Je, Umewahi Kukutana na Xoloitzcuintli?
Je, Umewahi Kukutana na Xoloitzcuintli?
Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Mexico
MARA ya kwanza nilipomgusa Xoloitzcuintli *—au Xolo kwa ufupi—nilishangaa sana. Mwili wake mweusi usiokuwa na manyoya ulikuwa laini sana na moto! Mbwa huyo hodari wa maonyesho alimfuata mmiliki wake kwa fahari, hivyo tukapata fursa ya kutazama mwili wake mwembamba uliorembwa na ncha nyeupe ya mkia inayoshabihi “brashi ya kupakia rangi”—ilitofautiana sana na mwili wake mweusi ulio laini!
Kabla ya kuwasili kwa Wahispania, mbwa walithaminiwa sana wakiwa wanyama-vipenzi huko Mesoamerika. Baadhi yao walizikwa na wamiliki wao, ili wawe ‘waandamani katika maisha ya baada ya kifo.’ Mbwa aina ya Xolo walikuwa muhimu sana katika jamii. Iliaminika kwamba walikuwa muhimu kwa tiba. Naam, ilionekana kwamba kumgusa mwandamani huyu mdogo mwenye joto kuliwasaidia wale waliougua baridi-yabisi. Bila shaka, Xolo angeweza kupasha joto miguu yako katika usiku wenye baridi!
Leo, wengi humwona Xolo kuwa mnyama-kipenzi anayefaa kabisa. Kama mbwa wengineo wengi, Xolo waweza kuzoezwa nao huwa na ukubwa mbalimbali—hata kuna jamii moja ya mbilikimo. La maana zaidi ni kwamba, Xolo hawana viroboto kwa sababu hawana manyoya, nao wanawafaa kabisa wale wenye mzio wa manyoya ya mbwa. Kumtunza Xolo ni jambo rahisi sana. Ili kudumisha ngozi ya mbwa huyo ikiwa laini, ni muhimu kumpaka mafuta ya ngozi mara kwa mara. Miguel Ángel Moreno, mfugaji wa mbwa, ataja faida nyingine ya Xolo: “Kumwosha kunachukua dakika moja tu,” asema, “naye hukauka kwa dakika mbili.” Vipi juu ya umuhimu wa Xolo kimatibabu? Hata leo, watu fulani husema kwamba maumivu yao ya baridi-yabisi hutulia wanapoegemeza kiungo cha mwili kinachouma karibu na Xolo. Hata hivyo, Moreno anaamini kwamba Xolo huponya kama “chupa ya maji moto.” *
Miaka michache iliyopita Xolo walionwa kuwa wanyama walio katika hatari ya kutoweka, lakini jitihada kubwa imefanywa ili kuhifadhi mnyama huyu. Leo, Xolo waweza kupatikana si Mexico tu bali pia katika nchi nyingine, kama vile Peru na Marekani. Basi je, ungependa kukutana na Xoloitzcuintli? Iwapo utawahi kukutana naye, hutamsahau mbwa huyu wa pekee sana.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Hutamkwa soloiskwintli.
^ fu. 5 Joto la mwili wa Xolo si juu zaidi ya mbwa wengineo wote, lakini ukosefu wake wa manyoya humfanya mtu ahisi joto zaidi anapomgusa.