Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Uchaguzi Wako wa Matibabu—Je, Ni Muhimu?

Uchaguzi Wako wa Matibabu—Je, Ni Muhimu?

Maoni ya Biblia

Uchaguzi Wako wa Matibabu—Je, Ni Muhimu?

MARADHI na majeraha ni mambo ya kawaida kwa wanadamu. Wanapokabili maadui hao wa afya, wengi hutafuta kitulizo kwa matibabu. Yesu Kristo alitambua manufaa ya jitihada hizo alipokiri kwamba “wale walio na afya hawahitaji tabibu, bali wale wenye kuugua.”—Luka 5:31.

Mwandishi wa Biblia aliyeandika maneno hayo, Luka, alikuwa tabibu. (Wakolosai 4:14) Labda mtume Paulo alinufaika na ujuzi wa matibabu wa Luka walipokuwa wakisafiri pamoja. Lakini je, Maandiko hutoa mwongozo kuhusu aina ya matibabu yanayowafaa Wakristo? Je, uchaguzi wako wa matibabu ni muhimu?

Mwongozo wa Kimaandiko

Biblia yaweza kumwongoza mtu anapofanya maamuzi yenye hekima kuhusu matibabu. Mathalani, Kumbukumbu la Torati 18:10-12 husema waziwazi kwamba mazoea kama vile uaguzi na uchawi ni “chukizo” kwa Yehova. “Zoea la uwasiliani-roho,” ambalo Paulo alionya dhidi yake, latia ndani mambo hayo yaliyokatazwa. (Wagalatia 5:19-21) Kwa hiyo, Wakristo wa kweli huepuka utaratibu fulani wa kubaini ugonjwa au wa matibabu ambao kwa wazi huhusisha uwasiliani-roho.

Biblia pia hufunua jinsi Muumba anavyothamini sana utakatifu wa uhai na damu. (Mwanzo 9:3, 4) Huku wakiwa wameazimia kutii amri ya ‘kuendelea kujiepusha na damu,’ Mashahidi wa Yehova hukataa matibabu ambayo hukiuka amri ya Biblia ya kujiepusha na damu. (Matendo 15:28, 29) Hilo halimaanishi kwamba wanakataa matibabu yote. Badala yake, wao hutafuta matibabu bora zaidi kwao na kwa watoto wao. Lakini wao huwasihi wanatiba wawape matibabu ambayo hupatana na usadikisho wao wa kidini.

Angalia Sana Uendavyo

Mfalme Solomoni alionya kwamba “mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.” (Mithali 14:15) Hata kama uamuzi wa matibabu haupingani moja kwa moja na kanuni za Biblia, mtu apaswa ‘kuangalia sana aendavyo.’ Si matibabu yote yanayosaidia. Yesu aliposema kwamba ‘wale wenye kuugua wanahitaji tabibu,’ hakuwa akiidhinisha matibabu yote yaliyokuwapo siku hizo. Alijua kwamba matibabu fulani yalikuwa halali ilhali mengine yalikuwa bandia. *

Hali kadhalika leo, matibabu fulani yaweza kuwa ovyo, hata ya ulaghai. Kushindwa kufanya uamuzi mzuri kwaweza kumhatarisha mtu isivyofaa. Lazima pia ieleweke kwamba matibabu yanayomsaidia mtu mmoja yaweza kuwa yasiyomfaa—hata yenye kumdhuru—mwingine. Mtu mwenye busara anapokabili uamuzi wa kitiba, atafikiria uchaguzi wake kwa uangalifu badala ya ‘kuamini kila neno,’ hata anapopokea ushauri kutoka kwa marafiki wenye nia njema. Atadhihirisha “utimamu wa akili” kwa kutafuta habari yenye kutegemeka ili kuweza kufanya uchaguzi unaotegemea ujuzi.—Tito 2:12.

Ona Mambo Kihalisi na Ukubali Sababu

Inafaa kuhangaikia afya yako. Kutunza kwa usawaziko hali njema ya kimwili huonyesha uthamini kwa zawadi ya uhai na Chemchemi yake ya kimungu. (Zaburi 36:9) Ingawa watajitahidi kupata matibabu yafaayo, Wakristo watahitaji kusawazika katika masuala ya afya. Kwa mfano, ikiwa mtu mwenye afya ya kadiri atajishughulisha kupita kiasi na afya na hali njema, hilo laweza kumfanya ashindwe kuzingatia “mambo yaliyo ya maana zaidi.”—Wafilipi 1:10; 2:3, 4.

Mwanamke mmoja aliyekuwa mgonjwa sana siku za Yesu “alikuwa ametumia mali zake zote” akitafuta msaada wa matabibu ili wamtibu ugonjwa wake wenye kudumu. Matokeo yalikuwa nini? Badala ya kuponywa, hali yake ikawa mbaya zaidi, jambo ambalo bila shaka lilimfadhaisha sana. (Marko 5:25, 26) Alifanya juu chini kupata kitulizo, lakini hakufua dafu. Hali yake yaonyesha mipaka ya sayansi ya tiba nyakati hizo. Hata leo, licha ya maendeleo katika utafiti wa tiba na tekinolojia, watu wengi hujikuta katika hali iyo hiyo. Kwa hivyo ni muhimu kuwa na maoni halisi kuhusu yale ambayo yanaweza kutimizwa na sayansi ya tiba. Afya bora kabisa haiwezi kupatikana sasa. Wakristo hutambua kwamba wakati wa Mungu wa “kuponya mataifa” haujafika bado. (Ufunuo 22:1, 2) Kwa hiyo, ni lazima tusitawishe mtazamo uliosawazika kuhusu matibabu.—Wafilipi 4:5.

Ni dhahiri kwamba machaguzi tunayofanya ni muhimu. Kwa sababu hiyo, tunapolazimika kufanya uamuzi kuhusu matibabu, uchaguzi wetu wapasa kuonyesha tamaa yetu ya kuwa na afya bora na tamaa ya kudumisha uhusiano mzuri na Mungu. Tunapofanya hivyo, twaweza kuendelea kutazamia kwa uhakika utimizo wa ahadi ya Yehova ya kwamba katika ulimwengu mpya mtukufu unaokuja, “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Kwa mfano, katika ensaiklopedia ya kitiba ya karne ya kwanza ya Dioscorides, matibabu yaliyokusudiwa kuponya homa ya nyongo ya manjano yalikuwa kunywa mkorogo wa divai na kinyesi cha mbuzi! Bila shaka, sasa twajua kwamba dawa ya aina hiyo huenda ingezidisha maumivu ya mgonjwa.

[Picha katika ukurasa wa 26]

“The Doctor,” 1891, ilichorwa na Sir Luke Fildes

[Hisani]

Tate Gallery, London/Art Resource, NY