Dhahabu Iliyohamisha Milima
Dhahabu Iliyohamisha Milima
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Hispania
“Mchongo wa udongo wa mfinyanzi wenye minara mingi mirefu umechongwa mlimani. Jambo hilo lilisababishwa na Waroma na utafutaji dhahabu. Kupita kwa wakati na umaridadi wa michongo hiyo kumefanya kosa lao lisahauliwe.” —Pedro García Trapiello.
KASKAZINI-MAGHARIBI mwa Hispania mna mchongo wa ajabu uliofanyizwa kwa jiwe-mchanga la kidhahabu. Miti ya chestinati ambayo imefunika eneo lote hudanganya kwamba magenge na minara hiyo mirefu imefanyizwa kiasili. Vijia vya kuingia ardhini ndivyo tu hufunua siri ya zamani sana. Hapa, mahali ambapo leo huitwa Las Médulas, wakati mmoja palikuwa na mgodi mkubwa zaidi wa dhahabu katika Milki ya Roma.
Dhahabu imekuwa daima ikiwavutia wanadamu na kuwachochea kufanya jitihada kubwa ili kuipata. Kitabu cha Biblia cha Ayubu hueleza jinsi ‘wanadamu walivyofukua mashimo na kuipindua milima hadi kwenye misingi yake na kukata mifereji kati ya majabali’ wakitafuta dhahabu, fedha, na vito vya thamani milenia nyingi zilizopita.—Ayubu 28:1-10.
Roma ilipokuwa ikitawala dunia karne nyingi baadaye, dhahabu ilikuwa bado na thamani kubwa. Maliki Augustus alitamani uchumi wenye ufanisi, na dinari ya fedha na aureus ya dhahabu zilikuwa sarafu muhimu alizohitaji ili kusitawisha biashara ya Roma. Bila shaka, alihitaji dhahabu na fedha ili kutengeneza sarafu za kutosha. Ndiposa, wenye kutafuta-tafuta dhahabu walifika eneo fulani muda mfupi tu baada ya majeshi ya Roma kulitiisha.
Majeshi ya Roma yalipotiisha eneo la kaskazini-magharibi mwa Hispania, karibu mwanzo wa Wakati Wetu wa Kawaida, waligundua hifadhi mpya ya dhahabu. Kwa kusikitisha, kito hicho cha thamani, kilifunikwa na mlima mkubwa wa matope na haikuwa rahisi kuifikia dhahabu hiyo. Ingechukua muda wa karne mbili u nusu wa kazi ya kisulubu ili kufukua hazina hiyo.
Hata hivyo, Waroma hawakukata tamaa. Wafanyakazi walipatikana kwa urahisi, na mbinu za wakati huo za kuchimba dhahabu—ingawa za sulubu—zilikuwa na mafanikio. Walinuia kufukua dhahabu hiyo kwa kumomonyoa mlima kwa maji hatua kwa hatua. Ili kutimiza hilo, walijenga zaidi ya mifereji 50 ya maji, mabwawa kadhaa makubwa kwenye miinuko ya milima na kuchimba vijia vya chini ya ardhi vyenye urefu wa mamia ya kilometa.
Mara tu baada ya uchimbaji wa mfumo wa vijia vya chini kukamilika katika sehemu moja ya mlima, wahandisi walishinikiza vijia hivyo vyote kwa maji. Maji hayo yenye kwenda kasi yalimomonyoa tani nyingi za udongo. Mchanga na mawe yenye kuchanganyikana na dhahabu ulipelekwa hadi sehemu ya chini ya mlima, ambapo dhahabu ilitenganishwa kwa kusafisha mchanga katika sinia na kuchuja. Kazi hiyo ilirudiwa tena katika sehemu nyingine ya mlima kwa kuchimba vijia vingine chini ya ardhi.
Je, kazi hiyo ya kisulubu ilifanikiwa? Kwa saburi, Waroma waliweza kupata tani 800 hivi za dhahabu kutoka Las Médulas. Ili kupata kiasi hicho cha dhahabu, ilibidi maelfu ya wafanyakazi wahamishe milima kihalisi—zaidi ya kyubiki-meta milioni 240 za udongo. Na kwa kila tani 10 za udongo walipata gramu 30 za dhahabu.
Leo, hakuna kitu kilichosalia ila vijia vya chini ya ardhi na magofu ya mlima ambao umemomonyolewa na maji kisha kufunikwa na miti ya chestinati. Kinyume cha hilo, matunda matamu ya chestinati yaliyoletwa Hispania na Waroma yamedumu huko kuliko dhahabu.
[Picha katika ukurasa 22]
Sarafu ya dhahabu (“aureus”) inayoonyesha kichwa cha Maliki Augustus
[Picha katika ukurasa 23]
Las Médulas, eneo lililokuwa na mgodi mkubwa zaidi wa dhahabu katika Milki ya Roma
[Picha katika ukurasa 23]
Sehemu ya mfumo wa kale wa vijia vya chini ya ardhi
[Picha katika ukurasa 23 zimeandaliwa na]
Sarafu zote: Musée de Normandie, Caen, France