Unapokumbwa na Ugonjwa
Unapokumbwa na Ugonjwa
John, baada ya kugundua kwamba alikuwa na ugonjwa wenye kudhoofisha—“Nilishtuka sana.”
Beth, baada ya kufahamu hatari ya ugonjwa wake.—“Nilihofu sana.”
KUFAHAMU kwamba una ugonjwa wa kudumu au wa kulemaza au kufahamu kwamba utalemaa kabisa kwa sababu ya majeraha uliyoyapata katika aksidenti ni mojawapo ya mambo yenye kuhuzunisha zaidi maishani. Iwe utapokea habari za ugonjwa wako katika ofisi tulivu ya daktari au utagundua ulemavu wako katika chumba cha tiba ya dharura chenye hekaheka, yamkini utapigwa na bumbuazi. Maisha hayakutayarishi kukabiliana na hisia-moyo kali zinazokukumba wakati unaposhikwa na tatizo baya sana la kiafya.
Ili kukusanya habari ambazo zaweza kuwasaidia wale ambao afya yao imezorota vibaya hivi karibuni, Amkeni! liliwahoji watu kadhaa kutoka nchi mbalimbali ambao wamekabiliana kwa mafanikio na ugonjwa wa kudumu wenye kulemaza kwa miaka mingi. Waliombwa watoe maoni yao kwa maswali kama vile: Ulihisije? Ni nini kilichokusaidia ustahimili tatizo hilo na kupata usawaziko tena? Ulichukua hatua gani ili kudhibiti tena maisha yako kwa njia fulani? Habari yenye kuarifu kutoka kwa mahoji hayo ya moja kwa moja na vilevile matokeo ya watafiti ambao wanachunguza athari za magonjwa ya kudumu yameandikwa ili kuwanufaisha wale wanaokabili ugonjwa hivi sasa. *
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Ingawa mfululizo huu unaelekezwa hasa kwa wale walio wagonjwa au walemavu, mfululizo “Ugonjwa wa Kudumu—Kukabiliana Nao Mkiwa Familia” (Gazeti la Amkeni! la Mei 22, 2000) ulikuwa na habari iliyoelekezwa hasa kwa wale ambao wanawatunza wagonjwa.