Ulimwengu Wetu Wenye Kustaajabisha—Je, Ulitokea kwa Nasibu?
Ulimwengu Wetu Wenye Kustaajabisha—Je, Ulitokea kwa Nasibu?
BAADHI ya watu husema hivi: ‘Naam, ulimwengu wetu ulitokea kwa nasibu.’ Wengine, hasa watu wa kidini, hupinga wazo hilo. Na wengine hata hawana uhakika. Wewe je?
Haidhuru maoni yako, bila shaka utakubali kwamba ulimwengu wetu unastaajabisha. Fikiria magalaksi (makundi ya nyota). Imekadiriwa kwamba magalaksi yapatayo bilioni 100 yanaweza kuonekana. Kila galaksi ina idadi ya nyota inayopungua bilioni moja hadi zaidi ya nyota trilioni moja.
Magalaksi mengi ya nyota yamepangwa kwenye makundi makubwa zaidi yenye makumi machache hadi maelfu ya magalaksi. Kwa mfano, galaksi ya Andromeda iliyo karibu nasi imeelezwa kuwa pacha ya galaksi yetu ya Kilimia. Makundi hayo makubwa sana ya magalaksi yameunganishwa na nguvu za uvutano. Makundi hayo pamoja na makundi mengine madogo ya magalaksi yaliyo karibu hufanyiza kundi kubwa sana la magalaksi.
Kuna idadi isiyohesabika ya makundi makubwa ya magalaksi katika ulimwengu. Baadhi ya makundi hayo yameunganishwa na makundi mengine na nguvu za uvutano na kufanyiza makundi makubwa kupindukia ya magalaksi. Lakini nguvu za uvutano hupungua kadiri makundi yanavyokuwa makubwa. Wanasayansi wanagundua kwamba makundi hayo makubwa kupindukia yanatengana. Yaani, ulimwengu unapanuka. Ugunduzi huo wa kushangaza unadokeza kwamba kuna wakati ulimwengu ulikuwa mdogo sana na wenye kushikamana sana. Kwa kawaida ulimwengu husemwa kuwa ulitokana na mlipuko mkubwa.
Wanasayansi fulani wana shaka kuhusu uwezo wa mwanadamu wa kujua namna ulimwengu ulivyotokea. Wengine hukisia njia ambazo kupitia hizo ulimwengu wetu ungeweza kutokea pasipo kuumbwa na muumba mwenye akili. Jarida la Scientific American, katika toleo lake la Januari 1999, lilizungumzia kichwa “Ulimwengu Ulitoka Wapi?” Tayari nadharia kadhaa za wanasayansi zimethibitishwa kuwa na kasoro. “Kwa kusikitisha,” lasema gazeti hilo, “huenda ikawa vigumu sana . . . kwa wataalamu wa nyota kuthibitisha yoyote ya nadharia hizo.”
Dhana ya kwamba ulimwengu ulitokea kwa nasibu humlazimu mtu aamini kile
kinachoitwa na wanasayansi, “aksidenti [nyingi] za bahati” au “sadfa.” Mathalani, ulimwengu hufanyizwa kwa atomu nyingi sana sahili—za hidrojeni na heli. Lakini, uhai hautegemei hidrojeni tu bali hutegemea pia idadi kubwa ya atomu tata zaidi, hususa kaboni na oksijeni. Wanasayansi walikuwa wakishangaa kuhusu chanzo cha atomu hizo muhimu sana.Je, ni sadfa kwamba atomu tata sana zilizo muhimu katika kutegemeza uhai zinatengenezwa ndani ya nyota fulani kubwa? Na je, milipuko mikubwa ya baadhi ya nyota hizo kubwa ambayo husambaza shehena yake ya atomu adimu sana, hutokea kwa nasibu? Sir Fred Hoyle, aliyeshiriki katika ugunduzi huo, alisema hivi: “Mimi siamini kwamba mwanasayansi yeyote aliyechunguza uthibitisho huo angeshindwa kufikia mkataa wa kwamba sheria za fizikia ya nyuklia zimebuniwa kimakusudi.”
Basi acheni tuchunguze kwa makini zaidi kinachofanyiza ulimwengu wetu.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]
NADHARIA YA KUPANUKA
Wanasayansi fulani wanaamini kwamba hali fulani za ulimwengu wa kale, kama vile kiwango chake barabara cha kupanuka, zaweza kufahamika bila uhitaji wa muumba mwenye akili. Wanatumia ile inayoitwa nadharia ya kupanuka kwa ulimwengu. Hata hivyo, nadharia ya kupanuka kwa ulimwengu haielezi chanzo cha ulimwengu. Inategemea kuamini kitu kilichokuwako tayari ambacho kilitokeza ulimwengu wetu kwa nasibu.
Kulingana na nadharia ya kupanuka kwa ulimwengu, ulimwengu ulikuwa mdogo sana zaidi ya atomu kisha ukapanuka na kuwa mkubwa sana kupita galaksi yetu kwa muda usiozidi sekunde moja. Yasemekana kwamba tangu hapo, ulimwengu uliendelea kupanuka polepole kwa kiwango cha kawaida. Leo, sehemu tunayoweza kuona ya ulimwengu husemwa kuwa kisehemu kidogo mno cha ulimwengu wote mzima. Watetezi wa nadharia ya kupanuka kwa ulimwengu hudai kwamba ingawa sehemu ya ulimwengu tunayoweza kuona ina muundo taratibu, sehemu kubwa tusiyoweza kuona yaweza kuwa tofauti, au hata shaghalabaghala. “Nadharia ya kupanuka kwa ulimwengu haiwezi kamwe kuthibitishwa kwa kuona,” asema mtaalamu wa fizikia ya nyota Geoffrey Burbidge. Kwa kweli, nadharia ya kupanuka kwa ulimwengu inapingana na uthibitisho mpya unaoonekana. Sasa yaonekana kwamba endapo nadharia hiyo ingekuwa kweli, tungehitaji kukisia kuwapo kwa nguvu mpya inayopingana na nguvu ya uvutano. Mwanasayansi mmoja, Howard Georgi wa Chuo Kikuu cha Harvard, alisema kwamba nadharia ya kupanuka ni “ngano nzuri ya kisayansi, ambayo kwa ufupi yafanana na ngano nyingine yoyote ya uumbaji niliyopata kusikia.”
[Picha katika ukurasa wa 3]
Karibu kila kitu katika picha hii iliyopigwa na Darubini ya Angani ya Hubble ni galaksi
[Hisani]
Ukurasa wa 3 na 4 (picha zenye ukungu): Robert Williams and the Hubble Deep Field Team (STScI) and NASA
[Picha katika ukurasa wa 4]
“Sheria za fizikia ya nyuklia zimebuniwa kimakusudi.”—Sir Fred Hoyle, pamoja na mlipuko mkubwa wa nyota nambari 1987A
[Hisani]
Dr. Christopher Burrows, ESA/STScI and NASA
Photo courtesy of N. C. Wickramasinghe