Maajabu na Mafumbo Katika Bahari
Maajabu na Mafumbo Katika Bahari
WANASAYANSI wawili na rubani wao waliingia ndani ya Bahari ya Pasifiki karibu na pwani ya Ekuado, wakiwa ndani ya chombo kidogo cha kuzamia baharini kinachoitwa Alvin. Walikuwa wakielekea wapi? Mahali panapoitwa Bonde la Ufa la Galápagos. Chombo cha Alvin chenye taa zenye mwanga mkali, kamera, na vifaa kadhaa vya kisayansi, kilijitosa kina cha meta 2,800 baharini katika giza tititi ambalo halijawahi kuonwa na wanadamu.
Je, umewahi kujiuliza ni nini kilichofichwa milimani, makorongoni, na kwenye mabonde yaliyo chini ya vilindi vyenye giza vya bahari zote ulimwenguni? Ikiwa ndivyo, basi utafurahia kusoma kuhusu ugunduzi ulioanza mwaka wa 1977 wakati chombo cha Alvin kilipojitosa baharini kwa mara ya kwanza kama ilivyotajwa hapo awali. Yamkini utashangazwa na mambo waliyoona waliokuwa chomboni; hata kwa wanasayansi mahiri sana ilikuwa ni kama kugundua uhai katika sayari nyingine.
Kusudi la safari ya chombo cha Alvin lilikuwa kutafuta chemchemi za maji moto—chemchemi zilizo chini ya bahari zinazomimina michirizi ya maji moto baharini. Bonde la Ufa la Galápagos lilifaa kwa sababu ni sehemu ya bonde lililo baharini lenye utendaji mkubwa wa volkano, ambalo limezingirwa na safu tata ya milima inayozunguka ulimwenguni pote, inayoitwa safu ya milima iliyo katikati ya bahari. Safu hiyo ndefu ajabu yenye urefu wa mlalo wa zaidi ya kilometa 65,000, hujipinda-pinda na kuzunguka dunia yote kama mshono ulio kwenye mpira wa tenisi. Kama haingefunikwa na bahari, “mara moja [ingekuwa] sehemu kubwa zaidi katika uso wa dunia, ikisambaa kwenye eneo linalozidi eneo linalofunikwa na safu zote kubwa za milima duniani,” aandika Jon Erickson katika kitabu chake kiitwacho Marine Geology.
Sehemu yenye kutokeza hasa ya safu ya milima iliyo katikati ya bahari ni kwamba kwa kweli ni safu mbili—safu mbili za milima zilizo sambamba na zenye kimo cha meta 3,000 kutoka kwenye sakafu ya bahari. Kati ya safu hizo kuna nyufa kubwa zaidi duniani—makorongo yenye upana wa kilometa zipatazo 20 na kina cha kilometa 6—zenye kina ambacho ni mara nne zaidi ya kina cha lile Korongo Kuu la Amerika Kaskazini! Milipuko mikali ya volkano hutukia chini ya nyufa hizo zilizo bondeni. Wanasayansi walipochunguza kwa mara ya kwanza sehemu ya safu hiyo ya milima kwenye Bahari ya Atlantiki, inayoitwa Safu ya Milima Iliyo Katikati ya Atlantiki, vifaa vyao vilifunua milipuko mikali ya volkano “hata ilionekana ni kana kwamba sehemu ya ndani ya Dunia ilikuwa ikitoka nje,” asema Erickson.
Baada ya kushuka kwa muda wa dakika 90, chombo cha Alvin kilianza kwenda sambamba na sakafu ya bahari, kisha wanasayansi waliokuwamo wakawasha taa. Inaeleweka ni kwa nini walidhani kwamba walikuwa katika sayari nyingine. Taa zao zilimulika matundu kadhaa yenye maji moto yanayomeremeta kwenye sakafu ya bahari, ambako kwa kawaida maji hukaribia kuwa barafu. Karibu na matundu hayo, jambo lenye kustaajabisha hata zaidi lilitokea—jamii nzimanzima za viumbe ambao hawakuwa wamejulikana awali waliibuka. Miaka miwili baadaye, watafiti waliokuwa katika Alvin waligundua matundu yenye maji moto kupindukia yanayoitwa smokers katika Safu ya Milima ya Pasifiki Mashariki karibu na pwani ya Mexico. Baadhi ya matundu hayo hufanyiza mabomba ya ajabu, mengine hufikia kimo cha meta sita. Baadhi ya wanyama wengi walioonekana katika Bonde la Ufa la Galápagos waligunduliwa mahali hapo. Katika makala ifuatayo, tutachunguza kwa makini zaidi viumbe hawa wenye kustaajabisha na mazingira yenye hali zinazopita kiasi wanamoishi viumbe hao.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
JALADA na ukurasa wa 3: OAR/National Undersea Research Program