Fumbo la Korobindo wa Uingereza
Fumbo la Korobindo wa Uingereza
Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Uingereza
KOROBINDO mwenye kuenea sana, anayejulikana kwa sauti yake nyororo, amekuwa akionekana kwa ukawaida nchini Uingereza. Lakini sasa anatoweka—mara nyingi kwa ghafula—katika sehemu za mijini, na hakuna ajuaye sababu. Gazeti Independent la London limetoa zawadi ya dola 5,000 za Marekani (pauni 7,200 za Uingereza) kwa mtu yeyote atakayekuwa wa kwanza kuandika insha ya kisayansi itakayotatua fumbo hilo. Shirika la Royal Society for the Protection of Birds na shirika la British Trust for Ornithology litachunguza insha hiyo. Mradi huo watazamiwa kuchukua miaka miwili hivi ili kukamilishwa.
Uchunguzi waonyesha kwamba idadi ya korobindo imepungua sana katika miji na majiji kote nchini. Katika maeneo mengine wametoweka kabisa. Hata hivyo, korobindo wangali wengi sana katika majiji mengine ya Ulaya, kama vile Paris na Madrid. Dakt. Denis Summers-Smith, mtaalamu wa korobindo, asema hivi: ‘Ni mojawapo ya mafumbo ya ajabu ya wanyama-mwitu katika miaka 50 iliyopita.’
Inasemekana kwamba kupungua kwa idadi ya korobindo kwa asilimia 65 katika sehemu za mashambani kumesababishwa hasa na kilimo kinachofanywa kwa kiwango kikubwa. Aina nyingine za ndege zimepungua sana vilevile huko mashambani. Lakini hilo halielezi kwa nini korobindo wamepungua kwa asilimia 92 sehemu za mijini. Mwanamazingira Michael McCarthy amalizia kwa kusema kwamba kutoweka kwa korobindo “kwaonyesha hakika kwamba kuna kasoro kubwa sana katika mfumikolojia wa korobindo—na labda wetu pia.” Twatumaini kujua hasa kuna kasoro gani na ni mbaya kadiri gani.