuwalinda tembo kwa kuuza picha zilizochorwa na tembo, laripoti gazeti la The Indian Express. Tembo mmoja wa miaka sita aitwaye Ganesan aonekana mwenye kufurahia sana “usanii” wake. Wakati anapotaka kuchora, yeye hutikisa masikio yake na kuchukua burashi kutoka kwa mwalimu wake. Ganesan hapendi kusumbuliwa anapochora, hataki ndege wala kindi wawe karibu. Baada ya kuchora sehemu fulani ya picha yenye kuvutia, Ganesan hutua na huonekana kana kwamba anaitafakari kazi yake. Hata hivyo, si tembo wote wachanga hupenda kuzoezwa kuwa wanyama “wasanii.” Baadhi yao huonyesha kutopendezwa kwao kwa kuvunja burashi za kuchorea.
Kupanga Wakati wa Kuzaa
Kwa mujibu wa gazeti Corriere della Sera, la Italia, “watoto wamejifunza kuzaliwa wakati hospitali inataka wazaliwe.” Katika mkutano mmoja kuhusu kuzaa uliofanyika hivi karibuni huko Florence Italia, Mswisi Fred Paccaud, ambaye ni daktari wa wanawake, alisema hivi: “Tangu karne ya 19, katika nchi za Magharibi, idadi ya watoto wanaozaliwa siku ya Jumamosi na Jumapili imeshuka kwa asilimia 95. Na si hilo tu: Tunaweza kusema kwa hakika kwamba watoto wengi huzaliwa kwenye masaa ya kazi, yaani wakati ambapo wengi wa madaktari na wauguzi wanapatikana.” Kuzaa huku huanzishwa ama kupitia dawa au upasuaji. “Tunajikuta tukizalisha kwa kutumia dawa au upasuaji,” asema Angelo Scuderi, ambaye ni daktari wa wanawake huko Florence. “Leo kuna ongezeko kubwa sana la wanawake wanaozaa kupitia upasuaji na zaidi ya asilimia 20 ya wanawake wanazaa kwa njia hiyo.” Hata hivyo, Profesa Carlo Romanini, msimamizi wa Sosaiti ya Jinakolojia na Ukunga ya Italia, adai kuwa “‘kupangia’ wakati wa kuzaa hakuwanufaishi madaktari tu” bali pia hulinda akina mama na watoto wao dhidi ya matatizo yasiyotazamiwa. Alisema kwamba “afadhali mtoto azaliwe wakati wafanyakazi wa hospitali wanapatikana ili kuhakikisha kwamba utunzaji mzuri iwezekanavyo unatolewa.”